Mkutano Mkuu
Mwaminifu hadi Mwisho
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Mwaminifu hadi Mwisho

Kwa mkono Wake, utaweza kumuangusha kila Goliathi ajaye katika maisha yako.

Wapendwa marafiki wadogo, leo ningependa kuzungumza nanyi moja kwa moja—vijana wa Kanisa.

Ni mwaka sasa tangu Urais wetu Mkuu wa Wasichana ulipoitwa. Ni mengi kiasi gani yametokea katika mwaka huu uliopita!

Tumekutana na wengi wenu na kujifunza mafundisho ya Kristo pamoja. Tumeimba nyimbo, tumetengeneza marafiki wapya na kutumikia pamoja nanyi katika jamii zetu. Tumeimarishwa kwa kusikiliza shuhuda zenu kwenye mikutano ya vijana na matukio ya ulimwengu. Na tumeabudu pamoja katika nyumba ya Bwana.

Kila mara, tumeshiriki ujumbe kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Usiku wa leo hauna tofauti; nina ujumbe kwa ajili yenu, enyi vijana wa Kanisa la Yesu Kristo.

Swali la Msingi

Je, umeshawahi kujiuliza jinsi ya kuwa mwaminifu kwa Mungu wakati mkiishi katika ulimwengu wa dhambi? Mnapata wapi ujasiri wa kusonga mbele na kuendelea kutenda mema? Mnapataje shangwe ya kweli?

Nadhani uzoefu wa Daudi na Goliathi unaweza kusaidia.

Daudi na Goliathi

Katika Agano la Kale, jeshi la Wafilisti lilikuwa likipigana na Waisraeli, na kila asubuhi na kila jioni, Mfilisti mmoja shujaa aitwaye Goliathi aliwatishia Waisraeli wapigane naye.

Picha
Daudi na Goliathi.

Miongoni mwa watu wa Israeli alikuwa ni Daudi, kijana mchunga kondoo mdogo sana kuliko Goliathi lakini mwenye imani kubwa katika Yesu Kristo! Daudi alijitolea kupigana. Hata mfalme alijaribu kumzuia, lakini Daudi alichagua kuweka tumaini lake katika Yesu Kristo.

Hapo awali, Daudi alipigana na simba na dubu pia. Kutoka kwenye uzoefu wake mwenyewe, alijua kwamba Mungu amemlinda na kumfanya mshindi. Kwa Daudi, dhumuni la Mungu lilikuwa dhumuni la msingi sana. Hivyo, akiwa amejaa imani kwa Mungu ambaye hatamwacha, alichukua mawe matano malaini, akachukua kombeo lake na kwenda kukutana na shujaa yule.

Picha
Mawe matano ya Daudi.

Maandiko yanatwambia kwamba jiwe la kwanza Daudi alilorusha lilipiga paji la uso wa Goliathi, likiitimisha maisha yake.

Kutafuta Majibu

Wakati Daudi akitumia jiwe moja tu kumuua Goliathi, alijiandaa kwa matano. Kwa matano! Hii hunifanya nifikirie kuhusu jinsi ninavyoweza kujiandaa mwenyewe kukabiliana na ulimwengu.

Vipi kama kila jiwe la Daudi liliwakilisha nguvu tuliyohitaji kuwa washindi katika maisha yetu? Je, mawe hayo matano yanaweza kuwa ni nini? Nimefikiria mambo yafuatayo:

  1. Jiwe la upendo wangu kwa Mungu.

  2. Jiwe la imani yangu kwa Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

  3. Jiwe la maarifa ya utambulisho wangu halisi.

  4. Jiwe la toba yangu ya kila siku.

  5. Jiwe la uwezo wangu wa kupokea nguvu za Mungu.

Hebu tuzungumze kuhusu jinsi tunavyobarikiwa na nguvu hizi.

Kwanza, jiwe la upendo wangu kwa Mungu. Kumpenda Mungu ni amri kuu ya Kwanza. Mwongozo wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana hutufundisha: “Mungu anakupenda. Yeye ni Baba yako. Upendo wake mkamilifu unaweza kukuvutia wewe kumpenda Yeye. Wakati upendo wako kwa Baba wa Mbinguni unapokuwa ni ushawishi muhimu katika maisha yako, maamuzi mengi yanakuwa rahisi sana.”

Upendo wetu kwa Mungu na urafiki wetu wa karibu pamoja Naye hutupatia nguvu tunayohitaji ya kubadili maisha yetu na kwa urahisi kushinda changamoto zetu.

Pili, jiwe la imani katika Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Wakati Yesu Kristo alipokuja duniani, aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu, na alijichukulia huzuni zetu, maumivu yetu, madhaifu yetu na magonjwa yetu ya kimwili na kiakili. Hiyo ndiyo sababu Yeye anajua jinsi ya kutusaidia. Kuwa na imani katika Yesu Kristo humaanisha kutegemea tumaini lake, muda Wake, upendo Wake na nguvu Zake kamili za kulipia dhambi zetu. Jiwe la imani katika Yesu Kristo litampiga “shujaa” yeyote katika maisha yetu. Tunaweza kuushinda ulimwengu huu ulioanguka kwa sababu Yeye aliushinda kwanza.

Namba tatu, jiwe la maarifa ya utambulisho wangu halisi. Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, ametufundisha kwamba utambulisho wetu muhimu ni kama watoto wa Mungu, watoto wa agano na wanafunzi wa Yesu Kristo.

Kila kitu hubadilika ninapojua mimi ni nani. Ninapotia shaka uwezo wangu, mara kwa mara najisemea akilini mwangu au kwa sauti, “mimi ni binti wa Mungu, mimi ni binti wa Mungu,” mara nyingi niwezavyo mpaka nihisi ujasiri tena wa kuendelea.

Nne, jiwe la toba yangu ya kila siku. Katika mwongozo wa Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana, tunasoma: Toba siyo adhabu kwa ajili ya dhambi; ni njia ambayo kwayo Mwokozi anatuweka huru kutokana na dhambi. Kutubu maana yake ni kubadilika—kugeuka mbali na dhambi na kumgeukia Mungu. Inamaanisha kufanya maboresho na kupokea msamaha. Aina hii ya badiliko siyo tukio la wakati mmoja; bali ni mchakato unaoendelea.”

Hakuna kitu kinachotuweka huru zaidi kuliko kuhisi msamaha wa Mungu na kujua kwamba tu wasafi na kupatana Naye. Msamaha unawezekana kwa kila mmoja.

Jiwe la tano ni jiwe la uwezo wangu wa kupokea nguvu za Mungu. Maagano tunayofanya pamoja na Mungu, kama vile yale tuyafanyayo katika ibada ya ubatizo, hutuwezesha kupokea nguvu za uungu. Nguvu ya Mungu ni nguvu halisi ambayo hutusaidia kukabiliana na changamoto, kufanya maamuzi mazuri na kuongeza uwezo wetu wa kuvumilia hali ngumu. Ni nguvu ambayo kwayo tunakua katika uwezo maalumu tunaohitaji.

Mwongozo wa Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana huelezea: “Maagano hukuunganisha kwa Baba wa Mbinguni na Mwokozi. Maagano huongeza nguvu ya Mungu katika maisha yako.”

Hebu tuzungumze kuhusu muunganiko huo. Kumbuka wakati Kristo alipofundisha tofauti kati ya nyumba iliyojengwa juu ya mwamba na nyingine juu ya mchanga? Mzee Dieter F. Uchtdorf alielezea: “Nyumba hainusuriki katika dhoruba kwa sababu nyumba ni imara. Pia hainusuriki tu kwa sababu mwamba ni imara. Nyumba hunusurika katika dhoruba kwa sababu imeunganishwa kwa uthabiti kwenye ule mwamba imara. Ni nguvu za muunganiko huu kwenye mwamba ambazo ni muhimu.”

Picha
Nyumba juu ya mwamba.

Muunganiko wetu binafsi kwa Yesu Kristo utatupatia ujasiri na uthubutu wa kusonga mbele katikati ya watu wasioheshimu imani zetu au wanaotuchokoza. Kristo hutualika sisi kumuweka katika akili zetu muda wote; Yeye hutuambia, “Nitegemeeni katika kila wazo.” Kufikiria kuhusu Mwokozi hutupatia uwazi wa akili wa kufanya maamuzi, kutenda pasipo uwoga na kusema hapana kwa kile kilicho kinyume na mafundisho ya Mungu. Wakati siku yangu inapokuwa ngumu na kuhisi kama siwezi tena, kufikiri kuhusu Kristo huniletea amani na hunipa tumaini.

Tunawezaje kupata nguvu hii ya Yesu Kristo? Kutii maagano yetu na kuongeza imani yetu katika Yesu Kristo ni muhimu.

Natamani Daudi angekuwa na jiwe moja zaidi; hilo lingekuwa jiwe la ushuhuda wangu. Ushuhuda wetu hujengwa kwa uzoefu binafsi wa kiroho ambapo tunatambua ushawishi wa kiungu katika maisha yetu. Hakuna anayeweza kuondoa ufahamu huo kwetu. Kujua kile tukijuacho kwa kuishi uzoefu wetu wa kiroho ni cha thamani kubwa. Kuwa mkweli kwa ufahamu huo hutupatia uhuru. Hutupatia shangwe! Kama tunapenda ukweli, tutautafuta na mara tu tuupatapo, tutaulinda.

Mwaliko

Kama vile nilivyochagua jiwe namba sita, ninawaalika mkutane na darasa lenu, akidi au familia na kufikiria kuhusu nguvu zingine unazohitajika kuzipata ili kubakia mwaminifu kwa Mungu na, hivyo, kuushinda ulimwengu.

Ahadi

Marafiki wapendwa, Kristo ana hamu ya kutusindikiza kwenye safari ya maisha yetu. Ninakuahidi, unapoishikilia fimbo ya chuma, utatembea mkono kwa mkono pamoja na Yesu Kristo. Yeye atakuongoza, na Yeye atakufundisha. Kwa mkono Wake, utaweza kumuangusha kila Goliathi ajaye katika maisha yako.

Ushuhuda

Nashuhudia kwamba kuna shangwe katika kusali kila siku, katika kusoma Kitabu cha Mormoni kila siku, katika kushiriki sakramenti kila Jumapili na kwa kuhudhuria seminari—hata iwe mapema asubuhi. Kuna shangwe katika kutenda mema.

Kuna shangwe katika kuwa mwaminifu kwa Mungu wa ulimwengu, Mwokozi wa ulimwengu, Mfalme wa wafalme. Kuna shangwe katika kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo.

Mungu ni Baba yetu. Anajua matamanio ya moyo wako na uwezo wako na anakuamini.

Wapendwa vijana, Yesu Kristo atakusaidia kuwa mwaminifu hadi mwisho. Juu ya kweli hizi ninatoa ushuhuda wangu katika jina la Yesu Kristo, amina.