Mkutano Mkuu
Mahekalu, Nyumba za Bwana Zikienea Duniani
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Mahekalu, Nyumba za Bwana Zikienea Duniani

Unapokuja kwa kustahili na sala kwenye nyumba Yake takatifu, utakuwa umejiami kwa nguvu Zake.

Je, hampendi maneno mazuri tuliyotoka kuyaimba? “Nitawaimarisha, msimame, … Kwa mkono wangu, milele yote.” Bwana anawaimarisha Watakatifu Wake wa nyakati zote wanapokuja kwenye nyumba Yake takataifu. Kutoka Kinshasa hadi Zollikofen hadi Fukuoka hadi Oakland, vijana, kwa hiari yao wenyewe, wanafurika kwenye visima vya ubatizo hekaluni. Hapo zamani, wafanyakazi wengi wa ibada walikuwa na mvi—lakini siyo sasa. Wamisionari wanaoitwa, wamisionari watoa huduma, na wamisionari waliorudi wako kila kona. Kote ulimwenguni, kuna hisia zinazoongezeka zinazotuvuta kuja kwenye nyumba ya Bwana.

Mwaka mmoja tu uliopita, rafiki mpendwa wa familia, mwenye umri wa miaka 95 anayeishi pwani ya mashariki mwa Marekani, ambaye amefundishwa na wamisionari kwa miaka 70, alisema kwa binti yake, “Nataka kwenda hekaluni pamoja na wewe.”

Binti yake alijibu, “Vizuri, Mama, kwanza unahitaji kubatizwa.”

Picha
Ubatizo wa dada mzee.

“SAWA,” alijibu, “basi nataka kubatizwa. Alibatizwa. Siku chache baadaye, aliingia kwa staha katika kisima cha ubatizo cha hekalu. Na zaidi ya mwezi mmoja tu uliopita, alipokea endaumenti yake mwenyewe na kuunganishwa. “Elimu na nguvu za Mungu zapanuka; Pazia juu ya dunia linaanza kufunguka.”

Picha
Dada mzee nje ya hekalu.

Je, umewahi kujiuliza kwa nini Bwana amemwelekeza nabii Wake sasa kuijaza dunia kwa mahekalu Yake matakatifu? Kwa nini, kwa wakati huu mahususi, anatoa neema inayohitajika kwa watu Wake wa agano kwamba kupitia zaka zao takatifu, mamia ya nyumba za Bwana ziweze kujengwa?

Asubuhi hii, Rais Dallin H. Oaks alionyeshwa picha za mahekalu yanayojengwa ulimwenguni kote. Kathy na mimi hivi karibuni tulikuwa huko Ufilipino. Fikiria muujiza huu: Hekalu la Manila liliwekwa wakfu mwaka 1984. Imepita miaka 26 kabla ya hekalu la pili huko Jijini Cebu, kumalizika mwaka wa 2010. Sasa, miaka 14 baadaye, mahekalu 11 yanajengwa, yanasanifiwa au yameandaliwa kwa uwekaji wakfu. Kutoka kaskazini hadi kusini: Laoag, Tuguegarao, Santiago, Urdaneta, Alabang, Naga, Tacloban City, Iloilo, Bacolod, Cagayan de Oro na Davao. Inastaajabisha kuona matendo ya ajabu ya Mungu!

Picha
Mahekalu huko Ufilipino.

Duniani kote, nyumba za Bwana zinakuja karibu zaidi nasi. Kwa nini katika siku yetu?

Siku za Mwisho

Bwana ameonya kwamba katika siku za mwisho, kutakuwa na dhiki miongoni mwa mataifa, watu wangekuwa “wanajipenda wenyewe,” “vitu vyote [vingekuwa] katika vurugu,” kukanganyikiwa kungeongezeka, na “watu [wangevunjika] mioyo.” Hakika tumeona wanaume kwa wanawake waliovunjika mioyo: ushawishi wa ulimwengu, kupotezwa na sauti za kuvutia, kupuuza lishe ya kiroho, uchovu kutokana na mahitaji ya uanafunzi. Labda umesikitishwa kadiri ulivyomwona mtu unayempenda, ambaye wakati mmoja alizungumza kwa dhati juu ya imani yake kwa Yesu Kristo, alitoa ushahidi juu ya Kitabu cha Mormoni, na kwa ari kujenga ufalme wa Mungu, ghafla akiachana na hayo, angalau kwa sasa, akiachana na imani yake na kwenda kwenye kingo za Kanisa. Ushauri wangu kwako ni usivunjike moyo! Yote ni shwari! Kwani kwa Mungu hakuna lisilowezekana.

Kwa vurugu hii na kutokuamini huku kulikotolewa unabii ulimwenguni, Bwana ameahidi kwamba kutakuwa na watu wa agano, watu walio na shauku wakisubiri kurudi Kwake, watu wanaosimama katika mahali patakatifu na hawaondoshwi nje ya mahali pao. Bwana aliongelea watu wenye haki wakikinza ulaghai wa adui, wakiitiisha imani yao, wakifikiria kiselestia na wakimtumainia kabisa Mwokozi Yesu Kristo.

Kwa nini Bwana sasa analeta mamia ya mahekalu Yake jirani na sisi? Sababu moja ni kwamba katikati ya machafuko na majaribu ya ulimwengu, Yeye ameahidi kuwaimarisha na kuwabariki Watakatifu Wake wa agano, na ahadi zake zinatimia!

Ahadi kutoka Hekalu la Kirtland

Jinsi gani majumba haya matakatifu yanaimarisha, yanafariji na kutulinda sisi? Tunapata jibu katika maombi ya Nabii Joseph Smith katika kuweka wakfu Hekalu la Kirtland. Ilikuwa katika hekalu hili ambapo Watakatifu waliimba, “Tutaimba nao majeshi ya mbingu.” Mwokozi Mwenyewe alijitokeza, na manabii wa kale walirudi, wakitoa funguo za ukuhani za ziada kwenye urejesho wa injili.

Katika tukio hili takatifu katika Hekalu la Kirtland, Nabii aliomba kwamba katika nyumba takatifu ya Bwana Watakatifu wavikwe uwezo wa Mungu, kwamba jina la Yesu Kristo liweze kuwa juu yao, kwamba malaika wake wawalinde, na kwamba wakue katika Bwana na “kupokea utimilifu wa Roho Mtakatifu.” Maombi haya yenye nguvu yanatimia katika maisha yetu kwa uaminifu tunapoabudu katika nyumba ya Bwana.

Jihami kwa Nguvu

Katika nyumba ya Bwana, kwa uhalisia tunavikwa nguvu za mbinguni. Imani yetu katika Yesu Kristo na upendo wetu kwa ajili Yake vinathibitishwa na kuimarishwa. Tunahakikishiwa kiroho juu ya utambulisho wetu wa kweli na madhumuni ya maisha. Tunapokuwa waaminifu, tunabarikiwa na ulinzi dhidi ya majaribu na vikengeusha fikra. Tunahisi upendo wa Mwokozi wetu anapotuinua kutokana na magumu yetu na changamoto zetu. Tumevikwa silaha ya nguvu za Mungu.

Jina Lake juu Yetu

Katika nyumba Yake tunajichukulia jina Lake kwa utimilifu zaidi juu yetu. Tunapobatizwa, tunakiri imani yetu katika Yeye na utayari wetu wa kushika amri Zake. Ndani ya hekalu, tunathibitisha kwa utakatifu, kupitia maagano yetu, kumfuata Yeye milele.

Picha
Hekalu la Heber Valley, Utah

Vijana wa Kanisa hili ni wa kipekee. Katika ulimwegu mgumu, wanajichukulia juu yao wenyewe jina la Kristo. Katika Jiji la Heber, Utah, mkutano wa umma ulifanyika ili kujadili maelezo ya kina ya mipango ya ujenzi wa hekalu. Vijana mia tatu walijaza uwanja wa jirani ili kuonyesha kuunga mkono mapendekezo ya hekalu. Mvulana mmoja, akiongea kwa viongozi wa kiserikali katika jukwaa la wazi, kwa ujasiri alieleza, “Nina matumaini ya kufunga ndoa katika hekalu hili. [Hekalu hili litasaidia] kuniosha na kuwa msafi.” Mwingine alielezea hekalu kama alama ya nuru na matumaini. Wavulana na wasichana wa Kanisa kote ulimwenguni wanakumbatia jina la Yesu Kristo.

Picha
Vijana wakijaza uwanja huko Jiji la Heber

Malaika pamoja Nasi

Katika Hekalu la Kirtland, nabii Joseph aliomba kwamba “malaika wangewalinda [Watakatifu Wake].” Kila mara wakifanya ibada kwa niaba ya mababu zetu hekaluni huleta uthibitisho mtamu na wa uhakika kwamba maisha yanaendelea upande wa pili ya pazia.

Ingawa uzoefu wetu mwingi katika nyumba ya Bwana ni mtakatifu sana kuweza kushiriki hadharani, baadhi tunaweza kushiriki. Miaka arobaini iliyopita, wakati tukiishi Florida, Kathy na mimi tulisafiri kwenda hekaluni huko Atlanta, Georgia. Usiku wa Jumatano, Mei 9, 1984, tulipomaliza huduma hekaluni, mfanyakazi wa ibada alinijia na kuniuliza kama ningekuwa na muda wa kufanya ibada moja tu ya mwanzo ya maandalizi. Jina la mtu ambaye nilimwakilisha halikuwa la kawaida. Jina lake lilikuwa Eleazer Cercy.

Siku iliyofuata, hekalu lilijaa Watakatifu. Nilipokuwa nikijiandaa kwa ajili ya endaumenti yangu ya pili kwa siku hiyo, nilipewa jina la mtu ambaye ningemwakilisha. Cha kushangaza, jina lilikuwa la mtu yule yule kutoka usiku wa jana, Eleazer Cercy. Nilimhisi Roho wa Bwana palee endaumenti ile ilipokamilika. Baadaye mchana, tulipokuwa tukitembelea hekalu, Kathy alimwona mzee mmoja rafiki wa familia yetu, Dada Dolly Fernandez ambaye sasa alikuwa akiishi Atlanta. Bila mwanafamilia mwanaume pamoja naye, aliomba kama ingewezekana mimi kusaidia katika kuunganishwa kwa baba yake kwa wazazi wa baba yake. Nilifurahia heshima hiyo.

Nilipopiga magoti mwisho wa madhabahu kwa ajili ya ibada hii takatifu, nilisikia kwa mara nyingine tena jina ambalo sasa lilikuwa likiandikwa akilini mwangu, baba yake ni, Eleazer Cercy. Kwa utimilifu naamini kwamba baada ya maisha haya, nitakutana na kukumbatiana na mtu anayejulikana katika maisha ya duniani kama Eleazer Cercy.

Uzoefu wetu mwingi katika nyumba ya Bwana huleta amani ya shangwe na ufunuo tulivu badala ya kitu cha ghafla. Lakini tunahakikishiwa malaika watatulinda sisi!

Utimilifu wa Roho Mtakatifu

Kipawa cha Roho Mtakatifu kimetolewa kwetu sisi tunapothibitishwa kama waumini wa Kanisa. Kila wiki kwa kustahili tunapokula mkate na maji katika ukumbusho wa Mwokozi wetu, tunaahidiwa kwamba daima Roho Wake atakuwa pamoja nasi. Tunapokuja mioyo yetu ikiwa tayari kwenye nyumba ya Bwana, mahali patakatifu zaidi juu ya dunia, tunapiga hatua katika Bwana na tunaweza “kupokea utimilifu zaidi wa Roho Mtakatifu.” Kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu, tunajawa na amani na shangwe na matumaini yasiyotamkika. Tunapokea nguvu ili tubaki wanafunzi Wake hata kama tunajikuta tuko nje ya mahali patakatifu.

Rais Russell M. Nelson alitamka: “Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, atafanya baadhi ya kazi Zake kubwa kati ya sasa na wakati atakapokuja tena. Tutaona ishara za maajabu ambazo Mungu Baba na … Yesu Kristo … wanaongoza Kanisa hili katika enzi na utukufu.” Kazi kubwa na ishara ya maajabu itakuwa kuijaza dunia kwa nyumba za Bwana.

Wapendwa marafiki zangu, kama tunaweza na kama bado hatujaongeza uhudhuriaji wetu hekaluni, sasa mara kwa mara tutafute muda zaidi wa kuabudu katika nyumba ya Bwana. Na tuyaombee mahekalu ambayo yametangazwa, kwamba viwanja viweze kununuliwa, kwamba serikali ziidhinishe michoro, kwamba wafanyakazi wenye vipaji waone vipaji vyao vikikuzwa, na kwamba uwekaji wakfu mtakatifu ulete idhini ya mbinguni na ziara za malaika.

Ahadi

Hekalu kiuhalisia ni nyumba ya Bwana. Ninakuahidi wewe unapokuja kwa kustahili na kwa sala kwenye nyumba Yake takatifu, utakuwa umejihami na nguvu Zake, jina Lake litakuwa juu yako, malaika Zake watapewa jukumu la kukulinda, nawe utakua katika baraka ya Roho Mtakatifu.

Bwana ameahidi, “Kila mtu atakayeziacha dhambi zake na kuja kwangu, na kulilingana jina langu, na kuitii sauti yangu, na kushika amri zangu, atauona uso wangu na kujua kuwa Mimi ndiye.” Kuna njia nyingi tofauti za kuona uso wa Kristo, na hakuna mahali bora kuliko katika nyumba Yake takatifu.

Katika siku hii ya mkanganyiko na vurugu, ninashuhudia kwamba hekalu ni nyumba Yake takatifu, na itasaidia kutuhifadhi, kutulinda na kutuandaa sisi kwa ajili ya siku ile ya utukufu wakati, pamoja na malaika Wake watakatifu, Mwokozi wetu atarudi katika enzi, nguvu, na utukufu mkuu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Msingi Imara,” Nyimbo za Dini,, na. 36.

  2. “Roho wa Mungu,” Nyimbo za Dini, na. 2

  3. Kwa sasa kuna mahekalu 182 yanayofanya kazi. Sita yako katika marekebisho. Saba yanasubiri kuwekwa wakfu na moja likisubiri kuwekwa wakfu upya. 45 yako katika hatua za ujenzi na mengine zaidi 94 yametangazwa au katika hatua za upangaji na usanifu.

  4. Ona Luka 21:10.

  5. 2 Timotheo 3:2.

  6. Mafundisho na Maagano 88:91.

  7. Mzee David A. Bednar alisema: “Kanuni za injili zipo kwa ajili yangu mimi na wewe kama usukani ulivyo kwa meli. Kanuni sahihi zinatuwesha kupata njia yetu na kusimama imara, thabiti na tusiohamishika ili tusipoteze na kuanguka katika dhoruba za giza nene na machafuko ya siku za mwisho” (“Kanuni za Injili Yangu,” Liahona, Mei 2021, 126).

  8. Mafundisho na Maagano 45:26.

  9. “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate” [Mathayo 16:24].

  10. Ona Luka 1:37.

  11. Ona Mafundisho na Maagano 87:8.

  12. Nyimbo za Dini, na. 2.

  13. Ona Mafundisho na Maagano 110. Kabla ya wakati huu, Joseph Smith alipokea Ukuhani wa Haruni na funguo Zake kutoka kwa Yohana Mbatizaji, na yeye alikuwa amepokea Ukuhani wa Melkizedeki na funguo zake kutoka kwa Mitume Petro, Yakobo, na Yohana Mafundisho na Maagano 13:1; 27:12–13).

  14. Mafundisho na Maagano 109:15; ona pia mstari wa 22.

  15. Rais Russell M. Nelson alisema, “Hekalu linaweza kutusaidia sisi katika jitihada zetu. Huko tunapewa nguvu ya Mungu, inayotupatia uwezo wa kumshinda Shetani, mchochezi wa ubishi wote” (“Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023, 101).

  16. Ona Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 15, 2022), Gospel Library.

  17. Elder Colin Stauffer, personal correspondence, Jan. 30, 2024.

  18. Mafundisho na Maagano 109:22.

  19. Ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79.

  20. Mafundisho na Maagano 109:15.

  21. Ona Warumi 15:13.

  22. Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2018, 96.

  23. Rais Brigham Young alisema, “Tutakuwa na mamia ya mahekalu na maelfu ya wanaume na wanawake wakihudumu kwa niaba ya wale waliolala, bila kuwa nafursa ya kusikia na kutii injili” (Teaching of the Presidents of the Church: Brigham Young [1997], 312). Na Rais Ezra Taft Benson alisema: “Waliotutangulia walitoa unabii kwamba mahekalu yatasambaa kwenye nchi za Kaskazi na Kusini mwa Amerika, visiwa vya Pasifiki, Ulaya na kwingineko. Kama kazi hii ya ukombozi itafanywa kwa kiwango kinachopaswa, mamia ya mahekalu yatahitajika” (The Teaching of Ezra Taft Benson [1988], 247).

  24. Mafundisho na Maagano 93:1.

  25. Mzee David B. Haight alisema:

    “Ni kweli kwamba baadhi hakika wamemwona Mwokozi, lakini mtu anaporejelea kwenye kamusi, anajifunza kwamba kuna maana zingine nyingi za neno ona, kama vile kumjua Yeye, kumtambua Yeye na kazi Yake, kuelewa umuhimu Wake au kumuelewa Yeye.

    “Uelewa huo wa kimbingu na baraka unapatikana kwa ajili kila mmoja wetu” (“Temples and Work Therein,” Ensign, Nov. 1990, 61).