Mkutano Mkuu
Zaidi ya Shujaa
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Zaidi ya Shujaa

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo si tu shujaa wetu, Yeye ni Bwana na Mfalme wetu, Mwokozi na Mkombozi wa wote.

Kutoka 1856 hadi 1860, maelfu ya waanzilishi Watakatifu wa Siku za Mwisho walivuta mali zao kwa kutumia mikokoteni kwa zaidi ya maili 1,000 (kilomita 1600) wakati wakisafiri kwenda bondel la Salt Lake. Miaka mia moja sitini na saba iliyopita wiki hii, mnamo Oktoba 4, 1856, Rais Brigham Young alishangazwa alipogundua kwamba kombania mbili za mikokoteni, zilizokuwa zikiongozwa na Edward Martin na James Willie, bado zilikuwa mamia ya maili kutoka Salt Lake, majira ya baridi yalipokuwa yakikaribia kwa kasi.1 Siku iliyofuata, siyo mbali kutoka pale tunapokutana leo, Rais Young alisimama mbele ya Watakatifu na kutangaza, “Wengi wa kaka na dada zetu wako huko nyandani kwenye mikokoteni, na wanapaswa kuletwa hapa. … Nendeni na muwalete watu hao hapa uwandani.”2

Siku mbili tu baadaye, vikosi vya kwanza vya uokoaji viliondoka kuwatafuta waanzilishi wenye mikokoteni.

Mshiriki wa kombania ya Willie alielezea hali mbaya kabla ya kufika kwa timu kuu ya kikosi cha uokoaji. Alisema, “Wakati ilipoonekana kwamba vyote vitapotea, na kuonekana maisha hayana kitu tena, … kama radi bila wingu lolote, Mungu alijibu maombi yetu. Kundi okozi, likileta chakula na vitu vya kukidhi mahitaji … , lilionekana. … Ni jinsi gani tulimshukuru Mungu kwa ukombozi wetu.”3

Hawa waokoaji walikuwa mashujaa kwa waanzilishi, wakiweka maisha yao wenyewe kwenye hatari katika hali mbaya ya hewa ili kuwaleta nyumbani wengi kadiri iwezekanavyo. Shujaa mmojawapo alikuwa Ephraim Hanks.

Katikati ya Oktoba, na bila kujua magumu ya wasukuma mkokoteni, Hanks alikuwa akirejea nyumbani kwake Salt Lake, na usiku, aliamshwa na sauti, ikisema, “Wasukuma mkokoteni wako kwenye matatizo, na unahitajika; je, utakwenda na kuwasaidia?”

Familia yake ilijiunga na Kanisa kule Uingereza na kisha kwenda Jijini Salt Lake. Kwa swali hilo likizunguka akilini mwake, alirejea kwa haraka Jijini Salt Lake na, baada ya kusikia wito wa watu wa ziada wa kujitolea wa Rais Heber C. Kimball, Hanks alianza safari mwenyewe siku iliyofuata, kwenda kuokoa. Akienda kwa haraka, aliwapita waokoaji wengine njiani na, alipoifikia kombania ya Martin, Hanks anakumbuka, “Macho yaliyotazama ujio wangu nilipokuwa nikiingia kambini kwao kamwe hayawezi kufutika katika kumbukumbu zangu … na ilikuwa ya kutosha kugusa moyo shupavu zaidi.4

Ephraim Hanks alibakia kwa siku kadhaa akihama kutoka hema moja kwenda jingine akiwabariki wagonjwa. Anasimulia kwamba, “katika mifano kadhaa, wakati tukiwahudumia wagonjwa, na kukemea magonjwa katika jina la Bwana Yesu Kristo, maumivu yangepoa mara moja, waliponywa takribani muda huo huo.”5 Ephraim Hanks daima atakuwa shujaa kwa waanzilishi wasukuma mkokoteni.

Vivyo hivyo kama huo ukomboaji wa ajabu, matukio ambayo yanaathiri maisha yetu na hata mkondo wa historia mara nyingi ni matokeo ya maamuzi na mafanikio ya wanaume na wanawake binafsi—wasanii maarufu, wanasayansi, viongozi wa biashara na wanasiasa. Watu hawa wa kipekee mara nyingi huheshimiwa kama mashujaa, pamoja na sanamu na makumbusho kujengwa ili kuadhimisha walichokifanya.

Nilipokuwa mvulana mdogo, mashujaa wangu wa kwanza walikuwa wanariadha. Kumbukumbu zangu za mapema zilikuwa za kukusanya kadi za besiboli zenye picha na takwimu za wachezaji wa Ligi Kuu ya Besiboli. “Kumsujudia shujaa” kama mtoto inaweza kuwa ya kupendeza na si kosa, kama vile watoto wanapovaa kama mashujaa wao wanaowapenda kwa ajili ya Halloween. Ingawa tunawatamania na kuwaheshimu wanaume na wanawake wengi wenye vipaji na upekee kwa uwezo wao na michango yao, kiwango ambacho wao “huheshimiwa,” kama kikipitiliza kiasi, inaweza kuwa sawa na watoto wa Israeli kuabudu ndama wa dhahabu katika jangwa la Sinai.

Kama watu wazima, kile kilichokuwa furaha ya kitoto isiyo na kosa kinaweza kuwa kikwazo kama “kumsujudia shujaa” wa kisiasa, wanablogu, washawishi, wanariadha au wanamuziki hutusababishia kutazama “zaidi ya alama”6 na kuacha kile ambacho ni cha muhimu sana.

Kwa watoto wa Israeli, changamoto haikuwa dhahabu waliyoibeba katika safari yao kwenda nchi ya ahadi lakini badala yake waliruhusu dhahabu kuwa: sanamu, ambayo pia ikawa kitu cha ibada yao, hivyo kuondoa fokasi yao kwa Yehova, ambaye aligawanya Bahari ya Shamu na kuwaokoa kutoka utumwani. Fokasi yao kwa ndama iliathiri uwezo wao wa kumwabudu Mungu wa kweli.7

Yule shujaa—shujaa wetu, wa sasa na daima—ni Yesu Kristo, na chochote au yeyote, ambaye anatuondoa kwenye mafundisho Yake, kama yalivyo kwenye maandiko na kupitia maneno ya manabii walio hai, huweza kuwa na madhara hasi kwenye maendeleo yetu kwenye njia ya agano. Kabla ya uumbaji wa ulimwengu huu, tulimtegemea Yesu Kristo wakati ilipojulikana dhahiri kwamba mpango uliopendekezwa na Baba wa Mbinguni, ambao ulijumuisha fursa yetu ya kuendelea na kuwa kama Yeye, ulikuwa umevamiwa.

Sio tu kwamba Yesu Kristo alikuwa kiongozi kuutetea mpango wa Baba, lakini pia angebeba jukumu la muhimu sana katika kuutekeleza. Alimjibu Baba na kujitolea kuwa “mkombozi kwa ajili ya wote,”8 ili kulipia deni ambalo kila mmoja wetu angelibeba kupita dhambi ambalo tusingeweza kulilipa wenyewe.

Rais Dallin H. Oaks amefundisha, “[Yesu Kristo] amefanya kila kitu ambacho ni muhimu kwa ajili ya safari yetu hapa duniani kuelekea hatma iliyoelezwa katika mpango wa Baba yetu wa Mbinguni.”9

Katika Bustani ya Gethsemane, alipokabiliwa na jukumu hilo zito, Mwokozi kwa ujasiri alisema, “Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” na aliendelea kubeba juu yake mrundikano wa maumivu, magonjwa na mateso kwa ajili ya dhambi za wote ambao wangeishi.10 Katika tendo timilifu la utiifu na dhamira, Yesu Kristo alikamilisha tendo la kishujaa, lililo kuu katika uumbaji wote, likikamilishwa na Ufufuko Wake wenye utukufu.

Katika mkutano mkuu wetu wa hivi karibuni, Rais Russell M. Nelson alitukumbusha: “Maswali au shida zozote mlizonazo, jibu daima linapatikana katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo. Jifunzeni zaidi kuhusu Upatanisho Wake, upendo Wake, rehema Yake, fundisho Lake na injili Yake ya urejesho ya uponyaji na ukuaji. Mgeukie Yeye! Mfuate Yeye!”11 Na ningeongeza, “Mchague Yeye.”

Katika ulimwengu wetu changamani, inaweza kuwa yenye kushawishi kugeukia mashujaa wa jamii katika jitihada za kuleta udhahiri katika maisha wakati hali inaonekana kukanganya au kutuzidia. Tunanunua nguo wanazozalisha, tunakumbatia siasa wanazozitoa na tunafuata mapendekezo yao waliyoshiriki kwenye mitandao ya kijamii. Hili linaweza kuwa sawa kwa muda, lakini tunapaswa kuwa makini kwamba aina hii ya kumsujudia shujaa haiwi ndama wetu wa dhahabu. Kumchagua shujaa “sahihi” huwa na athari za milele.

Wakati familia yetu ilipofika Uhispania kuanza huduma yetu kama viongozi wa misheni, tulikuta nukuu kwenye fremu iliyotolewa na Mzee Neal A. Maxwell ambayo ilikuwa inahusika kwa mashujaa tunaochagua kuwafuata. Alisema, “Kama hujachagua ufalme wa Mungu kwanza, hatimaye hakutakuwa na tofauti kabisa katika kile unachokichagua kama mbadala.”12 Akina kaka na akina dada, ni kwa kumchagua Yesu Kristo, Mfalme wa Wafalme, kwamba tunachagua Ufalme wa Mungu. Uchaguzi mwingine wowote ni sawa na kumchagua binadamu, au ndama wa dhahabu, na mwishowe vitatufelisha.

Katika Kitabu cha Danieli kwenye Agano la Kale, tunasoma hadithi ya Shadraka, Meshaki na Abednego, ambao kwa dhahiri walijua ni shujaa yupi wa kumchagua—na haikuwa miungu yoyote ya Mfalme Nebukadreza. Walitangaza kwa ukakamavu:

“Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto. …

“Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako.”13

Kama Mtume Paulo alivyofundisha, “Kama vile walivyo miungu mingi,”14 na, ninaongezea, wapo mashujaa wengi, ambao tunaalikwa kuwasujudia, kuwaabudu na kuwakumbatia. Lakini kama vile marafiki watatu wa Danieli walivyojua, kuna Mmoja pekee yule anayetuhakikishia ukombozi—kwa sababu Yeye tayari na daima atafanya hivyo.

Kwetu sisi, katika safari yetu ya kurejea kwenye uwepo wa Mungu, kwenye nchi yetu ya ahadi, si mwanasiasa, mwanamuziki, mwanariadha au mwanablogu ambao ni mada hapa, bali, kuchagua kuwaruhusu wao wawe vitu vya msingi kwa ajili ya umakini na fokasi yetu badala ya Mwokozi na Mkombozi wetu.

Tunamchagua Yeye, Yesu Kristo, tunapochagua kuheshimu siku Yake iwe tuko nyumbani au safarini kwenye likizo. Tunamchagua Yeye tunapochagua maneno Yake kupitia maandiko na mafundisho ya manabii walio hai. Tunamchagua Yeye tunapochagua kuwa na kibali cha hekaluni na kuishi kwa kustahili matumizi yake. Tunamchagua Yeye tunapokuwa wapatanishi na kukataa kuwa wagomvi, “hasa pale tunapokuwa na tofauti za kimaoni.”15

Hakuna kiongozi aliyewahi kuonyesha ujasiri, hakuna binadamu aliyeonyesha wema zaidi, hakuna tabibu aliyetibu magonjwa mengi zaidi na hakuna mwana sanaa ambaye amekuwa mbunifu zaidi kuliko Yesu Kristo.

Katika ulimwengu wa mashujaa, pamoja na sanamu na makumbusho kuwekwa kwa ajili ya wanaume na wanawake wa ulimwenguni, kuna Mmoja ambaye husimama juu ya wote. Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo si tu shujaa wetu, Yeye ni Bwana na Mfalme wetu, Mwokozi na Mkombozi wa wote. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Uchunguzi uliojikita kwenye mkokoteni wa kombania ya Willie and Martin hujumuisha LeRoy R. and Ann W. Hafen, Handcarts to Zion: The Story of a Unique Western Migration, 1856–1860 (1960); Rebecca Cornwall and Leonard J. Arrington, Rescue of the 1856 Handcart Companies (1981); Howard K. and Cory W. Bangerter, Tragedy and Triumph: Your Guide to the Rescue of the 1856 Willie and Martin Handcart Companies, 2nd ed. (2006); and Andrew D. Olsen, The Price We Paid: The Extraordinary Story of the Willie Martin Handcart Pioneers (2006).

  2. Brigham Young, “Remarks,” Deseret News, Oct. 15, 1856, 252.

  3. John Oborn, “Brief History of the Life of John Oborn, Pioneer of 1856,” 2, in John Oborn reminiscences and diary, circa 1862–1901, Church History Library, Salt Lake City.

  4. Ephraim K. Hanks’s narrative, in Andrew Jenson, “Church Emigration,” Contributor, Mar. 1893, 202–3.

  5. Hanks, katika Andrew Jenson, “Church Emigration,” 204.

  6. Yakobo 4:14.

  7. Ona Kutoka 32.

  8. 1 Timotheo 2:6; ona pia Mathayo 20:28.

  9. Dallin H. Oaks, “Je, Mwokozi Amefanya Nini kwa ajili Yetu Sisi?,” Liahona, Mei 2021, 75.

  10. Ona Luka 22:39–44.

  11. Russell M. Nelson, “Jibu Daima Ni Yesu Kristo,” Liahona, Mei 2023, 127.

  12. Attributed to 18th-century English clergyman William Law; quoted in Neal A. Maxwell, “Response to a Call,” Ensign, May 1974, 112.

  13. Ona Danieli 3:13–18.

  14. 1 Wakorintho 8:5.

  15. Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023, 98.