Mkutano Mkuu
Nguvu ya Kuunganisha
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Nguvu ya Kuunganisha

Nguvu ya kuunganisha huruhusu wokovu wa mtu binafsi na kuinuliwa kwa familia kupatikane ulimwenguni kote kwa watoto Mungu.

Imekuwa ikitolewa unabii tokea siku za Isaya1 kwamba katika siku za mwisho, watu wa zamani wa agano wa Bwana, nyumba ya Israeli, wanapaswa “kukusanywa kutokana na kutawanywa kwao kwa siku nyingi, kutoka visiwa vya bahari, na kutoka pande nne za dunia”2 na kurejeshwa kwenye “nchi zao za urithi.”3 Rais Russell M. Nelson amesema mara nyingi na kwa nguvu zaidi kuhusu kukusanyika huku, akiita “kitu muhimu zaidi kinachotokea duniani.”4

Je, ni nini dhumuni la kukusanyika huku?

Kwa njia ya ufunuo kwa Nabii Joseph Smith, Bwana alitambulisha dhumuni moja la ulinzi wa watu wa agano. Yeye alisema, “Kukusanyika pamoja juu ya nchi ya Sayuni, na vigingi vyake, [kutakuwa] kwa ajili ya ulinzi, na kwa ajili ya kimbilio kutokana na dhoruba, na kutokana na ghadhabu ambayo itamwagwa pasipo kipimo juu ya dunia yote.”5 “Ghadhabu” katika muktadha huu inaweza kueleweka kama matokeo ya asili ya kuenea kwa kutokutii sheria na amri za Mungu.

Muhimu zaidi, kukusanyika ni kwa dhumuni la kuleta baraka za wokovu na kuinuliwa kwa wote walio tayari kuzipokea. Ndivyo ambavyo ahadi za agano kwa Ibrahimu zinatimia. Bwana alimwambia Ibrahimu kwamba kupitia uzao na ukuhani wake “familia zote za dunia zitabarikiwa, hata kwa baraka za injili, ambazo ni baraka za wokovu, hata za uzima wa milele.”6 Rais Nelson alielezea katika njia hii: “Tunapokumbatia injili na kubatizwa, tunajichukulia juu yetu wenyewe jina takatifu la Yesu Kristo. Ubatizo ni lango ambalo hutupeleka kwenye kuwa warithi wa pamoja wa ahadi zote zilizotolewa na Bwana kwa Ibrahimu, Isaka, Yakobo na uzao wao.”7

Mnamo mwaka 1836, Musa alimtokea Nabii Joseph Smith huko katika Hekalu la Kirtland na “kumkabidhi … funguo za kukusanyika kwa Israeli kutoka sehemu nne za dunia.”8 Katika tukio hilo hilo , Elia alitokea na “ kukabidhi kipindi cha injili ya Ibrahimu, akisema kwamba kupitia sisi na uzao wetu vizazi vyote baada yetu vitabarikiwa.”929 Kwa mamlaka haya, sasa tunaipeleka injili ya Yesu Kristo—habari njema ya ukombozi kupitia Kwake—sehemu zote na watu wote duniani na kuwakusanya wote walio tayari kuingia katika agano la injili. Wanakuwa “uzao wa Ibrahimu, na kanisa na ufalme, na wateule wa Mungu.”10

Katika tukio hilo hilo ndani ya Hekalu la Kirtland kulikuwa na mjumbe wa tatu mbinguni aliyewatokea Joseph Smith na Oliver Cowdery. Ninamzungumzia nabii Eliya, na ni mamlaka aliyoyarejesha ndiyo ninayotaka kuyazungumzia leo.11 Uweza wa kuhalalisha ibada zote za ukuhani na kuzifanya zifungwe kote duniani na mbinguni—uweza kwa kuunganisha—ni wa lazima kwa ajili ya kukusanyika na kuwatayarisha watu wa agano pande zote mbili za pazia.

Miaka ya mwanzoni, Moroni aliweka wazi kwa Joseph Smith kwamba Eliya ataleta mamlaka muhimu ya ukuhani: “Nitaufunua kwako Ukuhani kwa mkono wa Eliya nabii.”12 Joseph Smith baadaye alielezea: “Kwa nini amtume Eliya? Kwa sababu yeye anashikilia funguo za mamlaka ya kutumikia katika ibada zote za Ukuhani; na [isipokuwa] mamlaka hayo yametolewa, ibada hizo haziwezi kutolewa katika haki”13—hiyo ni kusema kwamba, ibada hizo hazingeweza kuwa halali kwa muda na kwa milele.14

Katika mafundisho sasa yanayotambuliwa kama maandiko katika Mafundisho na Maagano, Nabii alitangaza: “Yawezekana kwa wengine ikaonekana ni mafundisho mazito sana ambayo tunayazungumzia—uwezo ambao huandika au hufunga duniani na mbinguni.” Hata hivyo, katika umri wote wa ulimwengu, wakati wowote Bwana alipokuwa ametoa kipindi cha ukuhani kwa mtu yeyote kwa ufunuo halisi, au kwa kundi lolote la wanadamu, uwezo huu daima umekuwa ukitolewa. Kwa sababu hiyo, lolote watu wale walilolifanya katika mamlaka, katika jina la Bwana, na wakalifanya kwa ukweli na kwa uaminifu, na kutunza kwa usahihi na uaminifu kumbukumbu hiyo, lilikuwa sheria duniani na mbinguni, na haikuweza kuondolewa, kulingana na matamko ya Yehova mkuu.15

Huwa tunadhani kwamba mamlaka ya kuunganisha yanatumika tu kwa aina fulani ya ibada za hekaluni, lakini mamlaka hayo ni muhimu katika kufanya ibada yoyote kuwa halali na yenye kuunganisha baada ya kifo.16 Nguvu ya kuunganisha huweka muhuri wa uhalali kwenye ubatizo wako, kwa mfano, ili kwamba ubatizo huo utambulikane hapa na mbinguni. Hatimaye, ibada zote za ukuhani zinatekelezwa chini ya funguo za Rais wa Kanisa, na kama Rais Joseph Fielding Smith alivyoelezea: “Yeye [Rais wa Kanisa] ametupa sisi mamlaka, ameweka nguvu za kuunganisha katika ukuhani wetu, kwa sababu yeye anashikilia funguo hizo.”17

Kuna dhumuni jingine muhimu katika kukusanyika kwa Israeli ambalo lina maana maalumu tunapozungumzia kuhusu kufunga duniani na mbinguni—nalo ni ujenzi na uendeshaji wa mahekalu. Nabii Joseph Smith alifundisha: “Ni nini lengo la kukusanya … watu wa Mungu katika kila kipindi chochote cha ulimwengu? … Lengo kuu lilikuwa kumjengea Bwana nyumba ambayo kwayo angeweza kufunua kwa watu Wake ibada za nyumba Yake na utukufu wa ufalme Wake, na kuwafundisha watu njia ya wokovu; kwani kuna baadhi ya ibada na kanuni ambazo, wakati zinapofundishwa na kutekelezwa, lazima zifanyike mahali au katika nyumba iliyojengwa kwa kusudi hilo.”18

Uhalali ambao nguvu ya kuunganisha unatoa kwa ibada za ukuhani inajumuisha, ndiyo, ibada zinazofanywa katika mahali ambapo Bwana amepateua—hekalu Lake. Hapa tunaona ukuu na utakatifu wa nguvu ya kuunganisha—unafanya wokovu wa mtu binafsi na kuinuliwa kwa familia uwezekane ulimwenguni kote kwa watoto wote wa Mungu popote na kwa kipindi chochote walichoishi duniani. Hakuna thiolojia au falsafa au mamlaka inayoweza kulingana na fursa hii inayojumuisha wote. Nguvu hii ya kuunganisha ni onyesho kamilifu la haki, rehema na upendo wa Mungu.

Kwa kuweza kuifikia nguvu ya kuunganisha, mioyo yetu kwa inawageukia wale waliotutangulia. Kusanyiko la siku za mwisho ndani ya agano linavuka ng’ambo ya pazia. Katika utaratibu mkamilifu wa Mungu, walio hai hawawezi kupata uzima wa milele katika utimilifu wote pasipo kutengeneza miunganiko imara kwa “mababu,” wahenga wetu. Vile vile, maendeleo ya wale ambao tayari wako upande mwingine, au ambao bado hawajavuka kupitia pazia la kifo pasipo kufaidika na kuunganishwa, hawakamiliki hadi pale ibada ya uwakilishi itakapowaunganisha wao na sisi, watoto wao, na sisi kuunganishwa na wao katika utaratibu wa kiungu.19 Ahadi ya kusaidiana ng’ambo ya pazia inaweza kuainishwa kama ahadi ya agano, sehemu ya agano jipya na lisilo na mwisho. Katika maneno ya Joseph Smith, tunataka “kuwaunganisha wafu wetu ili wafufuke pamoja na [sisi] katika ufufuko wa kwanza.”20

Onyesho la juu zaidi na takatifu zaidi la nguvu ya kuunganisha ni katika unganiko la milele la mwanamume na mwanamke katika ndoa na unganiko la mwanadamu kwa vizazi vyao vyote. Kwa sababu mamlaka ya kuendesha ibada hizi ni matakatifu sana, Rais wa Kanisa binafsi husimamia unaibishaji wake kwa wengine. Rais Gordon B. Hinckley wakati mmoja alisema, “Nimesema mara nyingi kwamba kama hakuna kingine chochote kilichokuja kutokana na majonzi yote na masumbuko na maumivu ya urejesho kuliko nguvu ya kuunganisha ya ukuhani mtakatifu ya kuunganisha familia pamoja milele, kingekuwa ndicho cha thamani kwa gharama yake yote.”21

Pasipo kuunganisha ambako kunatangeneza familia za milele na kuunganisha vizazi hapa na baada ya hapa, tungeachwa milele pasipo kuwa na mizizi wala matawi, ambako ni kuwa pasipo nasaba wala uzao. Ni hali hii ovu, ya kutounganika ya watu binafsi, kwa upande mmoja, au miunganiko ambayo inapinga ndoa na uhusiano wa familia ambayo Mungu ameiteua,22 kwa upande mwingine, ambayo ingechafua dhumuni halisi la kuumbwa kwa dunia na uzoefu wetu hapa duniani. Kama hiyo ingekuwa kawaida, ingewezekana kwa dunia kupigwa kwa laana au “kuharibiwa kabisa” wakati wa kuja kwa Bwana.23

Tunaweza kuona kwa nini “ndoa kati ya mwanamume na mwanamke imeamriwa na Mungu na kwamba familia ni kiini cha mpango wa Muumbaji kwa hatima ya milele ya watoto Wake.”24 Wakati huo huo, tunatambua kwamba katika wakati huu usio mkamilifu, huu sio uhalisia au hata uwezekano wa uhalisia kwa baadhi. Lakini tunalo tumaini katika Yesu Kristo. Wakati tukimngojea Bwana, Rais M. Russell Ballard anatukumbusha kwamba “maandiko na manabii wa siku za mwisho wanathibitisha kwamba kila mtu aliye mwaminifu katika kushika maagano ya injili atapata fursa ya kuinuliwa.”25

Baadhi wamepitia hali za ndoa zisizo na furaha na zisizo nzuri na wanahisi hamu ndogo ya uhusiano wa milele wa familia. Mzee David A. Bedner alitamka hivi: “Kwenu ninyi mliopitia maumivu ya moyo ya talaka katika familia zenu au kuhisi maumivu ya kuvunjika kwa uaminifu, tafadhali kumbukeni [kwamba mpangilio wa Mungu wa familia] unaanza tena na wewe! Kiungo kimoja katika mnyororo wa vizazi vyako yawezekana kimevunjika, lakini viungo vingine viadilifu na kile kinachobaki katika ule mnyororo hata hivyo ni muhimu milele. Unaweza ukaongeza nguvu katika mnyororo wako na pengine hata kusaidia kurejesha vile viungo vilivyovunjika. Kazi hiyo itakamilishwa moja baada ya nyingine.”26

Katika ibada ya mazishi ya Dada Pat Holland, mke wa Mzee Jeffrey R. Holland Julai iliyopita, Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Baada ya muda, Patricia na Jeffrey wataungana tena. Kisha baadaye wataungana na watoto wao na uzao wao washika maagano ili kupata utimilifu wa shangwe ambayo Mungu ameweka ghalani kwa ajili ya watoto Wake walio waaminifu. Kwa kujua hilo, tunaelewa kwamba tarehe muhimu katika maisha ya Patricia haikuwa tarehe yake ya kuzaliwa au tarehe yake ya kufariki dunia. Siku yake muhimu zaidi ilikuwa Juni 7, 1963, wakati yeye na Jeff walipounganishwa katika Hekalu la Saint.George. … Kwa nini hili ni muhimu sana? Kwa sababu dhumuni hasa la kuumbwa kwa dunia lilikuwa kwamba familia zingeundwa na kuunganishwa kila mmoja kwa mwingine. Wokovu ni jambo la binafsi, lakini kuinuliwa ni jambo la famiia. Hakuna anayeweza kuinuliwa peke yake.”

Siyo siku nyingi sana, mimi na mke wangu tuliungana na rafiki yetu mpendwa katika chumba cha kuunganishwa cha Hekalu la Bountiful Utah. Kwa mara ya kwanza nilikutana na rafiki huyu wakati akiwa mtoto huko Cordoba, Argentina. Mimi pamoja na mmisionari mwenzangu tulikuwa tukitafuta watu wa kuwafundisha katika ujirani wetu nyumba kadhaa kutoka ofisi ya misheni, na yeye alitufungulia mlango tulipofika nyumbani kwao. Baada ya muda, yeye na mama yake na ndugu zake wakajiunga na Kanisa, na wamebaki kuwa waumini waaminifu. Sasa ni mwanamke mwenye kupendeza, na siku hiyo tulikuwa hekaluni tukiunganisha wazazi wake waliofariki na kisha yeye kwa wazazi wake.

Wanandoa ambao kwa miaka mingi wamekuwa rafiki zake wa karibu waliwawakilisha wazazi wake kwenye madhabahu. Ulikuwa wakati wa hisia ambao ulikuja kuwa mtamu zaidi wakati rafiki yetu alipounganishwa kwa wazazi wake. Tulikuwa watu sita tu mchana huo tulivu mbali na ulimwengu, na bado moja ya jambo muhimu zaidi linalotokea duniani lilikuwa likiendelea kutokea. Nilifurahishwa na kwamba jukumu na uhusiano wangu umekuwa duara kamili kutoka kubisha mlango wao kama mmisionari kijana hadi sasa miaka hii mingi baadaye, nikifanya ibada ya kuunganishwa ambayo inamuunganisha yeye kwa wazazi wake na vizazi vilivyopita.

Hili ni tukio linalofanyika mara kwa mara ulimwenguni kote katika mahekalu. Hii ni hatua ya mwisho katika kuwakusanya watu wa agano. Ni heshima ya hali ya juu sana ya uumini wako katika Kanisa la Yesu Kristo! Ninakuahidi kwamba unapotafuta kwa uaminifu heshima hiyo, baada ya muda au milele hakika itakuwa yako.

Ninashuhudia kwamba nguvu na mamlaka ya kuunganisha yaliyorejeshwa duniani kupitia Joseph Smith ni halisi, kwamba kile kilichofungwa duniani ni kweli kimefungwa mbinguni. Ninashuhudia kwamba Rais Russell M. Nelson, kama Rais wa Kanisa, ni mtu mmoja pekee duniani leo ambaye kwa funguo zake anaelekeza matumizi ya uweza huu mkuu. Ninashuhudia kwamba Upatanisho wa Yesu Kristo umefanya maisha ya milele yawezekane na uwezekano wa uhusiano wa familia zilizoinuliwa uwe kweli. Katika jina la Yesu Kristo, amina.