Mkutano Mkuu
Kwa Manufaa ya Vizazi Vyako
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Kwa Manufaa ya Vizazi Vyako

Usiwe kiunganishi dhaifu katika mnyororo huu wa kupendeza wa imani uliyoianzisha, au uliyoipokea kama urithi. Kuwa kiunganishi imara.

Miaka michache iliyopita, wakati nikihudumu katika Eneo la Kaskazini Magharibi mwa Amerika Kusini na nikiishi Peru, nilipata uzoefu wa kupendeza ambao ningependa kuushiriki nanyi.

Ulitokea wakati nikirejea nyumbani baada ya wikiendi yenye shughuli nyingi za majukumu. Hatimaye baada ya kukamilisha mchakato wa uhamiaji kwenye uwanja wa ndege, nilikutana na dereva taksi mkarimu kutoka kwenye huduma zetu za kawaida za taksi akiningojea. Alinipeleka kwenye gari lake, na niliketi nyuma tayari kupumzika na kufurahia safari ya nyumbani yenye utulivu. Baada ya kuvuka mitaa kadhaa, dereva alipokea simu kutoka kwa msimamizi wake, akimwambia kwamba nilichukua taksi ambayo haikuwa kwa ajili yangu. Gari tofauti lilikuwa limewekwa tayari kwa ajili yangu na msimamizi alimwomba anirudishe uwanja wa ndege ikiwa ningetaka kubadili gari. Nilimwambia haikuwa lazima na tungeweza tu kuendelea na safari. Baada ya dakika chache za ukimya, alinitazama kupitia kioo cha kutazama nyuma na kuuliza, “Wewe ni Mmormoni, sivyo?”

Hakika, baada ya swali hilo la mwaliko, nilijua nyakati zangu za ukimya zilikuwa zimekwisha. Nisingeweza kukataa kuchunguza ni wapi swali lake lingetupeleka.

Nilijifunza kwamba jina lake lilikuwa Omar, jina la mkewe lilikuwa Maria Teresa na walikuwa na watoto wawili—Carolina, miaka 14, na Rodrigo, miaka 10. Omar amekuwa muumini wa Kanisa tangu alipokuwa mtoto. Familia yake ilishiriki kikamilifu, lakini kwa wakati fulani, wazazi wake waliacha kwenda kanisani. Omar aliacha kabisa kushiriki kikamilifu alipokuwa na miaka 15. Kwa sasa alikuwa na miaka 40.

Wakati huo nilitambua kwamba sikukosea kuchukua taksi. Haikuwa bahati nasibu! Nilimwambia mimi nilikuwa nani na kwamba nilikuwa ndani ya taksi yake kwa sababu Bwana alikuwa akimwita arejee kwenye zizi Lake.

Kisha tulizungumzia wakati ambapo yeye na familia yake walipokuwa waumini hai wa Kanisa. Alikuwa na kumbukumbu zenye hisia nzuri za nyakati za kupendeza za jioni ya familia na baadhi ya nyimbo za Msingi. Kisha aliimba maneno machache ya “Mimi ni Mtoto wa Mungu.”1

Baada ya kupata anwani yake, namba ya simu na ruhusa ya kuishiriki na askofu wake, nilimwambia nitatafuta njia ili niwepo kanisani kwenye siku yake ya kwanza ya kurejea kanisani. Tulikamilisha safari yetu kutoka uwanja wa ndege mpaka nyumbani kwangu, kadhalika safari yetu fupi ya historia yake ya nyuma, na tuliachana.

Wiki chache baadaye, askofu wake alinipigia simu akinijulisha Omar alikuwa akipanga kuhudhuria kanisani siku fulani ya Jumapili. Nilimwambia ningekuwepo. Jumapili ile, Omar alikuwepo pale na mwanaye. Mkewe na binti bado hawakutaka. Miezi michache baadaye, askofu wake alinipigia tena, wakati huu kuniambia kwamba Omar atakuwa akimbatiza mkewe na watoto wake wawili, na alinialika niwepo. Hapa kuna picha ya Jumapili hiyo pale walipothibitishwa kuwa waumini wa Kanisa.

Picha
Mzee Godoy na familia ya Omar Jumapili waliyothibitishwa.

Jumapili ileile, nilimwambia Omar na familia yake kwamba ikiwa wangejitayarisha, ndani ya mwaka mmoja, ningepata heshima ya kufanya uunganisho wao ndani ya Hekalu la Lima Peru. Hapa kuna picha ya wakati huo wa kukumbukwa kwetu sote, iliyopigwa mwaka mmoja baadaye.

Picha
Mzee Godoy na familia ya Omar hekaluni.

Kwa nini ninashiriki nanyi uzoefu huu? Ninaushiriki kwa madhumuni mawili.

Kwanza, kuzungumza na wale waumini wazuri ambao kwa sababu fulani wameanguka kutoka kwenye injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo. Pili, kuzungumza pia na wale waumini wanaoshiriki leo ambao pengine si waaminifu kwenye maagano yao kama wanavyopaswa kuwa. Katika hali zote mbili, vizazi vijavyo vinaathirika, na baraka na ahadi ambazo ziliwekwa kwa ajili ya vizazi ziko hatarini.

Ngoja tuanze na hali ya kwanza, waumini wazuri ambao wameiacha njia ya agano, kama ilivyotokea kwa rafiki yangu wa Peru Omar. Nilipomuuliza kwa nini aliamua kurejea, alisema ilikuwa kwa sababu yeye na mkewe walihisi watoto wao wangekuwa wenye furaha katika maisha wakiwa na injili ya Yesu Kristo. Alihisi ulikuwa wakati wa kurejea kanisani kwa manufaa ya watoto wao.

Inahuzunisha sana wakati tunapokutana na waumini wa Kanisa wasioshiriki kikamilifu ambao wakati fulani walikuwa na injili ndani ya familia zao na waliipoteza kwa sababu ya maamuzi ya wazazi wao au bibi na babu ya kuacha kwenda kanisani. Uamuzi huo ungeweza kuwa na matokeo kwenye vizazi vyao milele!

Watoto na wajukuu wao wamezuiliwa kutoka kwenye ulinzi na baraka za injili ya Yesu Kristo katika maisha yao. Hata ya kuvunja moyo zaidi, wamepoteza ahadi ya familia ya milele ambayo ilikuwepo hapo awali. Uamuzi wa mtu mmoja umeathiri mnyororo wote wa vizazi. Urithi wa imani umevunjwa.

Hata hivyo, kama tunavyojua, chochote kilichovunjika kinaweza kuungwa kupitia Yesu Kristo. Kwa sababu hii, tafadhali zingatia mwaliko huu kutoka kwa Rais Russell M. Nelson: “Sasa, ikiwa umechepuka kutoka njiani, naomba nikualike kwa tumaini lote la moyo wangu tafadhali rudi. Bila kujali wasiwasi wako, changamoto zako, kuna nafasi yako katika hili, Kanisa la Bwana. Wewe na vizazi ambavyo havijazaliwa bado mtabarikiwa kwa matendo yenu kama mtarejea sasa katika njia ya agano.”2

Sasa, ngoja tuzungumzie hali ya pili, waumini wanaoshiriki leo ambao pengine si waaminifu kama wanavyopaswa kuwa. Kama vile maamuzi ya jana yanavyoathiri uhalisia wa leo, maamuzi ya leo yataathiri wakati wetu ujao na ya wanafamilia wetu.

Rais Dallin H. Oaks alitufundisha:

“Injili ya urejesho ya Yesu Kristo inatuhimiza kufikiria kuhusu wakati ujao. … Inafundisha mawazo makuu kuhusu wakati ujao ili kuongoza matendo yetu leo.

“Kinyume chake, sote tunawajua watu ambao wanajihusisha tu na wakati uliopo: wanaitumia leo, wanaifurahia leo na hawafikirii wakati ujao.

“… Tunapofanya maamuzi ya sasa, tunapaswa daima kujiuliza, ‘Hili litaongoza wapi?’”3 Je, maamuzi yetu ya sasa yatatuongoza kwenye shangwe sasa na milele, au yatatuongoza kwenye huzuni na machozi?

Baadhi wanaweza kudhani, “Hatuhitaji kuhudhuria kanisani kila Jumapili,” au “Tutalipa zaka yetu mambo yakiwa mazuri,” au “Sitawaunga mkono viongozi wa Kanisa kwenye mada hii.”

“Lakini,” wanasema, “tunajua Kanisa ni la kweli, na kamwe hatutaiacha injili ya Yesu Kristo.”

Wale wenye mawazo kama haya hawatambui madhara hasi ambayo aina hii ya uumini “vuguvugu” italeta kwenye maisha yao na maisha ya vizazi vyao. Wazazi wanaweza kubaki washiriki hai, lakini hatari ya kuwapoteza watoto wao ni kubwa—katika maisha haya na milele.

Kuhusu wale ambao hawataurithi utukufu wa selestia pamoja na familia zao, Bwana anasema, “Hawa ndiyo wale ambao si majasiri katika ushuhuda wa Yesu; kwa hiyo, hawatapokea taji la utukufu wa ufalme wa Mungu wetu.”4 Je, hilo ndilo tunalolitaka kwetu au kwa watoto wetu? Je, hatupaswi kuwa majasiri zaidi na si vuguvugu kwa manufaa yetu na kwa manufaa ya vizazi vyetu?

Mzee M. Russell Ballard pia alizungumzia wasiwasi sawa na huo:

Kwa wengine, mwaliko wa Kristo wa kuamini na kubaki unaendelea kuwa mgumu. … Baadhi ya wafuasi wanapata shida kuelewa sera au mafundisho mahususi ya Kanisa. Wengine hupata wasiwasi katika historia yetu au katika udhaifu wa baadhi ya waumini na viongozi, wa zamani na wa sasa.

“… Uamuzi wa ‘kutotembea tena’ na waumini wa Kanisa na viongozi waliochaguliwa na Bwana utakuwa na athari ya muda mrefu ambayo haiwezi kuonekana hivi sasa.”5

Urithi wenye huzuni ulioje kuutoa—na kwa sababu ipi? Kwa sababu yoyote ile, haitoshi kupuuzia madhara hasi ya kiroho utakayoleta kwa vizazi vya mbeleni.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, ikiwa unapitia moja ya hali hizi mbili nilizozitaja katika ujumbe wangu, tafadhali tafakari upya maamuzi yako. Mnajua kuna mpango kwa ajili yetu katika maisha haya. Mnajua kwamba familia zinaweza kuwa za milele. Kwa nini uiweke yako hatarini? Usiwe kiunganishi dhaifu katika mnyororo huu wa kupendeza wa imani uliyoianzisha, au uliyoipokea kama urithi. Kuwa kiunganishi imara. Ni zamu yako kufanya hilo na Bwana anaweza kukusaidia.

Kutoka kwenye kina cha moyo wangu, ninakualika ulifikirie, utazame mbele na utathmini “ni wapi hili litaongoza” na, ikiwezekana, kuwa jasiri vya kutosha kuifanya upya njia yako kwa manufaa ya vizazi vyako. Katika jina la Yesu Kristo, amina.