Mkutano Mkuu
Kukaza Mwendo, Kuifikilia Mede
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Kukaza Mwendo, Kuifikilia Mede

Sio sana juu ya kile tunachopitia maishani bali kile tunachokuwa.

Ninaposoma kitabu cha Matendo ya Mitume na nyaraka za Paulo, ninashangazwa na jinsi Paulo alivyoongozwa kwa upendo na shukrani katika kutumikia, kufundisha na kushuhudia juu ya Yesu Kristo. Ni jinsi gani mtu kama huyu anaweza kutumikia kwa upendo na shukrani kama hiyo, hasa ukizingatia mateso yake makubwa? Ni nini kilichomchochea Paulo kutumikia? “Ninakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”1

Kukaza mwendo kuifikilia mede ni kuendelea kwa uaminifu kwenye “njia nyembamba iliyosonga inayoongoza kwenye uzima wa milele”2 tukiwa na Mwokozi wetu na Baba Yetu wa Mbinguni. Paulo alitathmini mateso yake kama “si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu”3 Barua ya Paulo kwa Wafilipi, ambayo aliiandika wakati alipokuwa amefungwa gerezani, ni barua ya shangwe kubwa na furaha na ya kutia moyo kwetu sote, hasa katika wakati huu mgumu wa kutokuwa na uhakika. Sote tunahitaji kupata ujasiri kutoka kwa Paulo: “nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu Bwana wangu: ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi, ili nimpate Kristo.”4

Wakati tunapoangalia huduma ya Paulo, tunahamasishwa na kuinuliwa na “Mapaulo” wetu katika siku zetu, ambao pia hutumikia, kufundisha, na kushuhudia kwa upendo na shukrani kati ya changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao na katika maisha ya wapendwa wao. Uzoefu niliokuwa nao miaka tisa iliyopita ulinisaidia kutambua umuhimu wa kukaza mwendo kuifikilia mede.

Mnamo mwaka 2012, nilipoingia kwa mara ya kwanza katika mkutano wa viongozi wa mkutano mkuu, sikuweza kujizuia kuhisi kuzidiwa na kutostahili. Akilini mwangu kulikuwa na sauti ikirudia rudia, “Wewe si wa hapa! Kosa kubwa lilikuwa limefanywa!” Mara tu nilipokuwa nikijaribu kupata mahali pa kuketi, Mzee Jeffrey R. Holland aliniona. Alikuja kwangu na kusema, “Edward, ni vyema kukuona hapa”, na kwa upole aligusa uso wangu. Nilijihisi kama mtoto! Upendo wake na kumbatio vilinipa joto na kunisaidia kuhisi roho ya kustahili, roho ya undugu. Siku iliyofuata, nilimwona Mzee Holland akifanya yale yale aliyonifanyia siku iliyopita, kwa ukarimu akigusa uso wa Mzee Dallin H. Oaks, ambaye yuko nafasi ya juu kwake!

Wakati huo nilihisi upendo wa Bwana kupitia wanaume hawa tunaowaidhinisha kama manabii, waonaji, na wafunuzi. Mzee Holland, kupitia kwa matendo yake ya ukarimu, ya asili, alinisaidia kushinda ubinafsi wangu na hisia zangu za kutostahili. Alinisaidia kufokasi kwenye kazi takatifu na ya shangwe ambayo kwayo nilikuwa nimeitwa—kuleta nafsi kwa Kristo. Yeye, kama Paulo wa zamani, alinielekeza kukaza mwendo kuifikilia mede.

La kufurahisha, Paulo anatuhimiza tukaze mwendo, huku akituita tusahau yaliyopita—hofu zetu za zamani, fokasi yetu ya zamani, makosa yetu ya zamani, na huzuni yetu ya zamani. Yeye anatualika, kama vile nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, “kwenye mtazamo mpya zaidi, mtakatifu zaidi.”5 Ahadi ya Mwokozi ni halisi: “Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza: na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.”6

Katika hotuba yangu ya kwanza ya mkutano mkuu, nilishiriki uzoefu wa mama yangu akinifundisha kufanya kazi katika shamba letu. “Kamwe usitazame nyuma,” alisema. “Tazama mbele kwa yale ambayo bado tunapaswa kufanya.”7

Kuelekea mwisho wa maisha yake, wakati Mama alipokuwa akipambana na saratani, aliishi pamoja na mimi na Naume. Usiku mmoja nilimsikia akilia chumbani kwake. Maumivu yake yalikuwa makali, hata baada ya kumeza dozi yake ya mwisho ya kila siku ya morphine masaa mawili tu kabla.

Niliingia chumbani kwake na kulia naye. Nilimwombea kwa sauti apate afueni ya haraka kutokana na maumivu yake. Na kisha alifanya kitu kile kile alichokuwa akifanya shambani miaka kadhaa iliyopita: alipumzika kidogo na kunifundisha somo. Sitasahau kamwe uso wake wakati huo: dhaifu, aliyeteseka na mwenye maumivu mengi, akimtazama kwa huruma mwanaye mwenye huzuni. Alitabasamu kupitia machozi yake, akanitazama moja kwa moja machoni na kusema, “Sio juu yako au mtu mwingine yeyote, lakini ni juu ya Mungu ikiwa maumivu haya yataisha au la.”

Niliketi wima kimya. Yeye pia alikaa kimya. Tukio linabaki dhahiri akilini mwangu. Usiku ule, kupitia mama yangu, Bwana alinifundisha somo ambalo litakaa nami milele. Wakati mama yangu alipoelezea kukubali kwake mapenzi ya Mungu, nilikumbuka sababu ya Yesu Kristo kuteseka katika Bustani ya Gethsemane na msalabani Golgotha. Alisema: “Tazama, nimewapatia injili yangu, na hii ndiyo injili [yangu] ambayo nimewapatia—kwamba nilikuja ulimwenguni kufanya mapenzi ya Baba, kwa sababu alinituma.”8

Picha
Kristo katika Gethsemane

Ninatafakari juu ya maswali ya kinabii ya nabii wetu mpendwa Rais Nelson kwetu kwenye mkutano mkuu uliopita. Rais Nelson aliuliza: “Je, wewe uko radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yako? Je, wewe uko radhi kuacha Mungu awe ushawishi muhimu zaidi katika maisha yako? … Je, utaruhusu sauti Yake ichukue … kipaumbele cha juu zaidi ya tamanio jingine lolote? Je, wewe uko radhi kuruhusu mapenzi yako yamezwe katika Yake?”9 Mama yangu angejibu kwa “ndiyo,” yenye hisia lakini thabiti, na waumini wengine waaminifu wa Kanisa kote ulimwenguni pia wangejibu kwa “ndiyo,” yenye hisia lakini thabiti. Rais Nelson, asante kwa kutuhamasisha na kutuinua kwa maswali haya ya kinabii.

Hivi karibuni, nilikuwa na mazungumzo huko Pretoria, Afrika Kusini, na askofu aliyemzika mkewe na binti yake mtu mzima katika siku moja. Maisha yao yalichukuliwa na janga hili la ulimwengu la kirusi cha korona. Niliuliza alivyokuwa akiendelea. Jibu la Askofu Teddy Thabete liliimarisha azimio langu la kufuata maneno na ushauri kutoka kwa manabii, waonaji na wafunuzi wa Bwana. Askofu Thabete alijibu kwamba daima kuna tumaini na faraja katika kujua kwamba Mwokozi amejichukulia juu Yake maumivu ya watu Wake ili aweze kujua jinsi ya kutusaidia.10 Kwa imani ya kina alishuhudia, “Ninashukuru kwa mpango wa wokovu, mpango wa furaha.” Kisha akaniuliza swali: “Je! Hii sio kile nabii wetu alichokuwa akijaribu kutufundisha katika mkutano huu uliopita?”

Wakati changamoto za maisha haya zitakuja kwetu sote kwa njia moja au nyingine, acha tufokasi kwenye lengo la sisi “kukaza mwendo kuifikilia mede,” ambayo ni “thawabu ya mwito mkuu wa Mungu.”11

Mwaliko wangu mnyenyekevu kwetu sisi sote ni kutokata tamaa! Tumeitwa “tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi, na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu.”12

Sio sana juu ya kile tunachopitia maishani bali kile tunachokuwa. Kuna shangwe katika kukaza Mwendo Kuifikilia Mede. Ninashuhudia kwamba Yeye ambaye Alishinda yote Atatusaidia tunapomtazama. Katika jina la Yesu Kristo, amina.