Mkutano Mkuu
Kuhakikisha Hukumu ya Haki
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Kuhakikisha Hukumu ya Haki

Ili kuhakikisha hukumu ya haki, dhabihu ya upatanisho ya mwokozi itaondoa magugu yote ya ujinga na miiba ya maumivu ya uchungu yaliyosababishwa na wengine.

Kitabu cha Mormoni Kinafundisha Mafundisho ya Kristo.

Oktoba iliyopita, Rais Russell M. Nelson alitupa changamoto kufikiria jinsi ambavyo maisha yetu yangekuwa tofauti kama “uelewa wetu tulioupata kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni ghafla ungeondolewa?”1 Nimetafakari swali hili, kama nilivyo na uhakika wengi wenu mmefanya hivyo. Wazo moja limenijia mara kwa mara—bila Kitabu cha Mormoni na uwazi wake kuhusu mafundisho ya Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho, wapi ningeenda kwa ajili ya amani?

Mafundisho ya Kristo—ambayo yana kanuni za wokovu na ibada za imani katika Kristo, toba, ubatizo, Kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuvumilia mpaka mwisho—yanafudishwa mara nyingi katika maandiko yote ya Urejesho lakini kwa nguvu mahususi katika Kitabu cha Mormoni.2 Mafundisho yanaanza na imani katika Kristo, na kila moja ya kipengele chake kinategemea imani katika dhabihu Yake ya upatanisho.

Kama Rais Nelson alivyofundisha, “Kitabu cha Mormoni kinatoa ukamilifu na uelewa kamili wenye mamlaka wa upatanisho wa Yesu Kristo unaoweza kupatikana sehemu yoyote.”3 Tunapoelewa zaidi kuhusu zawadi ya kiungu ya Mwokozi, ndivyo zaidi tutakavyokuja kujua, katika akili zetu na mioyo yetu,4 ukweli wa hakikisho la Rais Nelson kwamba “kweli za Kitabu cha Mormoni zina nguvu ya kuponya, kufariji, kurejesha, kusaidia, kuimarisha, kuliwaza, na kufurahisha nafsi zetu.”5

Upatanisho wa Mwokozi Unakidhi Mahitaji Yote ya Haki

Mchango muhimu na wenye kutoa amani wa Kitabu cha Mormoni kwa uelewa wetu wa Upatanisho wa Mwokozi ni mafundisho yake kwamba dhabihu ya huruma ya Kristo inakamilisha mahitaji yote ya haki. Kama Alma alivyoeleza: “Mungu mwenyewe hulipia dhambi za ulimwengu, kutimiza mpango wa rehema, kuwezesha mahitaji ya haki, kwamba Mungu angekuwa mkamilifu, na Mungu mwenye haki, na Mungu wa huruma pia.”6 Mpango wa Baba wa huruma7—kile ambacho maandiko pia yanauita mpango wa furaha8 au mpango wa wokovu9—usingeweza kukamilika isipokuwa mahitaji yote ya haki yametimizwa.

Lakini ni yapi hasa “mahitaji ya haki”? Fikiria Uzoefu wa Alma. Kumbuka kwamba kama kijana, Alma alikwenda huku na huko akitafuta “kuliharibu Kanisa.”10 Kwa kweli, Alma alimwambia mwanaye Helamani kwamba “aliadhibiwa na uchungu wa jahanamu” kwa sababu alikuwa “ameua watoto wengi wa [Mungu]” kwa “kuwaelekeza kwenye maangamizo.”11

Alma alimwelezea Helamani kwamba amani hatimaye ilikuja kwake wakati “alipokumbuka” mafundisho ya baba yake “kuhusu kuja kwa mmoja aitwaye … Yesu Kristo … kulipia dhambi za ulimwengu.”12 Alma mwenye kujuta alisihi kwa ajili ya rehema ya Kristo13 na kisha alihisi furaha na faraja wakati alipotambua kwamba Kristo alikuwa amefanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zake na kulipa yote ambayo haki ilihitaji. Tena, ni nini haki ingehitaji kwa Alma? Kama Alma mwenyewe alivyofundisha baadaye, “Hakuna kitu kichafu kitakachorithi ufalme wa Mungu.”14 Hivyo, sehemu ya faraja ya Alma lazima ilikuwa kwamba, isipokuwa rehema iingilie kati, haki ingemzuia yeye kurudi kuishi na Baba wa Mbinguni.15

Mwokozi Huponya Majeraha Tusiyoweza Kuponya

Lakini je, furaha ya Alma ililenga kwake peke yake—juu ya yeye kuepuka adhabu na yeye kuwa na uwezo wa kurudi kwa Baba? Tunajua kwamba Alma pia alipata maumivu makali kwa ajili ya hao ambao alikuwa amewapotosha kutoka kwenye ukweli.16 Lakini Alma asingeweza kuwaponya na kuwarudisha wale wote aliowapotosha. Asingeweza mwenyewe kuhakikisha kwamba wangepewa fursa ya haki kujifunza mafundisho ya Kristo na kubarikiwa kwa kuishi kanuni zake za furaha. Asingeweza kuwarudisha wale ambao walikuwa wamekufa wakiwa bado wamepofushwa na mafundisho yake ya uongo.

Kama Rais Boyd K. Packer alivyowahi kufundisha: “Wazo ambalo lilimwokoa Alma … ni hili: Kurejesha kile ambacho huwezi kurejesha, kuponya jeraha ambalo huwezi kuponya, kutengeneza kile ambacho ulikivunja na huwezi kukitengeneza ndio lengo hasa la upatanisho wa Kristo.”17 Ukweli wa furaha ambao akili za Alma “ziliukumbuka” haukuwa tu kwamba Yeye mwenyewe angeweza kufanywa msafi bali pia kwamba wale ambao aliwaumiza wangeweza kuponywa na kufanywa wazima.

Dhabihu ya Mwokozi Inahakikisha Hukumu ya Haki

Miaka mingi kabla Alma hajaokolewa na maandiko haya yenye hakikisho, Mfalme Benjamini alikuwa amefundisha kuhusu upana wa uponyaji uliotolewa na dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi. Mfalme Benjamini alitangaza kwamba “habari njema za shangwe kuu” zilitolewa kwake “na malaika kutoka kwa Mungu.”18 Miongoni mwa habari hizo njema ilikuwa ukweli kwamba Kristo angeteseka na kufa kwa ajili ya dhambi na makosa yetu ili kuhakikisha kwamba “ hukumu ya haki iweze kuja juu ya watoto wa watu.”19

Ni nini hasa “hukumu ya haki” inahitaji? Katika mstari unaofuata, Mfalme Benjamini alieleza kwamba ili kuhakikisha hukumu ya haki, damu ya Mwokozi ilifanya upatanisho “kwa ajili ya dhambi za wale ambao wameanguka kwa sababu ya dhambi ya Adamu” na ambao “wameaga dunia bila kuelewa nia ya Mungu juu yao, au ambao wametenda dhambi bila kujua.”20 Hukumu ya haki pia ilihitaji, alifundisha, kwamba “damu ya Kristo inalipiza dhambi za watoto wadogo.21

Maandiko haya yanafundisha mafundisho matukufu: dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi inaponya, kama zawadi ya bure, wale wanaofanya dhambi bila kujua—wale ambao, kama Yakobo anavyosema, “hakuna sheria iliyotolewa.”22 Kuwajibika kwa ajili ya dhambi kunategemea mwangaza tuliopewa na kiini chake ni uwezo wetu wa kutumia uhuru wa kuchagua.23 Tunajua ukweli huu wa kuponya na wa kuleta faraja kwa sababu tu ya Kitabu cha Mormoni na maandiko mengine ya Urejesho.24

Bila shaka, pale ambapo sheria imetolewa, pale ambapo sisi si wasiojua mapenzi ya Mungu, tunawajibika. Kama Mfalme Benjamini alivyosisitiza: “Ole kwa yule anayefahamu kwamba anamuasi Mungu! Kwani wokovu haumjii yeyote ila tu kwa kupitia toba na imani katika Bwana Yesu Kristo.”25

Hii pia ni habari njema ya mafundisho ya Kristo. Si tu Mwokozi anaponya na kurejesha wale wote wanaotenda dhambi kwa kutofahamu, bali pia, kwa wale wanaofanya dhambi dhidi ya nuru, Mwokozi hutoa uponyaji kwa sharti la toba na imani katika Yeye.26

Alma lazima “alikumbuka” kweli hizi mbili. Je, Alma kweli angehisi kile anachokielezea kama “shangwe … nzuri”27 kama angefikiri kwamba Kristo alimwokoa yeye lakini akiwaacha kwenye maumivu ya milele wale ambao aliwapotosha kutoka kwenye ukweli? Kwa hakika sivyo. Kwa Alma kuhisi amani iliyo timilifu, wale aliowaumiza pia walihitaji fursa ya kuponywa.

Lakini ni kwa jinsi gani wangeweza—au wale tunaoweza kuwa tumewaumiza—wanaweza kuponywa? Ingawa hatuelewi kikamilifu mbinu takatifu ambazo kwazo dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi inaponya na kurejesha, tunajua kwamba kuhakikisha hukumu ya haki, Mwokozi atasafisha magugu ya ujinga na miiba ya maumivu ya uchungu yanayosababishwa na wengine.28 Kwa hili Yeye anatuhakikishia kwamba watoto wote wa Mungu watapewa fursa, pamoja na maono yasiozuilika, kuchagua kumfuata Yeye na kukubali mpango mkuu wa furaha.29

Mwokozi Atarekebisha Kile Tulichovunja

Ni kweli hizi ambazo zingeweza kumletea Alma amani. Na ni kweli hizi ambazo zinapaswa kutuletea sisi amani kuu vilevile. Kama wanaume na wanawake wa asili, sote tunarushwa, au wakati mwingine kuangukiana kwa kishindo, na kusababisha madhara. Kama mzazi yoyote anavyoweza kushuhudia, maumivu yanayoambatana na makosa yetu si hasa hofu ya adhabu yetu wenyewe bali hofu kwamba tunaweza kuwa tumefupisha furaha ya watoto wetu au kwa njia nyingine tumewazuia kuona na kuelewa ukweli. Ahadi tukufu ya dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi ni kwamba licha ya makosa yetu kama yanavyowapa wazazi wasiwasi, Yeye anawachukulia watoto wetu bila lawama na anaahidi uponyaji kwa ajili yao.30 Na hata wanapokuwa wametenda dhambi dhidi ya nuru—kama wote tunavyofanya—mkono Wake wa rehema umenyooshwa31 na atawakomboa kama watamtazama Yeye na kuishi.32

Ingawa Mwokozi ana nguvu za kurekebisha kile tusichoweza kutengeneza, anatuamuru kufanya vyote tunavyoweza kufanya marekebisho kama sehemu ya toba yetu.33 Dhambi zetu na makosa yanaondoa si tu mahusiano yetu na Mungu bali pia mahusiano yetu na wengine. Wakati mwingine juhudi zetu za kuponya na kurejesha zinaweza kuwa za kawaida kama kuomba msamaha, lakini wakati mwingine marekebisho yanaweza kuhitaji miaka mingi ya juhudi za unyenyekevu.34 Hata hivyo, kwa nyingi za dhambi zetu na makosa, kwa kawaida hatuwezi kuwaponya kikamilifu wale tuliowaumiza. Ahadi nzuri kabisa, inayotoa-amani ya Kitabu cha Mormoni na injili ya urejesho ni kwamba Mwokozi atarekebisha vile vyote tulivyovivunja.35 Na pia Ataturekebisha sisi kama tutamgeukia kwa imani na kutubu juu ya madhara tuliyoyasababisha.36 Anatoa zawadi hizi zote mbili kwa sababu anatupenda sisi sote kwa upendo mkamilifu37 na kwa sababu ameahidi kuhakikisha hukumu ya haki ambayo inaheshimu vyote haki na rehema. Nashuhudia hii ni kweli katika Jina la Yesu Kristo, amina.