Mlango wa 8
Amoni anawafundisha watu wa Limhi—Anajulishwa kuhusu yale mabamba ishirini na nne ya Kiyaredi—Maandishi ya kale yanaweza kutafsiriwa na waonaji—Hakuna kipawa kikuu kuliko uonaji. Karibia mwaka 121 K.K.
1 Na ikawa kwamba baada ya mfalme Limhi kumaliza kuwazungumzia watu wake, kwani aliwazungumzia vitu vingi na ni vichache tu nilivyoandika katika kitabu hiki, aliwaambia watu wake vitu vyote kuhusu ndugu zao waliokuwa katika nchi ya Zarahemla.
2 Na akasababisha Amoni asimame mbele ya ule umati, na kuwaelezea yale yote ambayo yaliwapata ndugu zao tangu Zenivu aondoke kutoka nchi ile hadi ule wakati ambao yeye mwenyewe aliondoka kutoka nchi ile.
3 Na pia akakariri yale maneno ya mwisho ambayo mfalme Benjamini aliwafundisha, na akayafafanua kwa watu wa mfalme Limhi, ili wafahamu yale maneno yote ambayo alizungumza.
4 Na ikawa kwamba baada ya kufanya haya yote, kwamba mfalme Limhi alilikiza ule umati, na kusababisha kila mmoja arudi nyumbani kwake.
5 Na ikawa kwamba alisababisha yale mabamba ambayo yalikuwa na maandishi ya watu wake tangu watoke nchi ya Zarahemla, yaletwe mbele ya Amoni, ili ayasome.
6 Sasa, baada ya Amoni kusoma yale maandishi, mfalme alimuuliza kama anajua kutafsiri lugha, na Amoni akamwambia kwamba hangeweza.
7 Na mfalme akamwambia: Nikiwa nimehuzunishwa na masumbuko ya watu wangu, nilisababisha watu wangu arubaini na watatu wasafiri nyikani, ili pengine waweze kuipata nchi ya Zarahemla, ili tuwaombe ndugu zetu watukomboe kutoka utumwani.
8 Na walipotea huko nyikani kwa muda wa siku nyingi, lakini bado walikuwa na bidii, na hawakuipata ile nchi ya Zarahemla lakini walirejea katika nchi hii, baada ya kusafiri katika nchi iliyo miongoni mwa maji mengi, wakiwa wamegundua nchi iliyojaa mifupa ya wanadamu, na ya wanyama, na pia ilijaa mabaki ya majengo ya kila aina, wakiwa wamegundua nchi iliyomilikiwa na watu waliokuwa wengi kama Waisraeli.
9 Na ili kuthibitisha kwamba vitu walivyosema ni vya kweli wameleta mabamba ishirini na nne ambayo yamejaa michoro, na ni ya dhahabu kamili.
10 Na tazama, pia, wameleta dirii, ambazo ni kubwa, na ni za shaba nyeupe na shaba nyekundu, na zingali nzuri.
11 Na tena, wameleta panga, ambazo mipini yake imeharibika, na ndimi zake kupata kutu; na hakuna yeyote nchini anayeweza kutafsiri ile lugha au michoro iliyo kwenye mabamba. Kwa hivyo nilikuuliza: Je unaweza kutafsiri?
12 Nakuambia tena: Je, unajua yeyote anayeweza kutafsiri? Kwani natamani kwamba maandishi haya yatafsiriwe katika lugha yetu; kwani, pengine, yatatupatia ufahamu wa baki la wale watu walioangamizwa, kule maandishi haya yalikotokea; au, pengine, yatatupatia ufahamu wa hawa watu ambao wameangamizwa; na natamani kujua sababu ya kuangamizwa kwao.
13 Sasa Amoni akamwambia: Naweza kukuambia kwa uhakika hivi, Ee mfalme, kuna mtu ambaye anaweza kutafsiri maandishi haya; kwani kuna kitu ambacho anaweza kutazama, na kutafsiri maandishi yote ya kale; na ni kipawa kutoka kwa Mungu. Na hivyo vitu vinaitwa vitafsiri, na hakuna mtu yeyote anayeweza kutazama ndani yake bila kuamriwa, la sivyo ataona yale asiyostahili na aangamie. Na yeyote anayeamrishwa kutazama ndani yake, huyo anaitwa mwonaji.
14 Na tazama, mfalme wa watu walio katika nchi ya Zarahemla ndiye yule mtu ambaye ameamriwa kufanya vitu hivi, na aliye na kipawa hiki cha juu kutoka kwa Mungu.
15 Na mfalme akasema kwamba mwonaji ni mkuu zaidi ya nabii.
16 Na Amoni akasema kwamba mwonaji ni mfunuzi na nabii pia; na hakuna kipawa kingine kikuu ambacho mwanadamu anaweza kupata, ila kuwa na uwezo wa Mungu, na hakuna yeyote anayeweza; walakini mwanadamu anaweza kupokea uwezo mkuu kutoka kwa Mungu.
17 Lakini mwonaji anaweza kujua vitu vilivyopita, na pia vitu vitakavyokuja, na kupitia kwao vitu vyote vitafunuliwa, kwa usahihi zaidi, vitu vya siri vitadhihirishwa, na vitu vilivyofichwa kuletwa katika nuru, na vitu visivyojulikana vitajulishwa na kwao, na pia vitu ambavyo havingejulikana vitajulishwa na wao.
18 Kwa hivyo Mungu ametoa njia ili mwanadamu, kwa imani, aweze kutenda miujiza mikuu; kwa hivyo anafaidi zaidi binadamu wenzake.
19 Na sasa, wakati Amoni alipomaliza kuzungumza maneno haya mfalme alifurahia sana, na akamshukuru Mungu, akisema: Bila shaka kuna siri kuu iliyo katika mabamba haya, na vitafsiri hivi bila shaka vilitayarishwa kwa madhumani ya kufunua siri zote za aina hii kwa watoto wa watu.
20 Jinsi gani kazi za Bwana zilivyo za kushangaza, na ni kwa muda gani mrefu ambao anawasubiri watu wake; ndiyo, na jinsi gani watoto wa watu walivyopofuka na hawawezi kupenyeka katika fahamu zao; kwani hawatatafuta hekima, wala hawataki kwamba yeye awatawale wao.
21 Ndiyo, wako kama mifugo wenye kichaa wanaomtoroka mchungaji, na kutawanyika, na kupotea, na kuliwa na wanyama wa mwituni.