Maandiko Matakatifu
Mosia 22


Mlango wa 22

Mipango inatayarishwa ili watu watoroke kutoka utumwa wa Walamani—Walamani wanaleweshwa—Watu wanatoroka, na kurejea Zarahemla, na kutawaliwa na mfalme Mosia. Karibia mwaka 121–120 K.K.

1 Na sasa ikawa kwamba Amoni na mfalme Limhi walishauriana na watu jinsi ya kujikomboa kutoka utumwani; na hata walisababisha kwamba watu wote wakusanyike pamoja; na walifanya hivi ili wapate sauti ya watu kuhusu jambo hili.

2 Na ikawa kwamba hawakupata njia yoyote ya kujitoa utumwani, ila tu wawachukue wake zao na watoto wao, na mifugo yao, na wanyama wao, na hema zao, na kwenda nyikani; kwani Walamani wakiwa wengi mno, ilikuwa haiwezekani kwa watu wa Limhi kupigana nao, wakifikiria kujikomboa kutoka utumwani kwa upanga.

3 Na sasa ikawa kwamba Gideoni alienda na kusimama mbele ya mfalme, na kumwambia: Sasa Ee mfalme, wewe umekuwa ukisikiliza maneno yangu mara nyingi wakati tulipokuwa tunabishana na ndugu zetu, Walamani.

4 Na sasa Ee mfalme, kama wewe hujaniona kuwa mimi ni mtumishi asiyeleta faida, au kama wewe umesikiliza maneno yangu kwa kiasi chochote, na yamekuwa yenye huduma kwako, hata hivyo natamani kwamba usikilize maneno yangu wakati huu, na nitakuwa mtumishi wako na kuwakomboa watu hawa kutoka utumwani.

5 Na mfalme akamruhusu kwamba azungumze. Na Gideoni akamwambia:

6 Tazama ule mlango wa nyuma, kupitia ukuta wa nyuma ulio upande wa nyuma wa mji. Walamani, au walinzi wa Walamani, huwa wamelewa usiku; kwa hivyo hebu tutume tangazo miongoni mwa watu hawa kwamba wakusanye pamoja mifugo yao na wanyama wao, ili wawapeleke kwa usiku huko nyikani.

7 Na nitaenda kulingana na amri yako ili nilipe ushuru wa mwisho wa mvinyo kwa Walamani, na watalewa; na tutapitia mlango wa siri ulio kushoto mwa kambi yao watakapokuwa wamelewa na kulala.

8 Na hivyo tutaondoka na wake zetu na watoto wetu, mifugo yetu, na wanyama wetu na kwenda nyikani; na tutasafiri kando ya nchi ya Shilomu.

9 Na ikawa kwamba mfalme alisikiliza maneno ya Gideoni.

10 Na mfalme Limhi alisababisha kwamba watu wake wakusanye mifugo yao pamoja; na akatuma ushuru wa mvinyo kwa Walamani; na pia alituma mvinyo zaidi, kama zawadi kwao; na walikunywa kwa wingi ule mvinyo uliotumwa kwao na mfalme Limhi.

11 Na ikawa kwamba watu wa mfalme Limhi waliondoka usiku na kwenda nyikani pamoja na mifugo yao na wanyama wao, na walizunguka nchi ya Shilomu nyikani, na wakapinda njia yao na kuelekea nchi ya Zarahemla, wakiongozwa na Amoni na ndugu zake.

12 Na walikuwa wamechukua dhahabu yao yote, na fedha, na vitu vyao vya thamani, vile ambavyo waliweza kubeba, na pia maakuli yao, na kwenda nyikani; na wakaendelea na safari yao.

13 Na baada ya kuwa nyikani kwa siku nyingi walifika katika nchi ya Zarahemla, na kuungana na watu wa Mosia, na kuwa watu wake.

14 Na ikawa kwamba Mosia aliwapokea kwa shangwe; na pia alipokea amaandishi yao, na pia bmaandishi ambayo yalipatwa na watu wa Limhi.

15 Na sasa ikawa kwamba wakati Walamani walipogundua kwamba watu wa Limhi walikuwa wameondoka nchini usiku, walituma jeshi huko nyikani kuwafuata;

16 Na baada ya kuwafuata kwa siku mbili, hawangefuata nyayo zao tena; kwa hivyo walipotea huko nyikani.