2015
Familia na sala
Septemba 2015


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Septemba 2015

Familia na Sala

Wakati mmoja nilipokuwa nimeketi karibu na kitanda cha baba yangu, alizungumza kuhusu utoto wake. Alizungumzia kuhusu upendo wa wazazi wake katika wakati mgumu na kuhusu upendo wake kwa Baba wa Mbinguni na Mwokozi. Nilijua angefariki kutokana na ugonjwa wa saratani, kwa hivyo haikunishangaza kwamba alichanganya upendo wake na upendo na wema wa baba yake wa hapa duniani. Baba yangu mara kwa mara alisema alifikiri aliweza kuona akilini mwake tabasamu la Baba wa Mbinguni.

Wazazi wake walikuwa wamemfundisha kwa mfano kusali kama kwamba alikuwa akizungumza na Mungu na kwamba Mungu angemjibu kwa upendo. Wakati maumivu yalipozidi, tulimkuta asubuhi kando ya kitanda chake akiwa amepiga magoti. Alikuwa amedhoofika na kutoweza kurejea kitandani. Alituambia alikuwa ameomba kumwuliza Baba wa Mbinguni kwa nini ilibidi ateseke sana na alikuwa amejaribu kuwa mwema. Alisema jibu lilikuja kwa upole: “Mungu anahitaji wana walio wajasiri.”

Na kwa jinsi hiyo akaendelea hadi mwisho, akiamini kwamba Mungu alimsikiliza na angemuinua juu. Alibarikiwa kupata kujua mapema na kamwe kutosahau kwamba Mungu ampendaye yu karibu kwa njia ya sala.

Ndiyo maana Bwana akawafundisha wazazi, “Na pia wawafundishe watoto wao kusali, na kusimama wima mbele za Bwana” (M&M 68:28).

Injili ya Yesu Kristo imerejeshwa —pamoja na Kitabu cha Mormoni na funguo zote za ukuhani zinazounganisha familia— kwa sababu Joseph Smith akiwa mvulana alisali kwa Imani. Alipata Imani ile katika familia yenye upendo na uaminifu.

Miaka ishirini iliyopita Bwana alizipa familia ushauri huu kwenye “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” kutoka Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili: “Ndoa na familia yenye mafanikio hujengwa na kudumishwa juu ya kanuni za imani, sala, toba, msamaha, heshima, upendo,huruma, kufanya kazi, na michezo ya burudani yenye kuleta afya.”1

Tuna deni kuu la shukrani kwa familia ya Joseph Smith kwa malezi yake. Familia yake ilikuwa mfano si tu kwa imani bali pia toba, msamaha, heshima, wema, kazi na michezo ya burudani yenye kuleta afya.

Familia itakayokuja baada yako wanaweza kukuita mbarikiwa kwa sababu ya mfano wako wa sala katika familia yako. Inawezakana usimlee mtumishi mkuu wa Mungu lakini unaweza, kwa sala na mfano wako wa uaminifu kumsaidia Bwana Yesu Kristo kuwalea wafuasi wema wapendwa.

Kati ya yote unayoweza kuchagua kufanya ili kumsaidia Bwana, sala itakuwa kiini chake. Kuna yamkini watu wa kawaida ambao wanaposali wanawavuvia wengine kufungua macho yao na kuona nani aliye pale. Unaweza kuwa mtu wa aina hiyo.

Fikiria kile kinachoweza kumaanisha kwa wale wanaopiga magoti pamoja nawe kwenye sala ya familia. Wanapohisi kwamba unapomzungumzia Mungu wewe huzungumza kwa imani, imani yao itaongezeka ili wao pia wazungumze na Mungu. Unaposali kumshukuru Mungu kwa baraka ambazo wao wanajua zimeshafika , imani yao itakuwa kwamba Mungu anawapenda na kwamba hujibu sala zako na hivyo atajibu zao. Hiyo inaweza kufanyika tu katika sala ya familia unapokuwa wewe una uzoefu huu kutoka katika sala yako binafsi, mara kwa mara.

Bado ninabarikiwa na baba na mama waliozungumza na Mungu. Mfano wao wa nguvu ya sala kwenye familia bado inabariki vizazi vilivyo kuja baada yao.

Watoto wangu na wajukuu wanabarikiwa kila siku kwa mfano wa wazazi wangu. Imani kwamba yule Mungu atupendaye husikia na kujibu maombi imepitishwa hadi kwao. Unaweza kuunda urithi kama huu kwenye familia yako. Ninaomba kwamba utafanya hivyo.

Muhtasari

  1. Familia: Tangazo kwa Ulimwengu, Liahona, Nov. 2010, 129.

Sherehekea miaka 20 ya Tangazo kuhusu Familia

“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” hufundisha kanuni ambazo zinatumika hivi leo kama zilivyotumika wakati lilipotolewa mara ya kwanza mnamo Septemba 23, 1995. Fikiria kuwaalika watu binafsi au familia unaowafundisha kusherehekea miaka 20 ya Tangazo kwa:

  1. Kuorodhesha kanuni zilizomo zenye umuhimu maalum kwao (Ona jinsi Rais Eyring alivyofanya hivi kwenye ujumbe hapo juu.)

  2. Kujadili jinsi kila kanuni zinavyoweza kuwabariki hivi leo na katika siku zijazo.

  3. Kuweka malengo maalum yatakayojumuisha kanuni hizo katika maisha yao na kushiriki na wengine.