2010–2019
Baada ya Majaribu ya Imani Yetu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Baada ya Majaribu ya Imani Yetu

Tunapofuata sauti ya Mungu na njia Yake ya agano, Yeye atatuimarisha katika majaribu yetu.

Wakati nilipokuwa mtoto, Frank Talley, muumini wa Kanisa, alijitolea kuisadia familia yangu kusafiri kwa ndege kutoka Puerto Rico hadi Jijini Salt Lake ili tuweze kuunganishwa hekaluni, lakini punde vikwazo vilianza kutokea. Mmoja kati ya dada zangu, Marivid, aliugua. Wakiwa na wasiwasi, wazazi wangu walisali kuhusu nini cha kufanya na bado walihisi msukumo wa kusafiri. Waliamini kwamba kadiri walivyokuwa wakifuata msukumo wa Bwana kwa uaminifu, familia yetu ingelindwa na kubarikiwa—na ilikuwa hivyo.

Haijalishi vizuizi tunavyokabiliana navyo katika maisha, tunaweza kuamini kwamba Yesu Kristo ataandaa njia mbele yetu wakati tunapotembea kwa imani. Mungu ameahidi ya kwamba wote wanaoishi kulingana na maagano ambayo wamefanya Naye, katika wakati Wake, watapokea baraka Zake zote zilizoahidiwa. Mzee Jeffrey R. Holland alifundisha, “Baraka zingine huja haraka, zingine huchelewa, na zingine haziji hadi tukifika mbinguni; lakini kwa wale wanaoikubali injili ya Yesu Kristo, zinakuja.”1

Moroni alifundisha kwamba “imani ni vitu ambavyo vinatumainiwa na havionekani; kwa hivyo, msishindane kwa sababu hamwoni, kwani hamtapata ushahidi wowote mpaka baada ya majaribu ya imani yenu.”2

Swali letu ni, Tunapaswa kufanya nini ili kukabiliana vyema na majaribu yanayotukabili?

Katika hotuba yake ya kwanza kama Rais wa Kanisa, Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Kama Urais mpya, tunataka kuanza na mwisho akilini. Kwa sababu hii, tunazungumza nanyi leo kutoka hekaluni. Mwisho ambao kila mmoja wetu hujitahidi kuufikia ni kupata endaumenti ya nguvu katika Nyumba ya Bwana, kuunganishwa kama familia, uaminifu katika maagano yaliyofanywa katika hekalu ambayo hutufanya tustahili baraka kubwa zaidi ya Mungu—ile ya uzima wa milele. Ibada za hekaluni na maagano unayofanya huko ni muhimu katika kuimarisha maisha yako, ndoa yako na familia yako, na uwezo wako wa kupinga mashambulizi ya adui. Kuabudu kwako hekaluni na huduma yako huko kwa niaba ya mababu zako itakubariki na ongezeko la ufunuo binafsi na amani na itaimarisha kujitolea kwako kubaki katika njia ya agano.”3

Tunapofuata sauti ya Mungu na njia Yake ya agano, Yeye atatuimarisha katika majaribu yetu.

Safari ya familia yangu hekaluni miaka iliyopita ilikuwa ngumu, lakini tulipokaribia Hekalu katika Jiji la Salt Lake, Utah, mama yangu, akiwa amejawa na furaha na imani, alisema, “Tutakuwa SAWA; Bwana atatulinda.” Tuliunganishwa kama familia, na dada yangu akapata nafuu. Hili lilifanyika tu baada ya majaribu ya imani ya wazazi wangu na katika kufuata misukumo ya Bwana.

Mfano huu wa wazazi wangu bado unashawishi maisha yetu leo. Mfano wao ulitufundisha kwa nini ya mafundisho ya injili na kutusaidia kuelewa maana, lengo, na baraka ambazo injili huleta. Kuelewa kwa nini ya injili ya Yesu Kristo kunaweza pia kutusaidia kukabiliana na majaribu yetu kwa imani.

Hatimaye, kila kitu ambacho Mungu anatualika na kutuamuru sisi tufanye ni kielelezo cha upendo Wake kwetu na hamu Yake ya kutupatia baraka zote zilizowekwa kwa ajili ya waaminifu. Hatuwezi kudhania kwamba watoto wetu watajifunza kuipenda injili wao wenyewe; ni jukumu letu kuwafundisha. Tunapowasaidia watoto wetu kujifunza jinsi ya kutumia uhuru wao wa kujiamulia kwa busara, mfano wetu unaweza kuwavuvia wao kufanya chaguzi zao wenyewe za haki. Maisha yao ya uaminifu hatimaye yatawasaidia watoto wao kujua ukweli wa injili kwa ajili yao wenyewe.

Wavulana na wasichana, msikieni nabii leo akizungumza nanyi. Tafuteni kujifunza kweli za kiungu na tafuteni kuelewa injili ninyi wenyewe. Rais Nelson hivi karibuni alishauri: “Ni hekima gani unayopungukiwa nayo? … Fuata mfano wa Nabii Joseph. Tafuta mahali tulivu. … Jinyenyekeze mbele za Mungu. Mimina moyo wako kwa Baba yako wa Mbinguni. Mgeukie Yeye kwa ajili ya majibu.”4 Unapotafuta mwongozo kutoka kwa Baba yako mpendwa wa Mbinguni, kusikiliza ushauri wa manabii wanaoishi na kutazama mifano ya wazazi waadilifu, wewe pia unaweza kuwa kiungo imara cha imani katika familia yako.

Kwa wazazi walio na watoto ambao wameondoka katika njia ya agano, kwa upole rudini nyuma. Wasaidieni kuelewa kweli za injili. Anza sasa; kamwe haujachelewa.

Mfano wetu ya kuishi kwa uadilifu unaweza kuleta tofauti kubwa. Rais Nelson amesema: “Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tumezoea kufikiria ‘kanisa’ kama kitu ambacho hutokea katika majumba yetu ya mikutano, kikisaidiwa na kile kinachotendeka nyumbani. Tunahitaji marekebisho kwenye mpangilio huu. Sasa ni wakati wa Kanisa linalolenga nyumbani, likisaidiwa na kile kinachotendeka ndani ya majengo ya matawi yetu, kata na vigingi.”5

Maandiko yanafundisha, “Mlee mtoto katika njia impasayo: Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”6

Pia yanasema, “Na sasa, kwa vile kuhubiri kwa neno kulikuwa na maelekezo makubwa ya kuongoza watu kufanya yale ambayo ni haki—ndio, ilikuwa na matokeo ya nguvu zaidi kwa akili za watu kuliko upanga, au kitu chochote kingine, ambacho kiliwahi kufanyika kwao—kwa hivyo Alma alifikiri ilikuwa bora kwamba wangejaribu matokeo ya uwezo wa neno la Mungu.”7

Hadithi inasimuliwa kuhusu mwanamke ambaye alikuwa amekasirika kwamba mwanaye alikuwa akila pipi nyingi sana. Haikujalisha ni kiasi gani alimkaripia, aliendelea kutosheleza tamaa yake ya sukari. Akiwa amevunjika moyo kabisa, aliamua kumpeleka mwanaye kuonana na mtu mwenye busara ambaye alimheshimu.

Alimkaribia na kusema, “Bwana, mwanangu anakula pipi nyingi kupitiliza. Tafadhali, ungeweza kumwambia kuacha kula pipi nyingi?”

Alimsikiliza kwa makini, kisha akamwambia mwanaye “Nenda nyumbani na urudi baada ya wiki mbili.”

Alimchukua mwanaye na kwenda nyumbani, akitatizika kwa nini mwanaume hakumwambia mvulana kuacha kula pipi nyingi.

Wiki mbili baadaye walirudi. Mwanaume mwenye busara alimtazama mvulana moja kwa moja na kusema, “Mvulana, unapaswa kuacha kula pipi nyingi. Si nzuri kwa afya yako.”

Mvulana alikubali kwa kichwa na kuahidi kwamba hangeendelea.

Mama wa mvulana aliuliza “Kwa nini hukumwambia hivyo wiki mbili zilizopita?”

Mwanaume mwenye busara alitabasamu. “Wiki mbili zilizopita nilikuwa ningali nala pipi nyingi mimi mwenyewe.”

Mwanaume huyu aliishi kwa uadilifu kiasi kwamba alijua ushauri wake ungekuwa na nguvu zaidi ikiwa tu yeye mwenyewe alikuwa anaishi kulingana na ushauri wake.

Ushawishi ambao tunao juu ya watoto wetu ni wa nguvu zaidi wanapotuona tukitembea kwa uaminifu katika njia ya agano. Nabii wa Kitabu cha Mormoni Yakobo ni mfano wa uadilifu sawa na huo. Mwanaye Enoshi aliandika kuhusu athari ya mafundisho ya baba yake:

“Mimi, Enoshi, nikijua kwamba Baba yangu alikuwa mtu wa haki—kwani alinifunza kwa lugha yake, na pia katika malezi na maonyo ya Bwana—na jina la Mungu wangu libarikiwe kwa hayo. …

“… Na maneno ambayo nilikuwa nimezoea kumsikia baba yangu akizungumza kuhusu uzima wa milele, na shangwe ya watakatifu, yakapenya ndani ya moyo wangu.”8

Akina mama wa vijana askari mashujaa waliishi injili, na watoto wao walijazwa na ari. Kiongozi wao aliripoti:

“Walikuwa wamefundishwa na mama zao, kwamba kama wasingekuwa na shaka, Mungu angewaokoa.

“Na walirudia kwangu maneno ya mama zao, wakisema: Hatuna shaka kuwa mama zetu walijua.”9

Enoshi na vijana askari mashujaa waliimarishwa na imani ya wazazi wao, ambayo iliwasaidia wao kukabiliana na majaribu yao wenyewe ya imani.

Tumebarikiwa na injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo katika siku zetu, ambayo inatuinua wakati tunahisi kukata tamaa na kutatizika. Tunahakikishiwa kwamba juhudi zetu zitazaa matunda katika wakati wa Bwana kama tutasonga mbele kupitia majaribu ya imani yetu.

Mimi na mke wangu, pamoja na Urais wa Eneo hivi karibuni tulijiunga na Mzee David A. Bednar katika kuwekwa wakfu Hekalu la Haiti Port-au-Prince. Mwana wetu Jorge, aliyeambatana nasi, alisema kuhusu uzoefu wake: “Ajabu, Baba! Punde tu Mzee Bednar alipoanza kwa sala ya kuweka wakfu, niliweza kuhisi chumba kikijazwa na joto na nuru. Sala iliongeza mengi zaidi kwenye uelewa wangu kuhusu lengo la hekalu. Kwa kweli ni nyumba ya Bwana.”

Katika Kitabu cha Mormoni, Nefi anafundisha kwamba tunapotamani kujua mapenzi ya Mungu, Yeye atatuimarisha. Aliandika, “Mimi, Nefi, nikiwa mdogo … na pia nikiwa na hamu ya kujua siri za Mungu, kwa hivyo, nikamlilia Bwana; na tazama akanijia mimi, na akanigusa moyo wangu kwamba nikaamini maneno yote ambayo baba yangu alikuwa amezungumza; kwa hivyo, mimi sikumwasi kama kaka zangu.”10

Akina kaka na akina dada, acha tuwasaidie watoto wetu na wote waliotuzunguka kufuata njia ya agano ya Mungu ili Roho wa Bwana aweze kuwafundisha na kulainisha mioyo yao ili watamani kumfuata Yeye katika maisha yao yote.

Ninapofikiria mfano wa wazazi wangu, ninatambua kwamba imani yetu katika Bwana Yesu Kristo itatuonesha njia ya kurudi nyumbani kwetu mbinguni. Ninajua muujiza huja baada ya majaribu ya imani yetu.

Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho. Ninajua Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Yeye na Baba yetu wa Mbinguni walikuja asubuhi ile ya majira ya kuchipua ya 1820 kwa kijana Joseph Smith, nabii wa Urejesho. Rais Russell M. Nelson ni nabii wa siku yetu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.