2010–2019
Njoo, Unifuate—Mkakati wa Kukinza na Mpango Hai wa Bwana
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Njoo, Unifuate—Mkakati wa Kukinza na Mpango Hai wa Bwana

Bwana anawatayarisha watu Wake dhidi ya mashambulizi ya adui. Njoo, Unifuate ni mkakati wa kukinza na mpango hai wa Bwana.

Tunafurahia katika kukutana pamoja katika mkutano huu mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ni baraka kupokea nia na mapenzi ya Bwana kupitia mafundisho ya manabii na mitume Wake. Rais Russell M. Nelson ni nabii aliye hai wa Bwana. Tuna shukrani iliyoje kwa ushauri na mwongozo wake wenye uvuvio uliopokelewa leo.

Ninaongeza ushahidi wangu kwenye ule uliotolewa hapo awali. Ninatoa ushuhuda juu ya Mungu, Baba yetu wa Milele. Anaishi na anatupenda na kutulinda. Mpango wake wa furaha unatoa baraka ya maisha haya ya duniani na hatimaye kurudi kwetu katika uwepo Wake.

Ninashuhudia pia juu ya Yesu Kristo. Ni Mwana Pekee wa Mungu. Alituokoa kutokana na mauti, na Anatukomboa kutokana na dhambi tunapoonesha imani Kwake na kutubu. Dhabihu Yake ya upatanisho isiyo na mwisho kwa niaba yetu inaleta baraka za kutokufa na uzima wa milele. Hakika, “Mungu na ashukuriwe kwa zawadi Yake kuu ya mwanawe mtakatiifu” (“Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume,Liahona, Mei 2017, upande wa ndani wa jalada la mbele).

Watakatifu wa Siku za Mwisho kote ulimwenguni wamebarikiwa kumwabudu Yesu Kristo katika mahekalu Yake. Mojawapo ya mahekalu hayo kwa sasa linajengwa kule Winnipeg, Kanada. Mimi na mke wangu, Anne Marie, tulipata nafasi ya kutembelea eneo la ujenzi Agosti ya mwaka huu. Hekalu limesanifiwa vizuri na bila shaka litakuwa la kupendeza wakati litakapomalizika. Hata hivyo, huwezi kuwa na hekalu la kupendeza kule Winnipeg, au mahali pengine popote, bila msingi imara na thabiti.

Mfumo wa kuganda-kuyeyuka na hali ya udongo kutanua kule Winnipeg vilisababisha iwe vigumu kutayarisha msingi wa hekalu. Hivyo basi, iliamuliwa kwamba msingi wa hekalu hili ungekuwa na mihimili 70 ya vyuma iliyofungwa katika saruji. Mihimili hii ina urefu wa futi 60 (m 18) na upana wa inchi 12 hadi 20 (sm 30 hadi 50) . Ilipigiliwa ardhini hadi ilipogonga mwamba, takriban futi 50 (m 15)chini ya ardhi. Kwa njia hii, mihimili hii 70 inatoa msingi imara, thabiti kwa ajili ya kile kitakachokuwa hekalu zuri la Winnipeg.

Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunatafuta msingi imara na wa uhakika sawa na huo katika maisha yetu—msingi wa kiroho unaohitajika kwa ajili ya safari yetu katika maisha ya duniani na kurudi nyumbani kwetu mbinguni. Msingi huo umejengwa juu ya mwamba wa uongofu wetu kwa Bwana Yesu Kristo.

Tunarejea mafundisho ya Helamani kutoka katika Kitabu cha Mormoni: “Na sasa, wana wangu, kumbukeni, kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenge msingi wenu; kwamba ibilisi atakapotuma mbele pepo zake kali, ndiyo, mishale yake kimbungani, … hautakuwa na uwezo juu yenu kuwavuta chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambako kwake mmejengwa, ambao ni msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka” (Helaman 5:12).

Kwa shukrani, tunaishi katika kipindi ambacho manabii na mitume wanatufundisha kuhusu Mwokozi Yesu Kristo. Kufuata ushauri wao kunatusaidia kujenga msingi imara katika Kristo.

Mwaka mmoja uliopita, katika hotuba yake ya ufunguzi ya mkutano mkuu wa Oktoba 2018, Rais Russell M. Nelson alitoa tangazo na onyo hili: “Kusudi la muda mrefu la Kanisa ni kuwasaidia waumini wote kuongeza imani yao katika Bwana wetu Yesu Kristo na Upatanisho Wake, kuwasaidia wao katika kufanya na kushika maagano yao na Mungu, na kuimarisha na kuunganisha familia zao. Katika hii dunia changamani leo, hili si rahisi. Adui anaongeza mashambulizi yake kwenye imani na juu yetu na familia zetu kwa kiwango kikubwa sana. Kunusurika kiroho, tunahitaji mikakati ya kukinza na mipango hai” (“Hotuba ya Ufunguzi,” Liahona, Nov. 2018, 7; msisitizo umeongezwa).

Kufuatia ujumbe wa Rais Nelson, Mzee Quentin L. Cook wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitambulisha Njoo, Unifuate nyenzo kwa ajili ya watu binafsi na familia. Hotuba yake ilijumuisha kauli zifuatazo:

Kuanzia Januari mwaka huu, Watakatifu wa Siku za Mwisho kote ulimwenguni walianza kujifunza Agano Jipya, pamoja na nyenzo za Njoo, Unifuate kama mwongozo wetu. Pamoja na ratiba ya kila wiki, Njoo, Unifuate inatusaidia kujifunza maandiko, mafundisho ya injili, na mafundisho ya manabii na mitume. Ni nyenzo ya ajabu kwetu sote.

Baada ya juhudi hii ya miezi tisa ya kusoma maandiko, tunaona nini? Tunawaona Watakatifu wa Siku za Mwisho kila mahali wakikua katika imani na kujitolea kwa Bwana Yesu Kristo. Tunaona watu binafsi na familia wakitenga muda katika wiki kwa ajili ya kujifunza maneno ya Mwokozi. Tunaona kuboreka kwa mafunzo ya injili katika madarasa yetu ya Jumapili tunapojifunza maandiko nyumbani na kushiriki umaizi wetu kanisani. Tunaona furaha na umoja mkubwa wa familia wakati tuliposonga kutoka kusoma tu maandiko hadi kujifunza maandiko kwa kina.

Imekuwa fursa kwangu kuwatembelea wengi wa Watakatifu wa Siku za Mwisho na kusikiliza kuhusu uzoefu wao wa moja kwa moja wa Njoo, Unifuate. Dhihirisho la imani yao linajaza moyo wangu kwa furaha. Hapa ni baadhi tu ya maoni ambayo nimesikia kutoka kwa waumini tofauti wa Kanisa katika sehemu tofauti za ulimwengu:

  • Baba alishiriki: “Ninafurahia Njoo, Unifuate kwa maana inatoa fursa ya kuwashuhudia watoto wangu juu ya Mwokozi.”

  • Katika nyumba nyingine, mtoto alisema: “Hii ni nafasi ya kuwasikia wazazi wangu wakishiriki shuhuda zao.”

  • Mama alishiriki: “Tumepewa mwongozo wa kiungu kuhusu jinsi ya kumuweka Mungu kwanza. Muda ambao [tulifikiri] ‘hatukuwa nao’ umeweza [kujazwa] na tumaini, furaha, amani, na mafanikio katika njia ambazo hatukudhani ingewezekana.”

  • Wanandoa walisema: “Tunasoma maandiko kwa njia tofauti kabisa na vile tulivyoyasoma hapo awali. Tunajifunza zaidi kuliko vile tulivyojifunza hapo awali. Bwana anatutaka tuone vitu kwa mtazamo mpya. Bwana anatutayarisha.”

  • Mama alisema: “Ninapenda kwamba tunajifunza pamoja vitu vinavyofanana. Kabla, tulikuwa tunasoma. Leo, tunajifunza.”

  • Dada fulani alishiriki mtazamo huu wa kimaizi: “Kabla, ulikuwa na somo na maandiko yaliongezea. Sasa, unayo maandiko na somo linaongezea.”

  • Dada mwingine alisema: “ninahisi tofauti ninapoifanya [ikilinganishwa na] wakati ambapo sifanyi. Ninakuta ni rahisi kuzungumza na wengine kuhusu Yesu Kristo na imani yetu.”

  • Bibi alisema: “Huwa nawapigia simu watoto na wajukuu zangu kila Jumapili, na tunashiriki umaizi kutoka Njoo, Unifuate Pamoja.”

  • Dada alisema: “Njoo, Unifuate inaonekana kana kwamba Mwokozi mwenyewe ananihudumia mimi. Ni uvuvio kutoka mbinguni.”

  • Baba alisema: “Tunapotumia Njoo, Unifuate, sisi ni kama wana wa Israeli, tukiweka alama kwenye miimo ya milango yetu, kulinda familia zetu dhidi ya ushawishi wa mwangamizi.”

Akina kaka na akina dada, ni furaha kuzungumza nanyi na kusikia jinsi juhudi zenu kwenye Njoo, Unifuate zinavyobariki maisha yenu. Asanteni kwa moyo wenu wa kujitolea.

Kujifunza maandiko kwa kutumia Njoo, Unifuate kama mwongozo ni kuimarisha uongofu wetu kwa Yesu Kristo na injili Yake. Si tu kwamba tunabadilisha na kuondoa saa moja kanisani jumapili kwa ajili ya saa moja zaidi ya kujifunza maandiko nyumbani. Kujifunza injili ni juhudi endelevu kwa wiki nzima. Kama dada mmoja alivyoshiriki kiumaizi, “Lengo si kufupisha kanisa kwa saa moja; ni kurefusha kanisa kwa siku sita!”

Sasa, fikiria tena onyo la nabii wetu, Rais Nelson, alilotoa wakati alipofungua mkutano mkuu wa Oktoba 2018:

“Adui anaongeza mashambulizi yake kwenye imani na juu yetu na familia zetu kwa kiwango kikubwa sana. Ili kunusurika kiroho, tunahitaji mikakati ya kukinza na mipango hai” (Hotuba ya Ufunguzi,” 7).

Kisha (takriban masaa 29 baadaye) Jumapili alasiri, alifunga mkutano kwa ahadi hii: “Utakapofanya bidii kupanga upya nyumba yako kuwa kitovu cha kujifunza injili, … ushawishi wa adui katika maisha yako na nyumbani kwako utapungua” (“Kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho wa Mfano,” Liahona, Nov. 2018, 113).

Ni kwa jinsi gani mashambulizi ya adui yanaweza kuwa yanaongezeka kwa kiasi kikubwa huku wakati huo huo pia ushawishi wa adui hakika unapungua? Inaweza kufanyika, na inafanyika kote katika Kanisa, kwa sababu Bwana anawatayarisha watu Wake dhidi ya mashambulizi ya adui. Njoo, Unifuate ni mkakati wa kukinza na mpango hai wa Bwana. Kama Rais Nelson alivyofundisha, “Mtaala mpya unaolenga nyumbani, unaosaidiwa na Kanisa na uliofanywa sawa una uwezo wa kufungulia nguvu za familia.” Hata hivyo, inahitaji na itahitaji juhudi zetu zote; tunahitaji “[kufuatilia] kwa makini na kwa uangalifu ili kubadilisha nyumba [zetu] kuwa kimbilio la imani” (“Kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho wa Mfano,” 113).

Hata hivyo, kama Rais Nelson pia alivyosema, “Kila mmoja wetu ana jukumu kwa ukuaji wetu binafsi wa kiroho.” (“Hotuba ya Ufunguzi,” 8).

Kwa nyenzo ya Njoo, Unifuate, Bwana anatutayarisha “kwa nyakati hatari ambazo sasa zinatukabili” (Quentin L. Cook, “Uongofu wa Kina na wa Kudumu,” 10). Yeye anatusaidia kujenga ule “msingi imara, msingi ambao watu wote wakijenga hawataanguka” (Helamani 5:12)—msingi wa ushuhuda uliosimikwa imara katika mwamba wa uongofu wetu kwa Bwana Yesu Kristo.

Acha juhudi zetu za kila siku katika kujifunza maandiko zituimarishe na kututhibitisha wastahiki wa baraka hizi zilizoahidiwa. Ninaomba hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.