2010–2019
Ninavijua Mwenyewe
Oktoba 2014


Ninavijua Mwenyewe

Tumekuja kujijulia wenyewe kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu na kwamba Joseph Smith ni nabii wa Urejesho.

Ndugu zangu wapendwa, tunaendelea kupata maongozi kwa mfano wa kibinafsi na huduma ya ukuhani ya Rais Thomas S. Monson. Majuzi, Mashemasi kadhaa waliulizwa, “Ni nini mnachopendezwa nacho sana kumhusu Rais Monson? Shemasi mmoja alikumbuka jinsi Rais Monson, kama mtoto alipeana wanaserere wake kwa watoto ambao walikuwa na mahitaji. Mwingine alitaja jinsi Rais Monson alivyowatunza wajane wengi katika kata yake. Wa tatu alisema kwamba yeye aliitwa kama Mtume katika umri mdogo sana na amewabariki watu ulimwenguni kote. Kisha kijana mmoja akasema, “Kitu ninachopendezwa nacho sana kumhusu Rais Monson ni ushuhuda wake wa nguvu.”

Kwa kweli, sisi sote tumeshahisi ushahidi maalum wa Mwokozi Yesu Kristo wa nabii wetu na sharti lake la daima kufuata mnong’ono wa Roho. Kwa kila uzoefu ambao yeye hushiriki, Rais Monson hutualika kuishi injili kikamilifu zaidi na kutafuta na kuimarisha shuhuda zetu wenyewe binafsi. Kumbuka kile alichosema kutoka kwenye jukwaa hili katika mikutano michache iliyopita: Ili sisi tuwe imara na kushinda nguvu zote zinazotuvuruta kwenye mwenendo usiyo sahihi  … , ni sharti tuwe na ushuhuda wetu wenyewe. Hata ikiwa una umri wa miaka 12 au 112---au popote katikati---unaweza kujijulia mwenyewe kwamba injili ya Yesu Kristo ni kweli.”1

Ingawa ujumbe wangu jioni ya leo unaelekezwa zaidi kwa wale wanaokaribia umri wa miaka 12 kuliko wa wale wenye miaka 112, kanuni ninazoshiriki zinatumika kwa kila mmoja. Katika mjibizo kwa taarifa ya Rais Monson, ningependa kuuliza, je, kila mmoja wetu anajijulia mwenyewe kwamba injili ni kweli? Je, tunaweza kusema kwa imani kwamba shuhuda zetu kwa kweli ni zetu? Kumnukuu Rais Monson tena: “Mimi naendelea kudai kwamba ushuhuda wa nguvu wa Mwokozi wetu na wa injili Yake vitawalinda kutoka kwa dhambi na uovu unaowazunguka. … Kama tayari hamna ushuhuda wa vitu hivi, fanyeni kile kinachohitajika ili kuupata. Ni muhimu kwenu kuwa na ushuhuda wenu wenyewe, kwani ushuhuda wa wengine unaweza kuwabeba kufikia hatua fulani tu.2

Ninavijua Mwenyewe

Kujifunza wenyewe kwamba injili ya urejesho ya Yesu Kristo ni ya kweli kunaweza kuwa mojawapo wa uzoefu mkuu na wa furaha sana katika maisha. Tunaweza kuanza kwa kutegemea shuhuda za wengine---tukisema kama vijana askari walivyosema, “Hatuna shaka kuwa mama zetu walijua.”3 Hii sehemu nzuri ya kuanza, lakini sharti tujenge kuanzia hapo. Kuwa imara katika kuishi injili, hakuna kitu kilicho muhimu sana kuliko kupokea na kuimarisha ushuhuda wetu wenyewe. Sisi sharti tuweze kutangaza, kama Alma alivyofanya, “Ninavijua … Mwenyewe.”4

“Na mnadhaniaje kwamba ninajua ukweli wao?” Alma anaendelea. “Tazama, ninawaambia kwamba yamesababishwa kujulikana kwangu na Roho Mtakatifu wa Mungu. Tazama, nimefunga na kusali siku nyingi ili nivijue vitu hivi mimi mwenyewe. Na sasa ninavijua mwenyewe kuwa ni vya kweli.”5

Natamani Kuona Vitu Ambavyo Baba Yangu Aliona.

Kama vile Alma, Nefi pia alikuja kujua ukweli yeye mwenyewe. Baada ya kumsikiliza baba yake akizungumza kuhusu uzoefu mwingi wake mwenyewe, Nefi alitaka kujua kile baba yake alijua. Hii ilikuwa zaidi kuliko udadisi tu---ilikuwa kitu alikuwa na njaa na kivu nacho. Hata ingawa alikuwa “kijana sana,” na alikuwa na “hamu kubwa ya kujua siri za Mungu,”6 alitamani aone pia, na kusikia, na kuvijua vitu hivi, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.”7

Wakati Nefi “alipokaa akitafakari katika moyo wake,” alibebwa na Roho … hata kwenye mlima mkubwa mrefu sana,” ambapo aliulizwa, “Ni nini unachotamani? Jibu lake lilikuwa rahisi: Natamani kuona vitu ambavyo baba yangu aliona.” 8 Kwa sababu ya moyo wake wa kuamini na juhudi zake za bidii, Nefi alibarikiwa na uzoefu wa ajabu sana. Alipokea ushahidi wa kuzaliwa, maisha, na Kusulubiwa kwa Mwokozi Yesu Kristo kuliokaribia kutokea; aliona kuja kwa Kitabu cha Mormoni na Urejesho wa injili katika siku za mwisho---yote kama matokeo ya hamu yake ya dhati ya kujijulia mwenyewe. 9

Uzoefu huu wa kibinafsi na Bwana ulimtayarisha Nefi kwa dhiki na changamoto angekumbana nazo punde. Ulimwezesha kusimama imara hata wakati wengine katika familia yake walikuwa wanayumba. Aliweza kufanya hivi kwa sababu alikuwa amejifunza mwenyewe na alijijulia mwenyewe. Alikuwa amebarika na ushuhuda wake mwenyewe.

Na Aombe Dua kwa Mungu

Vile vile kama Nefi, Nabii Joseph Smith pia alikuwa “kijana sana” wakati “akili yake ilipoitwa kwa tafakari nzito” kuhusu kweli za kiroho. Kwa Joseph, ilikuwa ni wakati “msukosuko mkubwa,” kuzungukwa na jumbe zenye utata na kukanganya kuhusu dini. Alitaka kujua ni kanisa gani lililokuwa sahihi.10 Akipewa maongozi na maneno haya katika Biblia: “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu.” 11 Naye akatenda mwenyewe ili apate jibu. Asubuhi maridadi katika msimu wa kuchipua wa mwaka wa 1820, alienda kwenye kichaka cha miti na kupiga magoti katika sala. Kwa sababu ya imani yake na kwa sababu Mungu alikuwa na kazi maalum kwake ya kufanya, Joseph alipokea ono tukufu la Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, na alijifunza mwenyewe kile alichopaswa kufanya.

Je! Unaona katika uzoefu wa Joseph mfumo unaoweza kuutumia katika kupata au kuimarisha ushuhuda wako mwenyewe? Joseph aliruhusu maandiko yapenye ndani ya moyo wake. Aliyatafakari kwa kina na kuyatumia kwa hali yake mwenyewe. Kisha akatenda juu ya kile alikuwa amejifunza. Matokeo yalikuwa Ono la Kwanza tukufu--- na kila kitu ambacho kinakuja baadaye. Kanisa kihalisi kabisa lilianzishwa juu ya kanuni kwamba kila mtu---ikijumuisha kijana wa shamba wa umri wa miaka 14---anaweza “kuomba dua kwa Mungu” na kupokea jibu la maombi yake.

Kwa Hivyo Ushuhuda ni Nini?

Kila mara tunawasikia washiriki wa Kanisa wakisema kwamba ushuhuda wao wa injili ndio mali yao yenye thamani kuu. Ni kipawa kitakatifu kutoka kwa Mungu ambacho huja kwetu kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Ni uhakika mtulivu, usioyumba tunaopokea tunapojifunza, kusali, na kuishi injili. Ni hisia ya Roho Mtakatifu akitoa ushahidi kwenye nafsi zetu kwamba kile tumejifunza na kufanya ni sahihi.

Baadhi ya watu huongea kuhusu ushuhuda kwa vile ni swichi ya mwanga---unaweza kuwa umewaka au umezima; unaweza kuwa una ushuhuda, au hauna. Kihalisi, ushuhuda ni zaidi kama vile mti ambao unapitia katika hatua nyingi za ukuaji na ustawi. Baadhi ya miti iliyo mirefu ulimwenguni inapatikana katika Redwood National Park katika Marekani magharibi. Unaposimama chini ya miti hii mikubwa sana, inashangaza kufikiria kwamba kila mmoja umekua kutoka kwa mbegu ndogo sana. Kwa hivyo ndivyo ilivyo na shuhuda zetu. Ingawa zinaweza kuanza kwa uzoefu mmoja wa kiroho, zinaweza kukua na kustawi katika muda kupitia kurutubishwa kila mara na kupata matukio ya kiroho kila mara.

Haishangazi, basi, kwamba wakati nabii Alma alipoelezea jinsi tanavyostawisha ushuhuda wetu, alizungumza juu ya mbegu ikikua kuwa mti. “Sasa ikiwa mtatoa nafasi,” alisema. “ili mbegu ipandwe ndani ya moyo wako, tazama, ikiwa itakuwa mbegu ya kweli, au mbegu nzuri, ikiwa hamtaitupa nje kwa kutoamini kwenu, ... itaanza kuvimba ndani ya vifua vyenu; na wakati mtakaposikia huu mwendo wa kuvimba, mtaanza kusema ndani yenu—inawezekana kwamba hii ni mbegu nzuri, au kwamba neno ni zuri, kwani linaanza kuwa ndani ya nafsi yangu; ndio, inaanza kuangaza kuelewa kwangu, ndio, inaanza kunipendeza mimi.”12

Hivi ndivyo jinsi ushuhuda huanza: kwa hisia takatifu, zenye kuelimisha, kuhakikisha ambazo zinaonyesha kwetu kwamba neno la Mungu ni kweli. Hata hivyo, ingawa hisia hizi zinaweza kuwa za ajabu, ni mwanzo tu. Kazi yako ya kukuza ushuhuda wako haijaisha---zaidi kuliko kazi ya kukuza mti wa redwood kuisha wakati miche midogo ya kwanza inapochomoza kutoka mchangani. Kama tutapuuza au kutelekeza hii minong’ono ya mapema ya kiroho, kama hatutaitunza kwa kuendelea kujifunza maandiko na kusali na kutafuta uzoefu zaidi wa Roho, hisia zetu zitafifia na shuhuda zetu zitadidimia.

Kama alivyosema Alma: “Lakini mkiuachilia mti ule, na msifikirie kuulisha, tazama hautapata mzizi wowote; na wakati joto la jua linawadia na kuuchoma, kwa sababu hauna mzizi hukaukia mbali, na mtaukata na kuutupa nje.”13

Katika hali nyingi, shuhuda zetu zitakua kwa njia sawa na vile mti hukua: hatimaye, bila kueleweka, kama matokeo ya utunzaji wetu wa kila mara na juhudi za bidii: “Lakini ikiwa mtalisha neno,” Alma aliahidi, “ndio, lisha mti unapoanza kukua, kwa imani yenu, kwa bidii kuu, na uvumilivu, mkitumainia kupata tunda kwake, utamea mizizi; na tazama utakuwa mti utakaokua na kuzaa matunda yasiyo na mwisho.”14

Sasa Ndiyo Wakati; Leo Ndiyo Siku

Ushuhuda wangu ulianza nilipojifunza na kutafakari mafundisho yanayopatikana kwenye Kitabu cha Mormoni. Nilipopiga magoti na kumwomba Mungu kwa sala ya unyenyekevu, Roho Mtakatifu alishuhudia kwenye nafsi yangu kwamba kile nilichokuwa ninasoma ni kweli. Ushahidi huu wa mapema ukawa kichocheo cha ushuhuda wangu wa kweli zingine nyingi za injili. Kwani kama alivyofunza Rais Monson: Tunapojua kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli, kisha hufuata kwamba Joseph Smith kwa kweli alikuwa nabii na kwamba alimwona Mungu Baba wa Milele na Mwanawe, Yesu Kristo. Pia inafuata kwamba injili ilirejeshwa katika hizi siku za mwisho kupitia kwa Joseph Smith---ikijumuisha urejesho wa Ukuhani wa Haruni na Melkidezeki.”15 Tangu siku hiyo, ninapata kuwa na uzoefu mwingi mtakatifu na Roho Mtakatifu ambaye amethibitisha kwangu kwamba injili ya urejesho ya Yesu Kristo ni kweli. Pamoja na Alma, naweza kusema bila shaka kwamba ninavijua mwenyewe.”

Rafiki zangu vijana, sasa ndiyo wakati na leo ndiyo siku ya kujifunza au kujihakikishia wenyewe kwamba injili ni ya kweli. Kila mmoja wetu ana kazi muhimu ya kufanya. Kutimiza kazi hiyo, ni sharti sisi tuwe na imani ya Alma, Nefi na kijana Joseph Smith ili kupata na kustawisha ushuhuda wetu wenyewe.

Kama shemasi kijana niliyezungumzia mapema, mimi napendezwa na Rais Monson kwa ajili ya uhuhuda wake. Ni kama mti mrefu sana wa redwood, lakini hata ushuhuda wa Rais ulibidi ukue na kustawi baada ya muda. Tunaweza kujijulia wenyewe, kama vile Rais Monson alivyofanya, kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu na Mkombozi wa ulimwengu, kwamba Joseph Smith ni nabii wa Urejesho, ikijumuisha urejesho wa ukuhani wa Mungu. Tunashikilia huo ukuhani mtakatifu. Na tujifunze vitu hivi na kujijulia wenyewe ndiyo maombi yangu matakatifu katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.