2025
Msaada kutoka kwa Yesu Kristo: Kwa Nini na Jinsi Gani
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, 2025


Ujumbe wa kila Mwezi wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Aprili 2025

Msaada kutoka kwa Yesu Kristo: Kwa Nini na Jinsi Gani

Elewa kwa nini Yesu Kristo ni jibu na jinsi gani Yeye anavyokusaidia wewe.

Yesu Kristo

Kielelezo na Dan Wilson

“Ninahisi kama ninaendelea kukosea. Ni vigumu kuendelea kujaribu.”

“Hali yangu ni ngumu. Sina uhakika jinsi ya kusonga mbele.”

“Nina mashaka kuhusu siku zijazo. Sijui kama nina kitu kinachohitajika ili kufanikiwa.

“Nimechoka, lakini bado kuna mengi ya kufanya.”

Je, unaweza kujifananisha na tatizo lolote kati ya matatizo haya? Rais Russell M. Nelson amefundisha, “Maswali au matatizo yoyote uliyonayo, jibu daima linapatikana katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo” (“Jibu Daima Ni Yesu Kristo,” mkutano mkuu wa Apr. 2023 [Liahona, Mei 2023, 127]).

Ni rahisi kusema, “Yesu Kristo ndiye jibu.” Inahitaji juhudi kidogo zaidi kuelewa kwa nini na jinsi gani Yeye ni jibu.

Kwa nini Kristo ni Jibu?

Alipovumilia dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Mwokozi alifanya mambo matatu muhimu:

  1. Alishinda kifo, akituruhusu kufufuka.

  2. Alilipa gharama ya dhambi zote, na kufanya iwezekane kwetu kutubu, kukua, na kurudi kwa Mungu. Hiyo pia inatusaidia kuwasamehe wengine wanapotenda dhambi, kwa sababu Kristo alijichukulia dhambi zao juu Yake.

  3. Alipitia maumivu yote, mateso, majaribu, magonjwa, na unyonge (ona Alma 7:11–13). Hiyo inamaanisha Yeye anajua kikamilifu jinsi ya kukusaidia na kukuponya na anaweza kukuimarisha ili uvumilie majaribu na kujitahidi kufanya vyema zaidi.

Chagua tatizo lolote, na unaweza kuunganisha suluhisho nyuma ya moja au zaidi ya kweli hizo tatu.

Umasikini? Kwa sababu Yesu Kristo alipitia mambo yote, Yeye anajua inakuwaje. Yeye sio kwamba daima ataondoa vikwazo, lakini anaweza kuwaimarisha watu wanaobeba mzigo huo (ona Mosia 24:15

Kushindwa? Kwa sababu Kristo alishinda dhambi, kushindwa kwetu hakuhitaji kuwa kwa kudumu. Toba inajumuisha kuboresha na kuwa zaidi ya mtu ambaye Yeye anajua tunaweza kuwa.

Ugonjwa? Kwa sababu alishinda kifo, tutafufuliwa tukiwa na miili mikamilifu yenye kinga dhidi ya magonjwa na maumivu. Kristo pia “[alijichukulia] juu yake … magonjwa” (Alma 7:11), ikimfanya Yeye kuwa mtu mkamilifu ili kutoa faraja na usaidizi.

Ni kwa Jinsi Gani Kristo Husaidia?

Lakini hata wakati tunapojua kwa nini Mwokozi ni jibu (kwa sababu ya yeye ni nani na kile Yeye alichotufanyia), bado tunahitaji kujua jinsi tunavyopata usaidizi na nguvu kutoka Kwake. Hapa kuna mifano michache:

Sala Kwa kusali katika jina la Yesu Kristo, watu wasio wakamilifu kama sisi tunanaweza kuzungumza na Mungu aliye mkamilifu. Tunaweza kuomba kwa ajili ya nguvu tunayohitaji katika hali yoyote, na Mungu atajibu—siyo daima katika njia tunayotaka au kuitarajia, lakini katika njia ambayo itatubariki. Mwaliko wa Mwokozi ni wa kweli: “Ombeni, nanyi mtapata” (Yohana 16:24; 3 Nefi 27:29; Mafundisho na Maagano 4:7).

Kipawa cha Roho Mtakatifu. Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu wana umoja katika dhumuni. Wanafanya kazi pamoja! Wakati wowote unapohisi mwongozo au faraja kutoka kwa Roho Mtakatifu, unaweza kuelewa hilo kama Kristo akikusaidia wewe pia.

Kushika Maagano. Mzee Dale G. Renlund wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amefundisha: “Neno njia ya agano linahusu mfululizo wa maagano ambayo kwayo tunakuja kwa Kristo na kuunganika Naye. Kupitia muunganiko huu wa agano, tunapata kuzifikia nguvu Zake za milele” (mkutano mkuu wa Apr. 2023 [Liahona, Mei 2023, 36]).

Neema. Tunapotumia imani katika Yesu Kristo na kutubu, tunaweza kupokea msaada wa ziada na nguvu (pia inaitwa neema) ili kutimiza mambo ambayo tusingeweza kuyatimiza sisi wenyewe (ona Mwongozo wa Maandiko, “Neema”). Nguvu hii, au neema, inaweza kuja katika njia nyingi: kutoka kwa Roho Mtakatifu, rafiki, mgeni, hisia. Kimsingi, chochote kizuri huja kutoka kwa Kristo (ona Moroni 7:22). Unapopata subira zaidi japo kidogo tu, unapata uwezo zaidi, nguvu zaidi ya kuvumilia, tambua hilo kwamba ni Kristo anakusaidia.

Kumbuka Kwa Nini na Jinsi Gani

Hivyo wakati mwingine unapohitaji jibu la swali au tatizo, mtegemee Kristo. Kumbuka kwamba kwa sababu ya ushindi Wake dhidi ya dhambi, kifo, na changamoto zingine zote za kidunia, hakuna kitu kisichowezekana. Tafuta jinsi gani Yeye anavyoweza kukubariki, na utaona ushawishi Wake katika maisha yako. Yeye anakupenda kwa kina!