Maandiko Matakatifu
Nakala Halisi 2


Nakala Halisi ya Mchoro kutoka Kitabu cha Ibrahimu

Na. 2

Picha
Nakala Halisi 2

Maelezo

Picha 1. Kolobu, ikiashiria uumbaji wa kwanza, karibu sana na selestia, au makazi ya Mungu. Kwanza katika utawala, wa mwisho juu ya kipimo cha wakati. Kipimo kulingana na wakati wa selestia, ambao wakati wa selestia ni sawa na siku moja kwa urefu wa mkono mmoja. Siku moja katika Kolobu ni sawa na miaka elfu kulingana na kipimo cha dunia, ambacho Wamisri hukiita Yah-o-e.

Picha 2. Isimama karibu na Kolobu, huitwa na Wamisri Oliblishi, ambayo ni uumbaji mkubwa wa pili ulio karibu na selestia au mahali Mungu huishi; ukishikilia ufunguo wa mamlaka pia, juu ya sayari nyingine; kama ilivyofunuliwa na Mungu kwa Ibrahimu, wakati alipokuwa akitoa dhabihu juu ya madhabahu, aliyomjengea Bwana.

Picha 3. Imetengenezwa kumwakilisha Mungu, akiwa amekaa juu ya kiti chake cha enzi, amevikwa uwezo na mamlaka; na taji la nuru ya milele juu ya kichwa chake; ikisimama badala ya Maneno Makuu ya Ukuhani Mtakatifu, kama yalivyofunuliwa kwa Adamu katika Bustani ya Edeni, na pia kwa Sethi, Nuhu, Melkizedeki, Ibrahimu, na kwa wale wote ambao Ukuhani huu ulifunuliwa.

Picha 4. Ni sawa sawa na neno la Kiebrania Raukeeyangi, likiashiria eneo pana, au anga la mbingu; pia ni umbo la tarakimu, Kimisri linaashiria elfu moja; sawa sawa na kipimo cha wakati wa Oliblishi, ambayo ni sawa na Kolobu katika mzunguko wake na katika kupima wakati wake.

Picha 5. Katika Kimisri unaitwa Enishi-go-oni-doshi; hii ni moja ya sayari zinazotawala pia, na inasemekana na Wamisri kuwa ndiyo Jua, nalo linaazima mwanga wake kutoka Kolobu kwa njia ya Kae-e-vanrashi, ambayo ni Ufunguo mkuu, au, kwa maneno mengine, nguvu ya kutawala, ambayo hutawala sayari nyingine kubwa kumi na tano au nyota, vile vile pia Floisi au Mwezi, Dunia na Jua katika mizunguko yao ya kila mwaka. Sayari hii hupokea nguvu yake kwa njia ya Kili-flos-is-esi, au Ha-kokaubimu, nyota zilizowakilishwa na nambari 22 na 23, hupokea mwanga kutoka kwenye mizunguko ya Kolobu.

Picha 6. Inaiwakilisha dunia hii katika pembe zake nne.

Picha 7. Inamwakilisha Mungu akiwa amekaa juu ya kiti chake cha enzi, akifunua kwa njia ya mbingu Maneno Makuu muhimu ya Ukuhani; kama vile, pia, ishara ya Roho Mtakatifu kwa Ibrahimu, katika umbo la njiwa.

Picha 8. Una maandishi ambayo hayawezi kufunuliwa kwa ulimwengu; bali yatakuwa katika Hekalu Takatifu la Mungu.

Picha 9. Hayapaswi kufunuliwa kwa wakati huu.

Picha 10. Pia.

Picha 11. Pia. Kama ulimwengu unaweza kuzigundua namba hizi, acha iwe hivyo. Amina.

Picha 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20 na 21 zitatolewa katika wakati wa Bwana utakapofika.

Tafsiri ya hapo juu imetolewa kadiri tulivyokuwa na haki ya kutoa kwa wakati huu.