2023
Mafundisho juu ya Desturi
Desemba 2023


Makala

Mafundisho juu ya Desturi

Jina langu ni Bapont Ngalamulume, ninaishi Kananga, katika Jamhuri ya Kongo ya kati; ningependa kushiriki hadithi kuhusu ndoa yangu pamoja na kila mtu ambaye ataisikia. Siku chache baada ya kurejea kutoka kuhudumu misheni yangu, nilikutana na askofu wangu kumwambia kwamba nilipaswa kurejea Kinshasa ili kuendelea na elimu yangu na kuyajenga maisha yangu. Mwingiliano wa changamoto za baada ya umisionari ulinisumbua mchana na usiku katika kila namna. Askofu wangu alinitazama machoni na kuniambia kwamba ilikuwa muhimu nibakie Kananga, mji nilipokulia na niiimarishe familia yangu ambayo ilijiunga na kanisa punde tu wakati nilipokuwa misheni. Viongozi wangu wa kigingi walinisihi nibakie na niliimarishe Kanisa na nilifanya uamuzi wa kubakia jijini na kuendeleza elimu yangu, kuyajenga maisha yangu na kuhudumu Kanisani. Hii haikuwa rahisi kwangu, kwa upande mmoja nilikuwa na masomo yangu ya kukamilisha na upande mwingine, nilipaswa kuwapatia wadogo zangu wa kiume mahitaji ya mara kwa mara ya kielimu na kumsaidia mama yangu ambaye alikuwa mjane.

Baraka mbili kuu ambazo nilipokea na nina shukrani kwa maisha yangu yote:

  • Ya kwanza kati ya hizi ni programu ya mafunzo ya ufundi inayoendeshwa na idara ya ujenzi ya Kanisa, ambayo ilinisaidia niboreshe ujuzi wangu wa useremala. Kama fundi seremala, nilipata fursa ya kufanya kazi katika nyumba za wamisionari na majengo ya Kanisa, ambapo ningeweza kutoa huduma na kupata pato kutoka kwa wakandarasi.

  • Ya pili ni usaidizi endelevu wa elimu ambao uliniruhusu nimalize masomo yangu ya shahada ya kwanza kabla ya kuweza kulipia masomo yangu ya elimu ya juu mimi mwenyewe.

Wakati wa muhula wangu wa mwisho kama mwanafunzi wa shahada ya kwanza, wakati nikitazama matangazo ya Mkutano wa Eneo la Kusini la Afrika, niliguswa na mafundisho juu ya ndoa na familia na haraka niliamua kufikiria ndoa. Jioni ileile, wakati wa mkutano wa baraza la familia, niliwashirikisha familia yangu kwamba nitaoa. Mama yangu mpendwa na kaka yangu walifurahishwa kwa tangazo hili, lakini nilikuwa bado sijampata mke wangu mpendwa mtarajiwa. Wiki chahce baadaye nilianza kusali na kutafuta mwenza. Baada ya kutafakari na kutafuta sana, nilikutana na msichana aliyeitwa Agnès KAMUANYA, ambaye baadaye alikuja kuwa mke wangu kipenzi wa milele.

Dada huyu alinipenda na mimi nilimpenda. Alikuwa akijitayarisha kuhudumu misheni na nilimuahidi kwamba hatutaanza maisha yetu pamoja hadi pale tutakapooana ndani ya Hekalu Takatifu, jambo ambalo lilimfurahisha zaidi. Wakati huo, Hekalu lilikuwa kwenye ujenzi na hatukujua ni lini lingekuwa tayari kwa sisi kuunganishwa. Lakini tulikuwa tukikabiliwa na changamoto kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na kupata mahari na kuanzisha nyumba. Ili kufanikisha hili, tunahitaji kuwa na miundombinu. Nilimwambia mchumba wangu kipenzi kwamba hakika ninampenda, lakini sina rasilimali muhimu za kulipa mahari. Alijibu kwamba alilifahamu hilo na kwamba tulipaswa kusali ili kufikia matamanio yetu. Alichagua siku ya kufunga ambayo ni Alhamisi na tulifunga kwa lengo la kupata kazi na kufunga ndoa.

Baraka mahususi

Nilipanga siku ya harusi na kuiwekea alama kwenye kalenda ya simu yangu. Wiki chache baada ya mfungo wetu, nafasi mbili za kazi ziliibuka, nilituma maombi na nilifaulu majaribio na usaili na niliajiriwa. Nilisaini mkataba wangu wa miezi sita. Ilinibidi nifanye kazi na niweke akiba ya pesa kutoka kwenye kazi yangu ili kujiandaa na ndoa. Viongozi wangu wa ukuhani walinisindikiza kwa wakwe zangu.

Kuwa katika mchakato wa kuoa, nilitegemea kwamba wakwe zangu wangenipa orodha ya mahari; baba mkwe wangu, aliyemtunza mke wangu kipenzi, alikuwa kiongozi wa Kanisa na wakati familia yangu ilipomwomba orodha, kwa ukarimu alijibu, “Nenda kajiandae na ulete kile utakachopata, hatumuuzi binti yetu”. Mshangao ulioje kwa familia yangu! Tuliandaa mahari na kuipeleka kwa wakwe zetu, na kisha kuandikisha ndoa yetu katika Ofisi ya Usajili wa Raia. Wakati huo, kazi ya ujenzi wa hekalu ilikuwa karibu kukamilika. Tulifunga ndoa na kukaa kwa siku chache katika nyumba za familia zetu za pande zote, tukisubiri kuunganishwa kabla ya kwenda kwenye nyumba yetu mpya kama vile nilivyomwahidi mke wangu kipenzi.

Baba mkwe wangu alipata wakati mgumu kutoka kwa wanafamilia wengine juu ya kwa nini hakutoa orodha ya mahari. Lakini bado kwa ukamilifu alifafanua umuhimu wa ndoa kwa kila mwanafamilia.

Katika kuelekea siku ya harusi, nilichukua pesa niliyokuwa nimeitenga kwa ajili ya sherehe ya harusi na kuielekeza kwenye kwenda hekaluni. Tulifanya uamuzi wa kugharamia safari yetu yote ya hekaluni. Tuliweka miadi hekaluni kwa maandishi na tulisafiri na kufika Kinshasa kukiwa na mvua kubwa. Sikuacha kwa shauku kumwambia mke wangu, “Tunakwenda kwenye nyumba ya Bwana na kutimiza ahadi zetu za ndoa”.

Baraka wakati tukiondoka Hekaluni

Siku ya kuunganishwa kwetu, wakati tukipiga picha na familia, nilipokea malipo ya ghafla kutoka kwa mteja niliyekuwa namdai. Muda mrefu kabla ya kwenda katika Hekalu Takatifu, nilimaliza mkataba wangu na kuomba kazi nyingine. Baada ya kuwa tumeunganishwa, nilialikwa kwenye majaribio ya kazi na usaili, lakini sikuweza kwenda kwani sikuwa na akiba ya ziada kwa ajili ya kupata tiketi ya kurudi.

Siku tatu baada ya kuunganishwa, nilipokea simu kutoka kwa mkuu wangu wa kazi akiniuliza ikiwa nitakuwa tayari kufanya kazi kwenye mradi mpya huko Kamako karibu na mpaka wa Angola. Baada ya sala, mke wangu kipenzi aliniambia kwamba niikubali kazi. Akiba niliyokuwa nayo, ambayo haikuruhusu kupata tiketi ya kurudi nyumbani kwa ndege, ilitosha kugharamia safari yangu kwa basi mpaka kwenye eneo la ajira yangu mpya, bila kufanya jaribio na usaili. Hii iliwezekana kwa rehema ya Bwana. Hivyo kupata kazi bila kupitia usaili ilikuwa ni moja ya baraka ya kwanza iliyopokelewa kutoka katika Hekalu Takatifu.

Kutokana na uzoefu huu nilijifunza kwamba mafundisho ya injili ya Kristo kuhusu ndoa yalikuwa muhimu katika kunisaidia niingie kwenye ndoa kwani niliweka ndoa kuwa kipaumbele ndani ya Hekalu Takatifu kuliko mahari iliyowekwa kwenye orodha. Ilinisaidia nielewe kwamba ndoa si jambo la mjadala kuhusu nini cha kutoa ili kupata mke, bali utiifu wa amri ya Mungu. Nilijifunza pia kwamba Bwana humbariki kila mmoja wetu kulingana na matamanio yetu na imani yetu Kwake.

Leo, ninapotazama baraka za Bwana katika nyumba yetu, watoto wetu wa thamani na familia zetu, ninakumbushwa juu ya ahadi hii, “Bwana Huwaheshimu wale wanaomheshimu Yeye.” Ni ushuhuda wangu kwa kila mvulana na msichana wakati wanapojiandaa kwa ndoa na mwaliko wangu kwa kila mzazi wakati wanapomwozesha mtoto wao, iwe Mtakatifu wa Siku za Mwisho au la, Mafundisho ya Bwana juu ya ndoa lazima yachukue nafasi ya kwanza na yawe mbele ya mila zetu.

Tunampenda Bwana.

Ninampenda mke wangu mrembo wa milele; ninazipenda familia zetu zote za pande mbili na ninawapenda watoto wetu wa milele.