2021
Watakatifu wa Kiafrika: mifano kwa ulimwengu ya upendo, shangwe na imani katika Kristo
Agosti 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Watakatifu wa Kiafrika: mifano kwa ulimwengu ya upendo, shangwe na imani katika Kristo

“‘Tunawashukuru kwa jinsi mnavyoishi maisha yenu, yaliyojawa imani katika Kristo na kwa hamu ya dhati ya kujenga ufalme wa Bwana katika bara hili lililotukuka.’”

Mimi pamoja na mke wangu Jacqui tuliitwa kutumikia Afrika mnamo 2016. Kabla ya kuja, niliomba ushauri kutoka kwa Mzee Carl B. Cook ambaye punde alikuwa amemaliza jukumu lake kama Rais wa Eneo la Kusini mwa Afrika. Alisema kitu cha busara sana ambacho tangu hapo nimegundua ni cha kweli kabisa: “Unadhani kuwa utawafundisha Watakatifu, lakini kiuhalisia watakufundisha wewe.”

Mmetufundisha jinsi ya kusamehe. Katika nchi kama vile Afrika kusini na Rwanda, uzoefu uliopita wa kikatili daima ungeweza kuvijaza vizazi vijavyo kwa chuki na uchungu. Lakini kadiri muda unavyosonga, tumeshuhudia mifano ya kipekee ya waongofu ambao wanaishi mafundisho ya Bwana kwamba tunapaswa “kuwasamehe watu wote”,1 hata wale “wanaowachukia . . . wanaowatumia kwa hila na kuwatesa”.2

Mmetufundisha kiini cha kuhudumu. Na jinsi gani ya kuhudumiana katika wakati wa uhitaji ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Kiafrika. Nakumbuka nikiwa kwenye kikao cha uongozi huko Gaborone, Botswana ambapo programu mpya ya kiwango cha juu na takatifu ya mafundisho ya nyumbani ilikuwa ikitambulishwa na ingeitwa “kuhudumu”. Baada ya hapo nilikuwa nikizungumza na kaka ambaye alisema kwa uso wa mshangao, “Hii inapaswa kuwa rahisi kwetu, kwa kuwa kuhudumu ndicho kitu ambacho kwa uasilia tunakifanya hapa Afrika.”

Mmetufundisha kuhusu utajiri wa kweli. Baadhi yenu mnaishi katika hali zenye mafanikio lakini bado mnabakia wanyenyekevu na mnatumikia kwa uaminifu. Wengine ambao tumekutana nao wanaweza kuhukumiwa na ulimwengu kuwa ni maskini. Lakini ninapofikiria kumbukumbu nyingi muhimu na takatifu za kuwatembelea waumini majumbani mwao na sehemu za kuabudu, ninahisi kama Paulo katika kuelezea kundi hili la siku za mwisho “kama wenye huzuni, bali siku zote wenye furaha, kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.”3

Mmetufundisha kuhusu muunganiko kati ya furaha na kujitoa wenyewe. Nukuu ifuatayo kutoka kwa Mzee Chadambuka, wakati akitumikia kama rais wa misheni ya Botswana/Namibia inaangazia muunganiko huu:

“Nimekuwa na fursa nyingi za kuwatembelea waumini na wachunguzi wa kanisa katika misheni yetu, nikiwa pamoja na wamisionari wazee wanandoa. Uchunguzi mmoja nilioufanya kutokana na kutembelea nyumba hizi, na pia uzoefu wangu kutokana na kuwa mwenyeji na nikiwa na uelewa mkubwa wa tamaduni na mienendo ya maisha ya watu wetu ni [huu]: hali zao zinaweza kuonekana ngumu kwenye kuwa na vitu muhimu ya kimwili, lakini sijawahi kuona watu wenye furaha ambao wana shukrani na wenye kuridhika kwa kile Bwana alichowabarikia. Hata katika hali yao ya umaskini wako radhi kushiriki kidogo walichonacho.

Nimeshuhudia hasa wamisionari wazee wanandoa (kutoka nchi za kigeni), wakitokwa machozi [kwa huruma kwa hali ngumu ya kukoswa mahitaji ya kimwili ya baadhi ya waumini wetu] na mara kwa mara nimebaki nikijiuliza kwa nini wanahisi huzuni hii kubwa kwa watu hawa imara, wenye furaha na wenye kuridhika . . . katika hali halisi mtu mwenye mamilioni ya dola katika mfuko wake hawezi kuwa mwenye furaha namna hiyo.”4

Mmetufundisha kuhusu ushuhuda wa dhati. Katika Jumapili yetu ya Kwanza Afrika, tulihudhuria mkutano wa Sakramenti huko kata ya Protea Glen katika kigingi cha Soweto. Kila hubiri tulilosikia kutoka kwenye mimbari siku hiyo lililenga kwa Kristo na lilijumuisha ushuhuda wa dhati wa Mwokozi na dhabihu Yake ya upatanisho. Tumegundua hili kuwa la kweli tena na tena katika mikutano ya sakramenti kote Afrika. Kama ilivyokuwa kwa Wanefi, inaweza kusemwa kuwahusu ninyi; “tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, tunahubiri kuhusu Kristo . . . ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao.”5

Mmetufundisha umoja. Tunahisi nguvu katika kuwa tofauti, na tunahisi umoja wa kweli kama akina kaka na akina dada wa asili na mbari nyingi tukitumikia bega kwa bega katika ufalme wa Bwana. Kitabu cha Mormoni kwa dhahiri kinafundisha kwamba “wote ni sawa kwa Mungu.”6

Fundisho la kwanza linalofundishwa na wamisionari ni kwamba sisi sote ni watoto wa Baba wa Mbinguni ambalo linamaanisha hasa kwamba sisi ni kaka na dada katika familia ya Mungu. Mtume Paulo alielezea kile kinachotokea wakati tunapokumbatia injili ya Yesu Kristo kwa kusema: “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.”7 na ndivyo ilivyo kwamba mimi na Dada Palmer hatujawahi kuhisi kama wageni au wapitaji miongoni mwa Watakatifu, japokuwa tumetokea nchi za kigeni. Tunajua waongofu wa mataifa na mbari tofauti wanahisi kukubaliwa sawa na huko na hisia ya mjumuisho pale tunapoabudu pamoja na kuhudumiana kwa upendo.

Mmetufundisha kuhusu SHANGWE. Kamwe hatutasahau shangwe kuu ya Watakatifu katika uwekaji wakfu wa mahekalu ya Kinshasa na Durban. Shangwe ya dhati ya wale waliokusanyika huko Harare na Nairobi kusikia kutoka kwa nabii wetu mpya aliyeidhinishwa, Rais Nelson pamoja na Dada Nelson na Mzee na Dada Holland. Shangwe ya Watakatifu zaidi ya 7,000 huko Johannesburg waliomsikiliza Mzee Holland akitangaza kwamba “jibu la kila tatizo katika Afrika linaweza kupatikana kwenye injili ya Yesu Kristo.” Na katika hali ndogo ndogo, shangwe tunayoihisi kutoka kwa waongofu wapya na kutoka kwa wale wanaokwenda hekaluni kwa mara ya kwanza pale wanapojifunga wao wenyewe kwa Kristo katika maagano matakatifu. Rais Nelson alitoa hubiri la kukumbukwa mwaka 2016 lenye kichwa cha habari “Shangwe na Uhai wa Kiroho”. Katika hubiri hilo alitoa neno ambalo lilichoma nafsi yangu nilipokuwa nikitafakari hali ngumu ambazo wengi wa waumini wanajikuta wakikabiliana nazo Afrika. “Shangwe tunayoihisi inahusika kwa kiasi kidogo sana na hali za maisha yetu na inahusika kwa kila kitu na fokasi ya maisha yetu.

Wakati fokasi . . . ikiwa kwa . . . Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi shangwe bila kujali kile kinachotokea—au kisichotokea—katika maisha yetu.”8

Haya ni machache ya vitu tulivyojifunza wakati wa kipindi hiki cha kipekee cha kuishi na kutumikia pamoja nanyi kwa miaka hii mitano iliyopita. Tunawashukuru kwa jinsi mnavyoishi maisha yenu, yaliyojawa imani katika Kristo na kwa hamu hiyo ya dhati ya kujenga ufalme wa Bwana katika bara hili lililotukuka.

Mwisho, ningependa kushiriki uzoefu binafsi wa mwaka jana ambao nauchukulia kama zawadi kutoka kwa Bwana kuja kwenu kupitia nabii Wake aliye hai.

Julai iliyopita, katikati ya janga la ulimwengu, nilibarikiwa kukaa na Rais Nelson na kumuuliza maswali yafuatayo: “Punde nitarudi kwa Watakatifu wetu wapendwa wa Afrika. Je, kuna ujumbe binafsi ungependa kushiriki pamoja nao?” Alitafakari swali hilo vyema kisha alijibu kwa yafuatayo:

“Waambie kwamba baadhi ya vitu viko nje ya uwezo wetu, lakini tunapaswa kufokasi kwenye vile vitu tulivyo na uwezo navyo. Hususan, jinsi tunavyoishi maisha yetu. Tunapaswa kuishi maisha yetu katika hali ambayo daima tuko tayari kukutana na Muumba wetu.”

Maneno haya ya nabii aliye hai ni kwa ajili yako na mimi kwa wakati huu na hali hii. Ninawaalika kutafakari ujumbe huu binafsi na mwaliko kutoka kwa mmoja wa watumishi waliochaguliwa wa Bwana. Ninashiriki hili kwa upendo na kwa ushuhuda wa dhati wa wito mtakatifu wa Rais Nelson kama nabii na mwonaji, ambaye hutufundisha njia ya kusonga mbele hata wakati wa huzuni na mashaka.

Daima tutakuwa na shukrani kwa fursa ya kuwa miongoni mwenu. Tunawashukuru ninyi—Watakatifu waaminifu katika nchi za Maeneo ya Kusini na Kati mwa Afrika—ambao mmetufundisha mengi na ambao daima tutawapenda kama kaka na dada zetu katika Kristo.

S. Mark Palmer aliitwa kama Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2016. Amemuoa Jacqueline Ann Wood; wao ni wazazi wa watoto sita.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 64:10.

  2. Mathayo 5:44.

  3. 2 Wakorintho 6:10.

  4. Ilitolewa wakati wa mkutano na Mzee Bednar na katika barua pepe yake ya ufuatiliaji kuja kwangu mnamo Nov. 2017.

  5. 2 Nefi 25:26.

  6. 2 Nefi 26:33.

  7. Waefeso 2:19.

  8. Russell M. Nelson, “Shangwe na Uhai wa Kiroho,” Liahona, Novemba 2016, 82.