2000–2009
Heri Wote Wenye Moyo Safi
Oktoba 2007


Heri Wote Wenye Moyo Safi

Mungu abariki juhudi zetu za dhati za kuwa safi wa moyo na akili, ili “wema [upate] kupamba mawazo yetu bila kukoma.”

Nikiwa natembea katika ufukwe wa Caribbean asubuhi moja ya jua miaka kadhaa iliyopita, mimi na mke wangu tuliona boti kadhaa ndogo za uvuvi ambazo zilikuwa zimevutwa kwenye mchanga. Tuliposimama kuangalia boti, nilijifunza kitu fulani juu ya uvuvi ambacho sijawahi kusahau. Badala ya kutumia nyavu au ndoano, wavuvi wa eneo hilo walitumia mitego rahisi iliyotengenezwa na waya wenye matundu. Kila mtego ulichongwa kama sanduku. Wavuvi waliweka matundu ya wima yenye urefu wa inchi nane kila upande wa mtego na kisha kukunja nyaya zilizokatwa kuelekea ndani, na kutengeneza nafasi nyembamba ambazo samaki wangeweza kuingia.

Labda unaweza kubashiri ni jinsi gani mtego ulifanya kazi. Wavuvi waliuchukua mtego na kuuweka ndani ya maji. Wakati samaki wa ukubwa wa chakula cha jioni alipokaribia mtego na kuhisi chambo, angeogelea na kuingia ndani ya mtego, aking’ang’aniza kupenya kati ya nyaya zilizokatwa. Halafu, samaki aliyenaswa anapojaribu kuogelea kutoka nje, angegundua kuwa ni jambo moja kupenya kupita nyaya zilizokatwa ili kuingia kwenye mtego, lakini ilikuwa jambo tofauti kabisa kuogelea dhidi ya ncha hizo kali ili kutoka—alikuwa amekamatwa. Wavuvi wanaporudi, wanatoa mtego nje ya maji, na samaki aliyekwama anakuwa chakula cha jioni.

Kuna hadithi katika Agano la Kale kuhusu mtu ambaye alianguka kwenye mtego kama huo. Mtu huyo alikuwa Mfalme Daudi mwenye nguvu, na kile kilichotokea ni moja ya hadithi za kusikitisha katika maandiko.

“Ikawa… wakati wafalme walipokwenda vitani, Daudi alimtuma Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; nao [wakapigana na Amoni]. Lakini Daudi alibaki Yerusalemu.

“Ikawa wakati wa jioni, Daudi aliinuka kitandani mwake, akatembea juu ya dari ya nyumba ya mfalme: na kutoka juu ya paa aliona mwanamke akijiosha; na yule mwanamke alikuwa mzuri sana” (2 Samweli 11:1–2).

Daudi aligundua jina la mwanamke huyo ni Bath-sheba. Mumewe Bath-sheba, Uria, mwanajeshi, alikuwa mbali kupigana na Waamoni na jeshi lililobakia, ambapo Daudi, mfalme wao, alipaswa kuwapo. Daudi aliamuru Bath-sheba aletwe kwenye nyumba ya mfalme. Wakazini, akapata ujauzito, na Daudi akaanza kuogopa uzinzi wao utagunduliwa. Akiwa na matumaini ya kuficha dhambi yake, Daudi aliamuru Uria arudishwe Yerusalemu. Uria alirudi, lakini alikataa kwenda nyumbani kwake kumtembelea Bath-sheba. Ndipo Daudi alipanga Uria auawe vitani (ona 2 Samweli 11:3–17). Mfululizo huu wa maamuzi mabaya ulileta kifo kwa Uria na taabu kwa Daudi, Bath-sheba, na mwishowe ufalme wote. Kwa maneno dhahiri, Biblia inasema, “Jambo alilofanya Daudi halikumpendeza Bwana” (2 Samweli 11:27).

Je, Unaona jinsi Daudi alivyonasa katika mtego huu? Alikuwa juu ya ua wa paa la nyumba yake, na akiangalia chini katika uwanja wa jirani, aliona kitu ambacho hakupaswa kuona kamwe. Huo ulikuwa mtego wa mpinzani. Staha, usafi wa mwili, na uamuzi mzuri ulihitaji kwamba Daudi ageuke mara moja na asiangalie, lakini hakufanya chochote. Badala yake, aliruhusu akili yake igeukie kwa ndoto zilizokatazwa, mawazo hayo yalipelekea matendo, na mambo haraka yaliporomoka toka kwenye mbaya kwenda mbaya zaidi hadi kuleta maafa. Daudi alinaswa, na kwake yeye matokeo yalikuwa ya milele.

Kuna mtego wa kiroho leo unaitwa ponografia, na wengi, wakivutiwa na ujumbe wake wa uchochezi, huingia katika mtego huu wa kufisha. Kama mtego wowote, ni rahisi kuingia lakini ni ngumu kutoroka. Wengine huhalalisha kwamba wanaweza kutazama ponografia bila kudhurika na athari zake mbaya. Wanasema mwanzoni, “Hii sio mbaya sana,” au, “Ni nani Anayejali? Haitaleta tofauti yoyote,” au, “nahitaji tu kujua ni kitu gani.” Lakini wanakosea. Bwana ameonya, “Na yule amwangaliaye mwanamke kwa kumtamani anaikana imani, na hatakuwa na Roho; na kama hatatubu atatupwa nje” (M&M 42:23). Hivi ndivyo ilivyomtokea Daudi: alimwangalia Bath-sheba, akamtamani, na kumpoteza Roho. Jinsi gani maisha ya Daudi yangekuwa tofauti ikiwa angeangalia tu pembeni.

Pamoja na kupoteza Roho, watumiaji wa ponografia pia hupoteza mtazamo na uwiano. Kama Mfalme Daudi, wanajaribu kuficha dhambi zao, wakisahau kwamba hakuna kitu kilichofichika kutoka kwa Bwana (ona 2 Nefi 27:27). Madhara halisi huanza kujilimbikiza wakati heshima ya kibinafsi inapotea, uhusiano mzuri kuwa mchungu, ndoa kuteketea, na wahanga wasio na makosa huongezeka. Wakigundua kwamba kile walichokuwa wakitazama hakiridhishi tena, hugeukia picha mbaya zaidi. Hupata uraibu taratibu hata kama hawajui au wanakana, na kama tabia ya Daudi, tabia zao zinaharibika kadiri viwango vyao vya maadili vinavyoharibika.

Kadiri utamaduni maarufu ulimwenguni unavyozidi kudorora, ukosefu maadili unazidi kusambaa kwenye vyombo vya habari, burudani, matangazo, na mtandao. Lakini umaarufu kulingana na kanuni za ulimwengu ni kiwango hatari sana kutumia kupima kile kilicho sawa au hata ambacho sio hatari. Tamthiliya au kipindi cha runinga kinaweza kujulikana na kupendwa sana na mamilioni ya watazamaji na hata hivyo huonyesha picha na mwenendo ambao ni ponografia. Ikiwa kitu katika tamthiliya “siyo kibaya sana,” hiyo inamaanisha kuwa sio nzuri pia. Kwa hivyo, ukweli kwamba wengine hutazama tamthiliya au kufungua Tovuti ambazo hazifai sio kisingizio kwetu. Maisha ya wenye ukuhani yanapaswa kuiga viwango vya Mwokozi na Kanisa Lake, sio viwango vya ulimwengu.

Bwana alifundisha, “Na heri wote walio na moyo mweupe, kwani watamwona Mungu” (3 Nefi 12:8). Ahadi za injili zinatia moyo na huadilisha, hata kwenye kuinuliwa. Tunapokea ahadi hizo kwa maagano ambayo yamewekwa katika maisha yetu kwa masharti ya usafi na maadili. Tunapoishi vyema na kutafuta kusafisha mioyo yetu, tunasogea karibu na Mungu na Roho. Hali ya moyo wetu huamua ni ushahidi kiasi gani wa uungu tunaouona ulimwenguni sasa na kutustailisha sisi kwa utimilifu wa ahadi kwamba wasafi “watamwona Mungu.” Juhudi zetu ni kutafuta kuwa wasafi. Kwa hivyo, Mtume Yohana aliandika:

“Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa: lakini twajua ya kuwa, atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

“Na kila mtu aliye na tumaini hili kwake hujitakasa kama yeye alivyo safi” (1 Yohana 3:2–3).

Ikiwa tayari umeshikwa na mtego wa ponografia, sasa ni wakati wa kujikomboa kwa msaada wa Mwokozi. Kuna njia ya kutoka, lakini utahitaji msaada Wake kutoroka. Kupona kwako kikamilifu kutategemea toba yako kamili. Nenda kwa askofu wako mara moja. Tafuta mwongozo wake atakaovuviwa. Atakusaidia kuweka mpango wa toba ambao utarejesha kujistahi kwako na kumrudisha Roho maishani mwako. Nguvu ya uponyaji ya Upatanisho wa Bwana Yesu Kristo hufikia shida zote, hata hii. Kama utamgeukia Mwokozi kwa moyo wako wote na kufuata ushauri wa askofu wako, utapata uponyaji unaouhitaji. Mwokozi atakusaidia kupata nguvu ya kupinga majaribu na nguvu ya kushinda uraibu. Kama Moroni alivyofundisha:

“Njoo kwa Kristo, na kushikilia juu ya kila karama nzuri, na msiguse ile karama mbovu, wala kitu kichafu. …

“Ndio, njoo kwa Kristo na mkamilishwe ndani yake, na mjinyime ubaya wote; na ikiwa mtajinyima ubaya wote, na kumpenda Mungu na mioyo yenu, akili na nguvu zenu zote, basi neema yake inawatosha, kwamba kwa neema yake mngekamilishwa katika Kristo” (Moroni 10:30, 32).

Mungu abariki juhudi zetu za dhati za kuwa safi wa moyo na akili, ili “wema [upate] kupamba mawazo yetu bila kukoma” (M&M 121:45). Nashuhudia juu ya upendo wa ukombozi wa Mwokozi na wa nguvu ya utakaso ya Upatanisho Wake katika jina la Yesu Kristo, amina.