2023
Fuata Nuru ya Kweli
Januari 2023


“Fuata Nuru ya Kweli,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2023.

Njoo, Unifuate

Yohana 1:1–5

Fuata Nuru ya Kweli

Nuru ya Kristo daima ipo kwa ajili yako—jana, leo na milele.

Picha
Yesu Kristo

Fikiria Maua ya Kondeni, na Haley Miller

Jua lilipokuwa likizama katika Jumapili nyingine mwaka 1948, nilijikuta nikitembea kando ya Mto Trent huko Nottingham, Uingereza. Nilikuwa mmisionari mwenye umri wa miaka 20 wakati huo. Ilikuwa siku ndefu, ya kuchosha, lakini nilikuwa mwenye furaha na niliyeridhika na kazi.

Nilipokuwa nikitembea kando ya mto, nilisema sala moyoni mwangu. Nikitumaini kupata hisia za mwongozo kutoka kwa Bwana, niliuliza, “Je, ninafanya kile unachotaka Wewe?”

Hisia nyingi za amani na uelewa ghafla zilinifunika. Na katika muda ule ule, nilikuja kujua kwamba Yesu Kristo alinijua na alinipenda. Sikuona ono au kusikia sauti, lakini nisingelijua uhalisia na uungu wa Kristo kwa nguvu zaidi ya hivi hata kama angelisimama mbele yangu na kuniita kwa jina langu.

Kuanzia siku ile hadi leo, kila uamuzi muhimu nilioufanya umekuwa ukiongozwa na ufahamu wangu kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Ninampenda Yeye kwa kina na kwa nguvu zaidi kuliko maneno yanavyoweza kuelezea. Yeye ni Bwana wangu, Mwokozi wangu na Mkombozi wangu na ni rafiki yangu.

Kwa miaka mingi na karibia kote ulimwenguni, nimetoa ushuhuda juu ya Mwokozi. Ninajua Yeye ni kweli na nuru isiyo na mwisho ile “ing’aayo gizani.” (Yohana 1:5). Ni heshima kwetu sisi kuja Kwake, kumfuata Yeye na kuhisi nuru Yake katika maisha yetu.

Ukweli kuhusu Nuru

Kila saa 24, mchana hugeuka usiku na usiku hugeuka mchana. Wakati giza la usiku linapoingia, hatuna hofu na kuogopa kwamba jua limeenda. Tunajua kwamba dunia itazunguka na jua litaangaza juu yetu tena. Yawezekana siyo daima tutaweza kuona au kuhisi nuru, lakini daima ipo.

Hilo pia ni kweli kiroho. Nilikumbushwa juu ya hili miaka mingi iliyopita wakati mimi na mke wangu Barbara, tulipoangalia juu kwenye anga la usiku. Mamilioni ya nyota tulizoziona zilionekana kuwa na uangavu na uzuri usio na kifani. Mawazo yangu kisha yakageuka kwa kustaajabu kwa Yesu Kristo.

Yeye alikuwako “hapo mwanzo pamoja na Mungu” (Yohana 1:2). Chini ya maelekezo ya Baba wa Mbinguni, Yeye aliumba ulimwengu na dunia zisizo na idadi (ona Musa 1:33). Yeye ni nguvu ambayo huvipa nuru jua, mwezi na nyota (ona Mafundisho na Maagano 88:7–10). Yeye ni chanzo cha nuru na uzima wa vitu vyote (ona Yohana 1:3–4; Mafundisho na Maagano 93:10). Yeye alitamka, “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” (Yohana 8:12).

Katika siku yetu, Shetani anafanya kazi masaa ya ziada ili azime nuru ya Mwokozi. Lakini kamwe huwezi kuwa katika mahali penye giza totoro kiasi kwamba nuru ya Yesu Kristo isiweze kukuangazia kama utakuja Kwake. Nuru Yake daima ipo.

Picha
asubuhi, mchana na usiku

Vielelezo na Adam Nickel

Yeye Anaiangaza Njia Yetu

Kama Mwana wa Mungu, Yesu Kristo alikuwa na utukufu pamoja na Mungu Baba “kabla ya ulimwengu kuwako” (Yohana 17:5). Yeye alikuwa mtiifu kikamilifu kwa Baba Yake (ona Yohana 5:30) na kwa hiari akaja duniani. Aliuacha utukufu Wake ili azaliwe katika zizi la ng’ombe mahali ambapo mama Yake “alimvika nguo za kitoto na akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe” (Luka 2:7).

Wakati wa ujana Wake, Yeye “alifanya kazi za Baba [Yake],” (Luka 2:49) na aliwashangaza wale waliosikia mafundisho Yake. Katika huduma Yake, Yeye alikuwa na nguvu ya kufanya miujiza, ya kuwabariki na kuwaponya wagonjwa, kuwarejeshea uhai wafu na mwishowe kuleta Upatanisho usio na mwisho.

Katika kila kitu Mwokozi alichosema na kufanya, hususan dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Yeye ametuonyesha sisi njia ya kwenda kwa Baba yetu wa Mbinguni. Mfano na mafundisho Yake vinaiangaza njia ambayo ni lazima tuifuate ili kurejea nyumbani kwetu mbinguni.

Shiriki Nuru Yake

Mara tunapoihisi nuru ya Mwana wa Mungu katika maisha yetu, tunapaswa kujitahidi kushiriki nuru hiyo kwa wengine. Nilipenda kuwa mmisionari huko Uingereza. Nilipenda kuwa rais wa misheni huko Kanada. Na ninapenda wito wangu wa sasa kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, ambao unaniruhusu mimi kushuhudia juu ya Yesu Kristo ulimwenguni kote.

Mwokozi alifundisha, “Tazama mimi ni mwangaza ambao mtainua—kwamba mfanye yale ambayo mmeniona nikifanya” (3 Nefi 18:24).

Nuru ya Mwokozi inang’aa ndani yetu kila wakati tunaposali na kuyatafuta maneno Yake katika maandiko. Nuru Yake inang’aa tunapopenda kama Yeye anavyopenda, tunaposhiriki shuhuda zetu na kutoa huduma isiyo na ubinafsi. Hii inalifukuza giza nje ya maisha yetu na kuwavutia wengine wanaotafuta nuru Yake.

Picha
msichana pamoja na mvulana akiwa ameshikilia taa

Nuru Yake Inadumu Milele

Nuru ya Yesu Kristo daima ipo kwa ajili yako. Hakuna chochote—hakika hakuna chochote—kinachoweza kuishinda au kuizima nuru Yake. Itadumu milele. Yesu Kristo “ni nuru na uzima wa ulimwengu; … nuru isiyo na mwisho, ambayo kamwe haiwezi kutiwa giza” (Mosia 16:9).

Nina shukurani milele kwa uzoefu niliopata nikiwa mmisionari kijana pale nilipokuja kujua hili mimi mwenyewe. Ninalijua hili kwa uhakika zaidi leo kutokana na uzoefu niliopata katika maisha pamoja na majaribu na shangwe zake zote.

Ikiwa hujui wapi pa kwenda au nini cha kufanya, tazama kwenye nuru ya kweli ya Mwana wa Mungu. Kama uko radhi kuja Kwake na kufuata nuru Yake, Yeye ataiangaza njia yako.