Maagizo na Matangazo
Tangazo la Urejesho


Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo

Tangazo kwa Ulimwengu la Maadhimisho ya Miaka Mia Mbili

Tangazo hili lilisomwa na Rais Russell M. Nelson kama sehemu ya ujumbe wake kwenye Mkutano Mkuu wa 190, tarehe 5 Aprili, mwaka 2020, katika Jiji la Salt Lake, Utah.

Kwa dhati tunatangaza kwamba Mungu anawapenda watoto Wake katika kila taifa la ulimwengu. Mungu Baba ametupatia uzazi mtakatifu, maisha yasiyo linganishika, na dhabihu ya upatanisho isiyo na mwisho iliyofanywa na Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo. Kwa uweza wa Baba, Yesu alifufuka tena na kupata ushindi dhidi ya kifo. Yeye ni Mwokozi wetu, Mfano wetu, na Mkombozi wetu.

Miaka mia mbili iliyopita, katika asubuhi nzuri ya majira ya kuchipua mnamo mwaka 1820, kijana Joseph Smith, akitafuta kujua kanisa lipi ajiunge nalo, alikwenda msituni kuomba karibu na nyumba yake huko kaskazini ya New York, Marekani. Alikuwa na maswali kuhusu wokovu wa nafsi yake na aliamini kwamba Mungu angemwongoza.

Kwa unyenyekevu, tunatamka kwamba katika kujibu sala yake, Mungu Baba na Mwanaye, Yesu Kristo, walimtokea Joseph na kuzindua “kufanywa upya kwa vitu vyote” (Matendo ya Mitume 3:21) kama ilivyotabiriwa katika Biblia. Katika ono hili, alijifunza kwamba kufuatia kifo cha Mitume wa mwanzo, Kanisa la Kristo la Agano Jipya lilipotea duniani. Joseph angekuwa chombo katika kurejeshwa kwake.

Tunathibitisha kwamba chini ya maelekezo ya Baba na Mwana, wajumbe wa mbinguni walikuja kumwelekeza Joseph na kuanzisha tena Kanisa la Yesu Kristo. Yohana Mbatizaji aliyefufuka alirejesha mamlaka ya kubatiza kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Watatu kati ya Mitume kumi na wawili wa mwanzo—Petro, Yakobo, na Yohana—walirejesha utume na funguo za mamlaka ya ukuhani. Wengine pia walikuja, ikiwa ni pamoja na Eliya, aliyerejesha mamlaka ya kuunganisha familia pamoja milele katika uhusiano usio na mwisho ambao unavuka mipaka ya kifo.

Tunaendelea kutoa ushahidi kwamba Joseph Smith alipewa karama na nguvu ya Mungu ili kutafsiri kumbukumbu ya kale: Kitabu cha Mormoni—Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo. Kurasa za maandishi haya matakatifu zinajumuisha simulizi juu ya huduma binafsi ya Yesu Kristo miongoni mwa watu wa Amerika ya Kaskazini na Kusini punde baada ya Ufufuko Wake. Kinafundisha juu ya dhumuni la maisha na kuelezea mafundisho ya Kristo, ambayo ni kiini cha dhumuni hilo. Kama maandiko mwenza ya Biblia, Kitabu cha Mormoni kinashuhudia kwamba wanadamu wote ni wana na mabinti za Baba wa Mbinguni mwenye upendo, kwamba Yeye ana mpango mtakatifu kwa ajili ya maisha yetu, na kwamba Mwanaye, Yesu Kristo, anazungumza leo kama vile ilivyokuwa katika siku za kale.

Tunatamka kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lililoanzishwa mnamo tarehe 6 Aprili, mwaka 1830, ni Kanisa la Kristo la Agano Jipya lililorejeshwa. Kanisa hili limeweka nanga katika maisha makamilifu ya jiwe lake kuu la pembeni, Yesu Kristo, na katika Upatanisho Wake usio na mwisho na Ufufuko wake halisi. Yesu Kristo kwa mara nyingine tena amewaita Mitume na amewapa mamlaka ya ukuhani. Anatualika sote kuja Kwake na kwenye Kanisa Lake, ili kupokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu, na kupata furaha ya kudumu.

Miaka mia mbili sasa imepita tangu Urejesho huu ulipoanzishwa na Mungu Baba na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo. Mamilioni kote ulimwenguni wamekumbatia ufahamu wa matukio haya yaliyotabiriwa.

Kwa furaha tunatamka kwamba Urejesho ulioahidiwa unasonga mbele kupitia ufunuo unaoendelea. Dunia kamwe haitabaki kama ilivyo, kwani Mungu “atavijumlisha vitu vyote katika Kristo” (Waefeso 1:10).

Kwa unyenyekevu na shukrani, sisi kama Mitume Wake tunawaalika wote mjue—kama tunavyojua—kwamba mbingu ziko wazi. Tunathibitisha kwamba Mungu anafanya yajulikane mapenzi Yake kwa wana na mabinti Zake wapendwa. Tunashuhudia kwamba wale wote ambao kwa sala wanajifunza ujumbe wa Urejesho na kutenda kwa imani watabarikiwa kupata ushahidi wao wenyewe wa utakatifu wake na wa lengo lake la kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili ulioahidiwa wa Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo.