Yesu Kristo
Kristo Aliye Hai


Kristo Aliye Hai

Ushuhuda wa Mitume

Tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo milenia mbili zilizopita, tunatoa ushuhuda wetu wa ukweli wa maisha Yake yasiyo linganishwa, na uwezo usio kikomo wa dhabihu Yake kuu ya upatanisho. Hakuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa na mvuto mkubwa kwa wale wote walioishi na watakaoishi duniani.

Alikuwa Yehova Mkuu wa Agano la Kale. Masiya wa Agano Jipya. Chini ya maelekezo ya Baba yake, Yeye alikuwa muumbaji wa dunia. “Vitu vyote vilifanyika [na Yeye] na pasipo Yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.” (Yohana 1:3). Japokuwa hakuwa na dhambi, alibatizwa ili kutimiza haki yote. “Akazunguka huko na huko akitenda kazi njema.” (Matendo 10:38) lakini bado alidharauliwa. Injili Yake ilikuwa ujumbe wa amani na habari njema. Aliwaomba wote wafuate mfano Wake. Alitembea katika barabara za Palestina akiwaponya wagonjwa, akiwafanya vipofu wapate kuona, na kuwafufua wafu. Alifundisha kweli za milele, uhalisia wa uwepo wetu mbinguni kabla ya kuzaliwa katika mwili, madhumuni ya maisha yetu duniani, na uwezekano wa makuzi kwa wana na mabinti wa Mungu katika maisha yajayo.

Alianzisha sakramenti kama ukumbusho wa dhabihu Yake kuu ya upatanisho. Alikamatwa na kuhukumiwa kwa shutuma za uongo, alitiwa hatiani ili kuridhisha matakwa ya kundi la watu wenye ghasia, na akahukumiwa kifo juu ya msalaba wa Kalvari. Aliyatoa maisha yake ili kulipia dhambi za wanadamu wote. Alikuwa ni tunu kubwa aliyejitoa kwa niaba ya watu watakaoishi duniani.

Kwa taadhima tunashuhudia kwamba maisha yake, ambayo yana umuhimu wa kimsingi katika historia yote ya mwanadamu, hayakuanzia Bethlehemu wala hayakuishia pale Kalvari. Alikuwa ni Mzaliwa wa kwanza wa Baba, Mwana Pekee aliyezaliwa katika mwili, Mkombozi wa ulimwengu.

Alifufuka kutoka kaburini na kuwa “limbuko la waliolala” (1 Wakorintho 15:20). Akiwa Bwana mfufuka, aliwatembelea wale ambao aliwapenda wakati wa maisha yake kabla ya kifo. Pia alifanya huduma kwa “wale kondoo wengine” (Yohana 10:16). Yeye na Baba yake walimtokea mvulana Joseph Smith, kuanzisha “kipindi cha wakati mkamilifu” (Waefeso 1:10), kilichoahidiwa tangu zamani.

Kuhusu Kristo Aliye Hai, Nabii Joseph aliandika: “macho Yake yalikuwa mithili ya mwale wa moto; nywele zake zilikuwa nyeupe mfano wa theluji safi, uso wake uling’ara kuliko mng’aro wa jua, na sauti yake ilikuwa mithili ya mvumo wa maji mengi yaendayo kasi, hata sauti ya Yehova, akisema:

“Mimi ndimi wa kwanza na wa mwisho; Mimi ndimi niliye hai, Mimi ndimi niliyeuawa; Mimi ndiye mwombezi wenu kwa Baba” (M&M 110:3–4).

Juu Yake Nabii pia alitamka: “Na sasa, baada ya shuhuda nyingi zilizokwisha tolewa juu yake, huu ni ushuhuda, wa mwisho, ambao tuna utoa juu yake: kwamba yu hai!

“Kwani tulimwona mkono wa kuume wa Mungu, na tulisikia sauti ikitoa ushahidi kwamba Yeye ndiye Mwana Pekee wa Baba—

“Kwamba, kwa yeye, na kwa njia yake, na kutoka kwake, dunia zipo na ziliumbwa, na waliomo ni wana na mabinti wa Mungu” (M&M 76:22–24).

Tunatamka kwa dhati, kwamba ukuhani Wake na Kanisa lake vimerejeshwa duniani—“limejengwa juu ya msingi wa … mitume na manabii, Yesu Kristo mwenyewe akiwa ndiye jiwe kuu la pembeni” (Waefeso 2:20).

Tunashuhudia kwamba siku moja atarudi duniani. “Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote wenye mwili wataona pamoja” (Isaya 40:5). Atatawala kama Mfalme wa Wafalme na atatawala kama Bwana wa Mabwana, na kila goti litapigwa mbele zake na kila ulimi utanena katika kumwabudu. Kila mmoja wetu atasimama kuhukumiwa Naye kulingana na matendo yetu na tamaa za mioyo yetu.

Tunatoa ushuhuda, kama Mitume Wake waliotawazwa rasmi—kwamba Yesu ndiye Kristo Aliye Hai, Mwana asiyekufa wa Mungu. Yeye ndiye Mfalme mkuu Imanueli, ambaye leo anasimama mkono wa kuume wa Baba Yake. Yeye ndiye nuru, uzima, na tumaini la ulimwengu. Njia yake ndiyo njia ile iongozayo kwenye furaha katika maisha haya na uzima wa milele katika ulimwengu ujao. Mungu ashukuriwe kwa zawadi isiyo na mfano ya Mwanawe mtakatifu.

Urais wa Kwanza

Picha
sahihi

Januari 1, 2000

Akidi ya Wale Kumi na Wawili

Picha
sahihi
Picha
sahihi