Maandiko Matakatifu
Mosia 9


Maandishi ya Zenivu—Historia ya watu wake, tangu waondoke nchi ya Zarahemla hadi ule wakati waliokombolewa kutoka mikononi mwa Walamani.

Yenye milango ya 9 hadi 22.

Mlango wa 9

Zenivu aongoza kikundi kutoka nchi ya Zarahemla ili wamiliki nchi ya Lehi-Nefi—Mfalme wa Walamani anawakubalia kurithi nchi—Kuna vita kati ya Walamani na watu wa Zenivu. Karibia mwaka 200–187 K.K.

1 Mimi, Zenivu, nikiwa nimefundishwa kwa lugha yote ya Wanefi, na nikiwa ninajua anchi ya Nefi, au nchi ya kwanza ya urithi wa baba zetu, na nikiwa nimetumwa kama mpelelezi miongoni mwa Walamani kwamba nipeleleze jeshi lao, ili jeshi letu liwashambulie na kuwaangamiza—lakini nilipoona yale yaliyokuwa mazuri miongoni mwao sikutaka waangamizwe.

2 Kwa hivyo, nikabishana na ndugu zangu nyikani, kwani nilitaka mtawala wetu afanye mkataba nao; lakini yeye akiwa mwenye ukali na mtu aliyependa kumwaga damu aliamuru kwamba niuawe; lakini niliokolewa kwa umwagaji wa damu nyingi; kwani kulikuwa na vita kati ya baba kwa baba, na kaka kwa kaka, hadi sehemu kubwa ya jeshi letu likaangamizwa huko nyikani; na tukarejea, wale kati yetu waliopona, katika nchi ya Zarahemla, kuelezea watoto wao na mabibi zao kuhusu ule mkasa.

3 Na bado, mimi nikiwa na uharara mkuu wa kurithi nchi ya baba zetu, niliwakusanya wengi waliotaka kwenda na kuimiliki ile nchi, na tukaanza tena safari yetu ya nyikani kuelekea ile nchi; lakini tulipatwa na njaa na mateso makali; kwani hatukumkumbuka Bwana Mungu wetu.

4 Walakini, baada ya kuzunguka huko nyikani siku nyingi tulipiga hema zetu mahali pale ndugu zetu walipouawa, ambapo palikuwa ni karibu na nchi ya babu zetu.

5 Na ikawa kwamba nilienda tena mjini na watu wangu wanne, kwa mfalme, ili nijue hali ya yule mfalme, na ili nijue kama nitakubaliwa kuingia nchi ile pamoja na watu wangu na kuimiliki kwa amani.

6 Na nikamwendea mfalme, na akaagana na mimi kwamba niimiliki nchi ya Lehi-Nefi, na nchi ya Shilomu.

7 Na pia akaamuru kwamba watu wake waondoke kutoka nchi ile, na mimi na watu wangu tukaingia nchi ile ili tuimiliki.

8 Na tukaanza kujenga majengo, na kurekebisha kuta za mji, ndiyo, hata kuta za mji wa Lehi-Nefi, na mji wa Shilomu.

9 Na tukaanza kulima ile ardhi, ndiyo, kwa kila aina ya mbegu, kwa mbegu za mahindi, na ngano, na shayiri, na nizi, na sheumu, na mbegu za matunda ya aina zote; na tukaanza kuongezeka na kufanikiwa katika nchi ile.

10 Sasa ilikuwa ni ujanja na werevu wa mfalme Lamani, akuwatia watu wangu utumwani, ndipo akaacha nchi ile ili tuimiliki.

11 Kwa hivyo ikawa kwamba, baada ya sisi kuishi katika nchi ile kwa kipindi cha miaka kumi na miwili kwamba mfalme Lamani alianza kuwa na wasiwasi, kwamba watu wangu watakuwa wenye nguvu nyingi katika nchi ile, na kwamba hawangeweza kuwalemea na kuwatia utumwani.

12 Sasa walikuwa watu wavivu na wenye kuabudu asanamu; kwa hivyo walitamani kutuweka utumwani, ili wajikinaishe na jasho la mikono yetu; ndiyo, ili wafanye karamu kwa mifugo ya mashamba yetu.

13 Kwa hivyo ikawa kwamba mfalme Lamani alianza kuwachochea watu wake kwamba wabishane na watu wangu; kwa hivyo kulianza kuwa na vita na mabishano katika nchi ile.

14 Kwani, katika mwaka wa kumi na tatu wa utawala wangu katika nchi ya Nefi, mbali kusini mwa nchi ya Shilomu, wakati watu wangu walipokuwa wanalisha na kunywesha mifugo yao, na kulima mashamba yao, kikundi kikubwa cha Walamani kiliwashukia na kuanza kuwaua, na kuchukua mifugo yao, na nafaka ya mashamba yao.

15 Ndiyo, na ikawa kwamba wale wote ambao hawakupatwa, walitoroka, hadi mji wa Nefi, na wakaniomba ulinzi.

16 Na ikawa kwamba niliwapa silaha kama vile pinde, mishale, panga, na visu, na rungu, na kombeo, na kila aina ya silaha ambayo tungevumbua, na mimi na watu wangu tukaenda kupigana na Walamani.

17 Ndiyo, kwa nguvu za Bwana tulienda kupigana na Walamani; kwani mimi na watu wangu tulimlilia Bwana kwa nguvu ili atukomboe kutoka mikononi mwa maadui zetu, kwani tulikumbushwa kuhusu ukombozi wa babu zetu.

18 Na Mungu aalisikia vilio vyetu na akajibu sala zetu; na tukaendelea kwa nguvu zake; ndiyo, tuliwashambulia Walamani, na kwa mchana mmoja na usiku tuliwaua elfu tatu, arubaini na tatu; tuliwaua hadi tukawafukuza kutoka nchi yetu.

19 Na mimi, mwenyewe, kwa mikono yangu, nilisaidia kuzika wafu wao. Na tazama, kwa huzuni yetu kuu na maombolezo, ndugu zetu mia mbili sabini na tisa waliuawa.