2018
Ile Asubuhi Angavu ya Jumapili
April 2018


Fasihi za Injili

Ile Asubuhi Angavu ya Jumapili

Kutoka katika hotuba ya mkutano mkuu wa Oktoba 2006.

“Katika siku ile, Bwana mfufuka alikata minyororo ya mauti. Aliibuka kutoka kaburini na kutokea kwa ushindi mtukufu kama Mwokozi wa wanadamu wote.

Picha
Mary Magdalene at the tomb

Tunajua Ufufuko ni nini—ni kuunganika tena kwa roho na mwili katika umbo lake kamilifu. …

Je, unaweza kufikiria hilo? Maisha katika kilele chetu? Kamwe pasipo kuugua, kamwe pasipo maumivu, kamwe pasipo kulemewa na magonjwa ambayo mara nyingi hutusumbua katika maisha ya duniani?

Ufufuko ndicho kiini cha imani zetu kama Wakristo. …

… Wakati Mwokozi alipoinuka kutoka kaburini, … Alifanya kitu ambacho hakuna mwingine angeweza kufanya. Alikata minyonyoro ya mauti, siyo tu kwa ajili Yake bali kwa ajili ya wote waliowahi kuishi—wenye haki na wasio haki. …

… Alifanya zawadi hiyo ipatikane kwa wote. Na kwa kitendo hicho adhimu, Alipoza huzuni inayoangamiza, inayoharibu ambayo inatesa mioyo ya wale waliopoteza wapendwa wao wa thamani.

Ninafikiria juu ya jinsi gani Ijumaa ile ya giza ilivyokuwa wakati Kristo alipoinuliwa juu msalabani. …

… Dunia ilitetemeka na kuwa giza. …

Wale watu waovu walioutafuta uhai Wake walishangilia. …

Katika siku ile pazia la hekalu lilipasuka katikati.

Mariamu Magdalena na Mariamu, mama wa Yesu, wote walizidiwa na huzuni. … Mtu mwema sana waliyempenda na kumheshimu alining’inia bila uhai juu ya msalaba. …

… Mitume walikuwa wamevurugwa. Yesu, Mwokozi wao—mtu aliyetembea juu ya maji na kufufua wafu—alikuwa Peke yake mikononi mwa watu waovu. …

Ilikuwa ni Ijumaa iliyojawa na vurugu, huzuni iteketezayo. …

Nadhani kwamba kati ya siku zote tangu mwanzo wa historia ya ulimwengu huu, Ijumaa ile ilikuwa yenye giza kuliko zote.

[Lakini] kukata tamaa hakukudumu kwa sababu Jumapili, Bwana mfufuka alikata minyororo ya kifo. Aliibuka kutoka kaburini na kutokea kwa ushindi mtukufu kama Mwokozi wa wanadamu wote.

Na papo hapo macho ambayo yalikuwa yamejawa na machozi yaliyotiririka bila kukoma yalikauka. Midomo ambayo ilinong’ona sala za huzuni na majonzi sasa ililijaza anga na sifa za kupendeza, kwani Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, alisimama mbele yao kama … uthibitisho kwamba kifo ni mwanzo tu wa maisha mapya na ya kupendeza zaidi.

Kila mmoja wetu tutakuwa na Ijumaa zetu—siku zile ambapo ulimwengu wenyewe huonekana kusambaratika na vigae vya ulimwengu wetu vimesambaa kote vipande vipande. …

Lakini ninashuhudia kwenu katika jina la Yule aliyeshinda mauti—Jumapili itafika. Katika giza la huzuni yetu, Jumapili itafika.

… Bila ya kujali huzuni yetu, Jumapili itafika. Katika maisha haya au yajayo, Jumapili itafika.

Ninashuhudia kwenu kwamba Ufufuko siyo hadithi ya uongo. Tunazo shuhuda binafsi za wale waliomuona. Maelfu katika ulimwengu wa Kale na Mpya walimshuhudia Mwokozi mfufuka. Waligusa vidonda katika mikono, miguu, na ubavu wake. …

Baada ya ufufuko, wanafunzi walipata nguvu mpya. Walienenda kote ulimwenguni … kwa ujasiri wakimtangaza Yesu aliye Kristo, Mwana mfufuka wa Mungu aliye hai.

Wengi wao … walikufa kama mashahidi wa dini, ushuhuda wa Kristo mfufuka midomoni mwao wakati walipotoweka.

Ufufuko ulibadilisha maisha ya wale walioushuhudia. Je, haupaswi kubadilisha yetu?

Sote tutafufuka kutoka kaburini. …

Kwa sababu ya maisha na dhabihu ya milele ya Mwokozi wa ulimwengu, tutakutana tena na wale tuliowapenda.

… Katika siku ile tutashangilia kwamba Masiya alishinda yote ili tuweze kuishi milele.

Kwa sababu ya ibada takatifu tunazopokea katika mahekalu matakatifu, kuondoka kwetu kutoka maisha haya mafupi ya duniani hakuwezi kutenganisha kwa muda mrefu mahusiano ambayo yamefungwa pamoja na kamba zilizotengenezwa kwa viunganisho vya milele.

Ni ushuhuda wangu wa dhati kwamba kifo siyo mwisho wa maisha. …

Na tuelewe na tuishi kwa shukrani kwamba zawadi ya bure ambayo huja kwetu kama wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na kwa ahadi ya siku ile angavu ambapo wote tutafufuka kwa shangwe kutoka kaburini.

… Bila kujali jinsi gani Ijumaa yetu ilivyo na giza, Jumapili itafika.