2018
“Ruka ndani ya Mto!”
April 2018


“Ruka ndani ya Mto!”

Elvin Jerome Laceda

Pampanga, Ufilipino

Picha
mother and baby in a hammock

Kielelezo na Gary Alfonso

Siku moja bibi yangu aliniomba nipeleke chakula alichoandaa kwa shangazi yangu. Ilikuwa ni Jumamosi mchana yenye joto, na kulikuwa na mambo mengine mengi niliyotaka kufanya badala ya kwenda kufanya kazi ya bibi yangu. Nilimwambia amuombe mmoja wa binamu zangu aende badala yangu, lakini alisisitiza kwamba ilipaswa kuwa mimi.

Saa moja ilipita, na nilianza kuhisi kwamba nilipaswa kufanya kile bibi alichoniomba nifanye. Nilichukua kile chakula na kushika njia kuelekea nyumbani kwa shangazi yangu. Ilikuwa mbali sana, na nilipofika, sikuwa nimepanga kukaa muda mrefu.

Nilimkuta shangazi yangu na mtoto wake mwenye umri wa miezi mitano kwenye kitanda cha bembea kilichofungwa kwenye miti miwili midogo ya miembe. Miti hiyo ilikuwa kando ya mto ambao ulitiririka nyuma ya nyumba. Nilitembea kuwaelekea wao ili kufikisha chakula. Ghafla, kamba za kitanda cha bembea zilikatika. Shangazi yangu na mtoto walibiringika mtoni. Hofu ilinishika. Sikujua jinsi ya kuogelea, na hakuna aliyekuwepo karibu kusaidia. Sikujua cha kufanya.

Kwa haraka, nilisikia sauti ya Roho: “Ruka ndani!”

Bila kufikiri mara mbili, niliruka. Kwa bahati nzuri, nilimpata mtoto ndani ya sekunde chache, na shangazi yangu aliweza kutoka nje ya maji. Nilipotoka nje ya maji na mtoto mchanga, sikuamini kile kilichokuwa kimetokea. Niliruka ndani ya mto wakati sikujua jinsi ya kuogelea, lakini kwa sababu nilimsikiliza Roho, mimi na binamu yangu mdogo tuliokolewa hatukuzama.

Niligundua jinsi gani ilivyo muhimu kutambua na kusikiliza maelekezo na mwongozo wa kiungu ambao Mungu hutupatia kupitia Roho Mtakatifu Ninashukuru kwamba hatimaye nilifanya kile ambacho bibi aliniomba na kupeleka chakula kwenye nyumba ya shangazi yangu. Ninajua lazima tufanye jitihada kuwa wepesi kusikia ushawishi wa kiroho ili tuweze kuwa mikono ya Mungu katika kuwasaidia watoto Wake.